Jumatatu, 10 Aprili 2017

KINYESI CHA BINADAMU CHAZALISHWA NJOMBE KUBORESHA MAZAO SHAMBANI


 Sehemu ya choo kinachoonyesha namna ya kuvuna
 kinyesi tayari kwa mbolea shambani

Na Michael Katona, Njombe

WAKATI jamii nzima ikielewa kwamba kinyesi cha binadamu kina madhara makubwa kwa afya ya binadamu, Shirika la SHIPO lililopo mkoani Njombe lenyewe limekuja na mtazamo mwingine kwa kuzalisha kinyesi cha binadamu kuwa mbolea ya kuotesha mazao shambani.

“Kinyesi kibichi cha binadamu kina athari kubwa kwa mwanadamua, lakini kinyesi kilichokauka vimelea haviwezi kuota, hilo ndiyo sababu tunasema kikisha kauka, kinyesi kinaweza kuwa ni mbolea nzuri,” anasema Venance Lulukila, Afisa Maendeleo ya Jamii.


“…Hatushauri kinyesi kibichi kitumike au kiwe kinakaribiana na vinywa vya binadamu au vyakula, ieleweke kinyesi cha binadamu kikiwa kibichi kinashida.  Lengo lake ni kuwawezesha wana jamii waweze kupata mbolea ambayo inapatikana kupitia binadamu mwenyewe,” anasema Lukulila.

Anasema katika hicho choo walichobuni, kina mifumo miwili ambayo inawezesha kukausha mbolea hiyo kwa kipindi cha miezi sita mara baada ya binadamu kujisaidia.

“ Hicho choo kina chemba mbili, ukishajisaidia chemba ya kwanza, unafunga hiyo chemba iliyojaa, unafungua chemba ya pili na kuanza kujisaidia, baada ya miezi sita ile chemba ya kwanza inakuwa tayari imekauka na hivyo unapakua mbolea yako vizuri unapeleka shambani,” alisema Lulukila. 

“…tumeanzisha hivi kwa kusaidia zile familia sizokuwa na watoto wasiozidi watano, usije ukajenga hiki choo katika nyumba ya kupangisha,” anasema.

Naye Julius Njunwens ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika shirika hilo, anazungumzia choo hicho cha kisasa walichokibuni kuwa, haitakiwi kuchimbwa shimo refu kama ilivyozoeleka katika uchimbaji wa vyoo vingine.

“Ni vigumu kuchimba kwenda chini, kwa kawaida vyoo inabidi uchimbe kuanzia mita 3 kwenda chini, kwa hiyo kama kuna mwamba mgumu huwezi kuchimba choo kwa kwenda chini zaidi, lakini pia maeneo yenye ufinyu wa ardhi huwezi ukawa unachimba choo kila mwaka,” anasema  Njunwens.

“…kwa vyoo vinavyohitaji kupakuliwa na kuna makazi holela, huwezi ukapitisha gari la kuzoa maji taka au kufika maeneo husika, lakini kwa kutumia hiki choo unaweza ukapakua mbolea na kuweza kutupa kama huwezi kutumia shambani,” anasema.

Wakati jamii ikiona kinyesi cha binadamu ni hatari kwa afya ya binadamu, utafiti uliofanywa na baadhi ya madaktari wamebainisha kuwa kinyesi cha binadamu ni tiba kwa afya ya binadamu.

Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni, madaktari wameeleza kuwa kinyesi cha binadamu kinaweza kuwa tiba pindi binadamu akala kinyesi hicho.

Inashauriwa na wataalamu wa afya kuwa iwapo mgonjwa ataugua ugonjwa unaofahamika kwa lugha la kiingereza “Ulcerative colitis” unaosababishwa na vijidudu aina ya Cdifficile vinavyosababisha binadamu kuugua ugonjwa wa kuhara sana zaidi ya mara arobaini kwa siku.

Ugonjwa huu unasababishwa katika utumbo mkubwa wadudu hao hushambulia, chanzo kikiwa ni utumiaji wa hovyo wa dawa kali za Antibiotics kwa kipindi kirefu ambazo huua wadudu wazuri na kufanya wadudu wabaya kuongezeka na hatimaye kuleta madhara ya kuhara sana.

Katika kutibu ugonjwa huo, madaktari wameeleza kuwa dawa kuu ni kumpa mtu anayeugua ugonjwa huo kinyesi cha binadamu chenye wadudu wazuri wakutosha.

Kabla mgonjwa hajapewa dawa hiyo, kinyesi chake kwanza hupimwa kuhakikisha hana magonjwa kama maambukizi ya virusi vya ukimwi n.k.

Baada ya kufanya hivyo, ndipo kinyesi hicho huchukuliwa na kusagwa kwenye mashine, halafu mgonjwa hupewa kwa njia ya mrija puani au mrija kwenye tundu la haja kubwa. 

Wakati hilo likifanyika kwa mtindo huo, nchini Uingereza, wataalamu pia wametumia kinyesi cha binadamu kama ni nishati mbadala inayoweza kusaidia basi kutembea.

Nchini humo, wataalam hao hivi karibuni walitumia kinyesi cha binadamu na mabaki ya vyakula vibovu kuanza kutembea barabarani.

Basi hilo lenye uwezo wa kuchukua watu  40 liitwalo "Bio-Bus" linatumia gesi ya  biomethane inayotokana na vyakula vibovu na maji taka pia. Basi hilo linalozingatia masuala ya mazingira linaweza kusafiri hadi kilomita 300 katika tangi moja la gesi, linalochukua takriban kinyesi cha watu watano kuzalisha kwa mwaka.


Meneja wa Kampuni ya GENeco, Mohammed Saddiq alisema magari  yanayotumia gesi yana wajibu mkubwa wa kuimarisha hali bora ya hewa katika miji ya Uingereza lakini Bio-Bus linavuka mipaka zaidi na linapata nishati yake kutoka kwa watu wanaoishi eneo hilo, wakiwemo bila shaka wanaopanda basi hilo.”


Si nishati hiyo tu ya kuweza kutumiwa katika usafiri, bali Kinyesi kwa upande mwingine hivi sasa kinatumika kama ni maji safi na salama bila kuleta madhara yoyote.

Hivi karibuni Tajiri na mmliki wa kampuni ya Microsoft Corporation, Bill Gates aliweza kuuthibitishia ulimwengu kwamba haogopi kuwekeza pesa yake kwenye biashara yoyote Duniani.

Gates kaamua kugeukia huu mradi wa maji safi ya kunywa ambayo yametengenezwa kutokana na kinyesi cha binadamu huku mikakati yake ikiwa ni kusambaza mitambo hiyo katika nchi mbalimbali maskini ikiwemo Senegal muda mfupi baada ya majaribio yake kukamilika.

Tayari Teknolojia hiyo imeungwa mkono na shirika la WaterAid ambalo limesema kuwa litasaidia sana katika maeneo ya mengi yenye ukame ambapo kulingana na shirika hilo watu millioni 748 hawana maji safi ya kunywa.

Maoni 1 :