Na Mwandishi Wetu, Makambako
Ni kelele za shangwe
zilizokuwa zikisikika usiku wa Jumamosi Agosti 2, 2014 baada ya wasikilizaji, mashabiki
na wapenzi mbalimbali wa redio Ice FM iliyopo katika Halmashauri ya Mji Makambako
wakati ilipokuwa ikifanya sherehe ya kutimiza mwaka mmoja tangu ilipoanza
kurusha matangazo yake rasmi.
“Tupo hapa kusherehekea
mafanikio makubwa yaliyofanywa na Ice FM redio, ni wachache wanaweza kuanzisha
redio na hatimaye kusimama kwa muda mrefu kama hii redio mbayo inatimiza mwaka
mmoja leo tangu ilipoanza kurusha matangazo yake mjini Makambako,” alisema Regina
Mwanyika mkazi wa Makambako.
Ice FM radio inarusha
matangazo yake kupitia masafa ya 99.3 kutoka mjini Makambako, mwishoni mwa wiki
ilifanya sherehe kubwa katika uwanja wa mpira wa miguu wa Amani Makambako na kujipongeza,
huku ikiwatambulisha rasmi watangazaji wake ambao wamekuwa ndiyo chachu ya
kufanya redio hiyo isimame hapo ilipofika hivi sasa.
“Sikiliza ndugu mwandishi,
nawapongeza sana hawa jamaa wa hii redio, hasa Mkurugenzi wake McDonald na timu
nzima ya watangazaji, wako makini sana, wanaweza kuwa namba moja hivi sasa hapa
Mkoani Njombe, kutokana na redio yao hii kuwa na matangazo bora sana, ” alisema
Ally Mwakyusa.
Katika sherehe hiyo, burudani
mbalimbali zilikuwepo uwanjani ikiwa ni pamoja na kundi maarufu mkoani Njombe
la Makhirikiri kutoka wilayani Makete.
Mbali ya kundi hilo, pia
msaanii maarufu Sam wa Ukweli kutoka jijini Dar es Salaam naye alitoa burudani
yake na hivyo kunogesha sherehe hiyo kabambe iliyovuta maelfu ya mashabiki
uwanjani hapo.
Hakika katika sherehe,
hakukosi burudani za kila aina, kwani mbali na burudani za muziki, vilevile
kulikuwa na mchezo wa kukimbiza kuku, mpira wa soka na mchezo wa ngumi.
Katika mchezo wa soka, timu
ya Ice Fm na Uhamiaji zilichuana vikali katika uwanja wa Amani na matokeo
yalikuwa 2-0 baada ya Ice Fm kukubali kichapo kutoka Uhamiaji.
Wakati kwenye mchezo wa
ngumi, Mkurugenzi wa Ice Fm Radio, Mc Donald alipigana na DJ Jose ambaye ni
mtangazaji wa redio hiyo, lakini katika mchezo huo wa raundi tatu, matokeo
yalikuwa sare baada ya kila mmoja kuangushwa chini mara mbili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni