Basi la Mwafrika lililopata ajali mbaya
eneo la Kibena mkoani Njombe
Na Michael Mapollu, Njombe
Basi la Kampuni ya Mwafrika jana lilipinduka na kujeruhi
abiria 32 ambao wamelazwa katika hospitali ya Kibena iliyopo mkoani Njombe
baada ya kulikwepa basi la Super Feo lisigongane uso kwa uso.
Basi hilo lililikuwa likitoka wilayani Makete kwenda Iringa,
ambapo ajali hiyo ilitokea saa 4:30 asubuhi katika eneo la kiwanda cha chai cha
Kibena km 20 kutoka stendi kuu ya mjini Njombe lililopokuwa limesimama kushusha
abiria.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo waliozungumza walisema
chanzo cha ajali hiyo kilitokana na dereva wa basi la Mwafrika kulikwepa basi
la Super Feo lililokuwa likipishana na trekta la kiwanda cha Chai ambalo
lilikuwa likitoka kubeba majani ya chai.
Habari zilizopatikana kwenye eneo la tukio la ajali hiyo
zilidai dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo alifahamika kwa jina la Furaha
Sanga ambaye alikimbia mara baada ya ajali hiyo kutokea, na kwamba basi hilo
lilikuwa na zaidi ya abiria 50.
Akizungumza ofisini kwake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kibena,
Dk. Patrick Msigwa alithibitisha hospitali hiyo kupokea majeruhi hao, ambapo
wanawake walikuwa 16 na mawaume ni 15.
Dk. Msigwa aliwataja majeruhi hao ambao kati yao wamepata
majeraha madogo madogo na wengine wakiwa wamevunjika viungo kuwa ni Eva
Mligilwa (37) kutoka Ilambibole, Monica Kyando (61) mkazi wa Ikonda, Adela
Mligo (12) mkazi wa Luponde, Winfrida Sanga (21) mkazi wa Ikonda, Rose Makweta
(48) mkazi wa Ikonda, Martha Ngalau (30) mkazi wa Ikonda, Beatrice Fute (42)
mkazi wa Ilambilole, Imara Irima (60) mkazi wa Ikonda, Safina Chaula (23) mkazi
wa Makete na Daniel Daniel (27) mkazi wa Ikonda.
Wengine ni Pendo Bernado (62) mkazi wa Ikonda, Prisca Sanga
(20) mkazi wa Mang’oto, Anna Sanga (28) mkazi wa Igola, Maria Sanga (37) mkazi
wa Bulongwa, Mwale Lumbilo kutoka Igilamelewa, Erica Mwihuta (31) kutoka
Mafinga na Jane Chengula (49) kutoka Makngarawe.
Dk. Msigwa aliwataja majeruhi wengine waliopata ajali hiyo
kuwa ni Ambwene Mbilinyi (15) mkazi wa Ikonda, Rajab Sanga (24) mkazi wa Mbeya,
Jeremiah Njeri (62) mkazi wa Mafinga, Betwel Sanga (30) mkazi wa Mbeya, Beni
Lyalimi (40) mkazi wa Mhaji, Aidan Sekreji (71) mkazi wa Masisiwe, Victory
Lupala (39) mkazi wa Isimila, Benito Ziku (22) mkazi wa Iringa, Mlende Chengula
(29) mkazi wa Iringa, John Njasi (60) mkazi wa Mafinga, Onesmo Mkiwa (32) mkazi
wa Mafinga, Isaya Lukulumbika (28) mkazi wa Mbalali, Hongela Lauli (32) mkazi
wa Iruyo, Linus Matofari (30) mkazi wa Makete, Benedict Sanga (47) mkazi wa
Mang’oto.
Alisema katika ya majeruhi hao, Sekreji ndiye hali yake iko
chini ya uangalizi wa madaktari kutokana na kuvunjika mkono.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Linus Matofari akizungumzia
chanzo cha ajali hiyo, alisema imesababishwa na harakati za dereva wa basi la
Mwafrika namba T726AGA kutaka kulikwepa basi la Super Feo, ambalo lilikuwa
limejaribu kulipita trekta la kiwanda cha chai Kibena.
Abiria alisema dereva wa basi hilo alikuwa katika mwendo wa
kawaida tangu walipotoka kwenye Stendi ya mabasi ya mjini Njombe kuelekea na
safari mkoani Iringa.
Kufuatia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe,
Fulgence Ngonyani jana alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza hakuna
abiria yoyote aliyepoteza maisha. Kamanda Ngonyani alisema ajali hiyo ilitokea
majira ya saa 4: 30 asubuhi na kwamba dereva Furaha Sanga amekamatwa na chanzo
cha ajali bado kinachunguzwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni