Somo lolote lenye namba kama hisabati, kwa miaka mingi, litaendelea kusumbua, siyo tu wanafunzi darasani, bali pia watu wazima, baadhi wakiwa ni viongozi.
Eti Kigawe Kidogo cha Shirika (KDS) jawabu lake huwa namba kubwa. Mfano, KDS ya 24, 32 eti ni 96; kwa nini isiwe 8? Na KDS ya 18, 27 eti ni 54; kwa nini isiwe 9?
Lakini Kigawe Kikubwa cha Shirika (KKS) jawabu lake huwa namba ndogo. Mwanafunzi akiambiwa atafute KKS ya 12 na 30 njia atakayotumia ni kupata vigawe vya 12 ambavyo ni 1, 2, 3, 4, 6 na 12 kisha vigawe vya 30 ambavyo ni 1, 2, 3, 5, 6, 10, 15 na 30. Jibu ni kwamba KKS ya 12 na 30 ni 6. Haya ndiyo maajabu yake.
Hesabu zinachanganya. Mfano, ikiwa watu 20 wanatumia kilo moja ya sukari kwa siku mbili (2), je, watu 40 watatumia kilo moja ya sukari kwa siku ngapi? Jawabu ni rahisi eeeeh! Lakini hesabu hiyo hiyo ikigeuzwa, kwamba mashine 250 za BVR zina uwezo wa kuandikisha watu wa mkoa mmoja kwa miezi miwili, je, mashine hizo zitatumia siku ngapi kuandikisha watu katika mikoa 30?
Maana, kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2012, Mkoa wa Njombe una watu 702,097 na nusu yao wana sifa ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Huko ndiko ambako tangu Februari 23 mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inahangaika kuandikisha wapigakura walau 300,000.
Hadi Jumatatu iliyopita ikiwa ni mwezi kamili, NEC ilikamilisha uandikishaji katika kata za mji wa Makambako tu na baadhi ya kata katika Wilaya ya Njombe.
Sasa, NEC itafanya miujiza gani ili Daftari la Kudumu la Wapigakura liwe limekamilika kwa ajili ya kupiga kura ya maoni ifikapo Aprili 30? Tupige hesabu.
Mashine moja ina uwezo wa kuandikisha watu wasiozidi 100.
Kwa hiyo, mashine 250 zikifanya kazi, kila moja ikaandikisha wastani wa watu 100 tu kwa siku, zitaandikisha watu 25,000. Hivyo basi, kwa siku saba zitakuwa zimeandikisha watu 175,000. Safi.
Taarifa ya NEC inaeleza kasi ya uandikishaji iliongezeka kutoka watu 4,300 kwa siku hadi 6,000.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, watu 58,000 waliandikishwa Makambako na Njombe 45,000.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni