Rais wa Shirikisho la Soka nchini, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa wanashikiriwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na wapo katika Kituo cha Polisi Salander Bridge ili kupisha uchunguzi dhidi yao.
Tukio hilo limethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Takukuru, Mussa Misalaba alipokuwa akihojiwa na kituo cha Radio EFM leo. Misalaba amesema ni kweli wanawashikilia na taarifa zaidi wataitoa baada ya kumaliza uchunguzi wao.
Licha ya kuwa tuhuma zinazowakabili hazijawekwa wazi, lakini mwezi uliopita ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliripoti kuhusu mabilioni ya shilingi yaliyobainika kuchotwa kwenye akaunti za TFF na kulipwa kwa wadau wa soka kinyume cha sheria.
Miongoni mwa waliotuhumiwa kunufaika na fedha hizo ni Rais wa TFF, Jamal Malinzi na aliyekuwa msaidizi wake, Juma Matandika.
Wengine ni aliyekuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka (FAT sasa TFF), Michael Wambura na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayubu Nyenzi.
Gazeti la Nipashe lilieleza kubaini kuwa, mkutano mkuu wa wanachama wa TFF uliofanyika Desemba 2011 uliidhinisha Kampuni ya Ukaguzi ya TAC kuwa mkaguzi wa hesabu za shirikisho kwa miaka mitano kuanzia mwaka ulioishia Desemba 31, 2011.
Ripoti ya ukaguzi wa kampuni hiyo inaonesha kuwa, katika kipindi cha kuanzia Agosti 15, 2014 hadi Septemba 30, 2015, TFF ililipa jumla ya Sh. milioni 274.072 kwa Wambura na kampuni za Punchlines (T) Ltd na Artriums Dar Hotel Ltd bila kuwa na nyaraka stahiki.
Pia, ripoti ya ukaguzi maalum wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa timu ya taifa (Taifa Stars) iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inabainisha matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi miongoni mwa baadhi ya watendaji wa TFF.
Katika ripoti hiyo inaelezwa kuwa, kuanzia Novemba 13, 2013 hadi Februari 15, 2014, jumla ya dola za Marekani 315,577 (sawa na sh. milioni 688.368) zilichotwa kwenye akaunti ya fedha za udhamini wa TBL kwa Taifa Stars na kutumika kinyume cha makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa shirikisho na kampuni hiyo.
Inaelezwa pia kwenye ripoti hiyo kuwa kuanzia Novemba 11, 2013 hadi Machi 11, 2014, jumla ya dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaanishwa katika mkataba wa TBL na TFF.
Miongoni mwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kutumia kinyume fedha hizo ni Malinzi, Matandika, Ali Ruvu, Nyenzi, Ally Mayay, Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara, Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen.
Ripoti ya ukaguzi wa TAC inaonesha Wambura alilipwa jumla ya Sh. milioni 67.5, Punchline (T) Ltd ililipwa Sh. milioni 147.154 na Artriums Dar Hotel Ltd ililipwa Dola za Marekani 28,027 (Sh. milioni 59.417).
Aidha, ripoti hiyo inaonesha malipo ya maelfu hayo ya Dola kwa Artrium yalifanyika siku moja ya Machi 4, 2015 kwa TFF kuandika vocha nne zenye namba 001467, 001468, 001469 na 001470, tatu zikiidhinisha malipo ya Dola 9,000 kila moja wakati moja ikiidhinisha malipo ya Dola 1,027.
Katika ripoti hiyo, inaelezwa kuwa timu ya ukaguzi ilibaini malipo kwa wadau hao wa soka yalifanyika bila idhini ya Kamati ya Utendaji ya TFF.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni