Historia na Urithi

Kimondo: Maajabu mengine ya Mungu yaliyotokea Mbozi


Na Mwandishi Wetu

Nikipi kinachoshindikana kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, kuweza kubuni na kuvuta hisia za Watanzania na Watalii wenye hamu ya kutaka kujifunza mambo mbalimbali ya vivutio hapa nchini?

Bila shaka hilo linaweza kuwa moja kati ya maswali wanayojiuliza wananchi wachache wanaotembelea eneo la mlima Marengi lililopo wilayani Mbozi mkoani Mbeya kwenda kushuhudia hazina kubwa iliyoshuka kutoka angani yenye ukubwa wa tani 16 mwaka 1930.

Ni umri wa mtu aliyekula chumvi nyingi hivi sasa, tangu hazina hiyo ishuke kutoka angani na kuangukia katika eneo hilo la milima ya Nyanda za Juu kusini. Ni zaidi ya miaka 1,000 iliyopita hivi sasa tangu hazina hiyo ya Kimondo kushuka kutoka angani ilipoonekana kwa mara ya kwanza, baada ya Mwananchi mmoja . W. H. Nott, soroveya kutoka Johannesburg, ambaye aliandika kwenye kitabu chake kuwa mnamo Oktoba 1930 alipotembelea eneo hilo aliona kuanguka kwa Kimondo hicho.

Lakini kugunduliwa kwa kimondo hicho, bado hakina ushawishi mkubwa kwa watanzania ama watalii wanaotaka kufahamu eneo na kutembelea eneo hilo ambalo limetengwa kama sehemu ya kivituo kikubwa cha kuingiza mapato katika wizara ya Maliasili na Utalii hapa nchini.

Bado hakuna utambuzi wowote unaoonyesha kuwa kuna eneo hilo muhimu la kujionea historia kubwa ndani ya Tanzania, licha ya kuonekana kama ni sehemu ya kawaida sana na isiyo kuwa na mvuto wa kuvutia kwa wageni wanaopenda kutembelea sehemu za vivutio kama hivtyo.

Tofauti iliyopo,licha ya Tanzania kupata bahati hiyo ya kuanguka kwa Kimondo hicho chenye ukubwa wa Tani 16, na kuwa ni kimondo cha sita kwa ukubwa duniani, lakini ajabu kubwa ni namna ambavyo kilivyoachwa kunakuwa na sehemu ya kawaida sana, ikiwa ni tofauti kubwa sana na kama ya Namibia iliyopo kwenye bara la Afrika walivyoweza kutumia hazina hiyo kuonyesha mvuto wa kipekee na kuwafanya wageni mbalimbali kutembelea sehemu hiyo.

Kimondo cha Mbozi kinaweza kuwa ni mfano mkubwa na chenye kutia chachu ya mapato yatakayoisaidia serikali ya Tanzania, lakini mazingira yalivyowekwa bado hayavutii na kutoa mwanya kwa wananchi wengi kutoshawishika kutaka kutembelea na kujionea hazina hiyo ya Taifa.

Vimondo vingi vinavyoingia katika anga ya dunia huungua kabisa kabla ya kufika duniani. Wakati mwingine vipande vingine vya mawe au chuma hustahimili joto jingi nakufanya kufika duniani. Hata hivyo vipande vingi huwa vidogo, lakini vingine vina uzito wa tani nyingi.

Katika kuthibitisha hilo, Kimondo kinachoelezwa kuanguka barani Afrika ni kule kilichopo nchini Namibia ambapo kilianguka kikiwa na uzito wa tani 60 na kwamba asilimia 90 ya kimondo hicho ni chuma.

Kwa upande wa kimondo cha Mbozi, chenyewe kina urefu wa mita tatu, upana mita moja, na uzito wa tani 16, huku asilimia 90 kikiwa ni chuma, asilimia tisa ikiwa ni nikeli pamoja na kuwa na kobalti, shaba, salfa na fosforasi.

Ukipita katika maeneo ya mlima Marengi huwezi kuelezwa wala kumkuta mtu anayefahamu ni siku gani kilianguka, zaidi ya kukueleza kwenye miaka ya 1930 ndipo kilielezwa kuonekana kwenye sehemu hiyo.
Hata hivyo, ajabu ambayo bado inajionyesha ilipoangukia kimondo hicho ni namna udongo ulivyosambaa, huku ukiongezewa kuchimbwa kwa ajili ya kuweka muonekano mzuri.

Wapo watu waliotembelea kimondo hicho kutaka kukata sehemu ya kiondo hicho ili kujiwekea kumbukumbu, lakini ilishindikana sana, kwani mnamo Desemba 1930 raia mmoja aliyetembelea sehemu hiyo D.R. Grantham wa chama cha Jiolojia alithubutu kutumia msumeno kukata eneo hilo la ukubwa wa sentimita kumi lakitini alishindwa.

Licha ya Tanzania kuhimiza wananchi wake kujenga tabia ya kutembelea sehemu za vivutio, lakini ukitembelea eneo hilo la Mbozi, kwa ajili ya kujionea kimondo hicho, bado hakuna alama zenye kuonyesha kuna sehemu ya kwenda kujionea kivutio hicho.
Ingekuwa ni vyema wahusika wanaoshughulika na shughuli za kutangaza vivutio vya kitalii nchini wakaiga na kujifunza kutoka nchi za wenzetu namna wanavyothamini kutunza hazina hizo za Taifa.

Nchini Namibia katika kijiji cha Otavi kikiwa umbali wa kilometa 123 kutoka mji wa Otjiwarongo ukifika katika eneo hilo bila shaka hakuna asiyepingana na mimi namna walivyoweza kubuni na kutunza eneo ilipoanguka kimondo  cha uzito wa tani 60, ambapo endapo utatembelea eneo hilo  ni dhahiri utafikiri ni uwanja wa mpira au kiunga fulani kilivyojengwa kwa ustadi mkubwa kuweza kuvutia wanaofika kwenye eneo hilo.

Wageni wanaotembelea eneo la Meteriote hufika na kujionea namna ya ukubwa wa kimondo hicho kilivyokuwa na ukubwa wa ajabu, huku wakipenda kupiga picha juu ya kimondo hicho ambapo kila mtu anatozwa kuanzia dola 50, ambapo kwa fedha za kitanzania ni shilingi elfu 70.


Lakini kwa upande wa kimondo cha Mbozi si rahisi kuyaona hayo yaliyofanyika kule Namibia, zaidi ya kukutana na kinyumba kidogo kilichoezekwa kwa bati, huku kikiwa kimejengwa kwa kutumia tofali za udongo, na kupokelewa na mwangalizi wa eneo hilo!

Licha ya kuwapata wageni kadhaa wanaofika kwenye eneo hilo la Kimondo cha Mbozi na kuandikisha majina yao, huku wakitozwa shilingi 1,000 kama ni kiingilio cha kuona maajabu ya kimondo hicho, bado ipo haja ya serikali kutenga fedha zakuboresha mazingira yanayozunguka eneo hilo, sambamba na kutengeneza barabara yenye hadhi ya lami, ikiwa pia na kuweka alama za mabango zinazotangaza eneo hilo.

Tazama katika picha kadhaa zinazoonyesha mandhari ya eneo la Otavi nchini Namibia jinsi muonekano wa eneo ilipoanguka kimondo hicho, na kufanya kuwa moja ya vivutio vya wageni raia mbalimbali wanaotembelea nchi hiyo kujionea maajabu hayo. Idadi kubwa ya wanaotembelea eneo hilo wanapenda kufika katika sehemu hiyo na kupiga picha, huku wakiwa juu ya kimondo hicho.


Wageni wanaweza kutembelea kimondo hicho cha Mbozi. Kuna nyumba ndogo ya mapokezi iliyo na benchi kadhaa na meza. Mtunzaji ambaye huishi kwenye nyumba ya udongo iliyo umbali wa meta 50 hivi kutoka kwenye kimondo hicho, anatuomba tuandike majina yetu katika kitabu cha wageni. Tunagundua kwamba wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wametembelea sehemu hiyo.

Mradi wa chuma Liganga, Mchuchuma ni 
neema mpya Nyanda za Juu Kusini







Na Mwandishi Wetu, Ludewa

Mradi wa uchimbaji madini ya chuma uliopo Nyanda za Juu Kusini wa Liganga na Mchuchuma unaweza kuwa mradi mkubwa na wenye manufaa zaidi kwa Taifa na hivyo kuwa neema kubwa ndani ya mkoa wa Njombe pindi utakapo kamilika, imeelezwa.
Rais Jakaya Kikwete tayari ameahidi kuusimamia mradi huo kabla ya kipindi chake cha uongozi hakijamalizika.
Mradi wa uchimbaji madini ya chuma tayari umeshaanza kufuatia wawekezaji kutoka nchini China kupeleka mitambo ya uchimbaji.
Uchimbaji huo wa madini ya chuma, utakuwa ni neema na faraja kwa Taifa, sambamba na mkoa wa Njombe, ambapo madini yaliyopo kwenye mradi huo wa chuma upo wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Rais Kikwete amewahi kutembelea mradi huo na kuona maendeleo yake katika ziara aliyoifanya mwaka jana mwezi Oktoba alipokuwa akiuzindua rasmi mkoa mpya wa Njombe.
Ahadi ya rais kuahidi kuusimamia mradi huo kabla ya kumalizika kwa kipindi chake imetolewa mbele ya viongozi 100 wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Kata chini ya mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe wakati wa ziara ya mafunzo iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo Ikulu Juni 13,2014 wakati viongozi hao walipofika na kutoa shukrani zao kwa Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa kutokana na kuisimamia vyema Ilani ya CCM sanjari na kukubali kwake kuanza kazi ya uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya Chuma yaliyopo Liganga.
“Nimefurahishwa sana na ubunifu huu wa mbunge wenu, mafunzo haya yanatakiwa kutolewa na chama kwa ngazi zote na kama wabunge wote wangejitolea kukisaidia chama kama alivyofanya Filikunjombe tusingepata upinzani katika chaguzi’’ alisema kikwete
Rais aliitaja wilaya ya Ludewa imekuwa ni rasrimali kubwa sana ya Taifa kwa muda mrefu lakini ilikuwa haiendelezwi na kwamba kupitia serikali yake ameamua kuiendeleza kupitia wawekezaji na tayari miradi hiyo imeanza baada ya serikali kutiliana sahihi na wawekezaji kampuni ya Sichuan Hongda Ltd kutoka China na kampuni ya MM Steel ya Tanzania.
Faida ambazo serikali itazipata kupitia mradi huo wa makaa ya mawe ni pamoja na ajira za moja kwa moja 32,000 na ajira zisizo za moja kwa moja kwa wajasiriamali wanaozunguka migodi hiyo.
Serikali itapata Sh2.8 trilioni kila mwaka, fedha ambazo zinaelezwa zitaikwamua Serikali kwa kiasi fulani na bajeti tegemezi.

Fredrick Elton Mzungu anayekumbukwakwa kuvumbua Hifadhi ya Kitulo Makete


Na Mwandishi Wetu, Makete


FREDRICK Elton (picha ndogo) ni mtu ambaye atakuwa anakumbukwa sana hapa nchini Tanzania, kufuatia kufanya jambo ambalo ni la kihistoria hivi sasa, kufuatia kuibua hifadhi ya Taifa ya milima ya Kitulo ambayo inaunganisha mkoa wa Njombe na Mbeya kupitia wilaya ya Makete iliyoko mkoani Njombe.

Elton amekuwa ni miongoni mwa watu mashuhuri hivi sasa katika historia ya Tanzania, kufuatia kuweza kuvumbua hifadhi ya Kitulo mnamo mwaka 1870, lakini mwaka 1960 Tanzania kupitia Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) nalo liliamua kulichukua eneo hilo la Hifadhi ya Kitulo kuwa eneo maalum mahusus kwa ajili ya kilimo cha Ngano na Ufugaji wa Kondoo.

Hifadhi ya Taifa  ya milima  ya Kitulo imekuwa ikipata sifa kufuatia kuwepo kwa vivutio vya asili vya aina mbalimbali, yakiwemo maua ya uoto wa asili ambayo baadhi ya wakazi wa eneo jirani na hifadhi hiyo wamediriki kuiita hifadhi hiyo kama ‘Bustani ya Mungu’!

Ukweli hasa wa hifadhi hiyo ambayo  inapatikana  kijiografia  katika  Nyanda za Juu  Kusini,  Mkoani  Mbeya na Njombe  takribani  umbali wa kilomita  100  kutoka  jiji la  Mbeya.  Ni  hifadhi  ambayo  imetawaliwa  na uoto wa asili  wa  Maua yakupendeza na yakuvutia kwa kila mpitaji ndani ya hifadhi hiyo.

Iwapo utahitaji kutembelea ndani ya hifadhi, inakulazimu uwe umejiandaa vyema kwa kuandaa huduma za mahitaji muhimu, kama vile, usafiri binafsi au usafiri wa kukodi ni lazima fungu la fedha litengwe pembeni   ili kufanikisha safari ya matembezi ndani ya hifadhini ya Kitulo.

Baadaye ikageuzwa kuwa shamba la ng’ombe ambalo lipo hadi leo. Kutokana na umuhimu wa eneo hilo la hifadhi, wadau mbalimbali wa mazingira walipendekeza Kitulo itangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda umaridadi wa maua na mimea adimu yanayopatikana ndani ya hifadhi hiyo.

Mwaka 2005, Hifadhi ya Kitulo ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo, Msitu wa Livingstone na bonde la Numbi kiasi cha kilometa za mraba 412.9 ndani ya mwinuko wa mita 2100 na 3000.


Hifadhi hii inasifika kwa kuwa na maua aina mbalimbali na zaidi ya aina 30 hupatikana Kitulo.
Katika hifadhi hiyo ndege aina ya Tandawili machaka (Denhams Bustard) wamekuwa wakipendelea kuweka hifadhi yao kwa makazi. Wapo aina mbalimbali ya ndege kama vile Mpasua mbegu mweusi (Kipengere seed eater) na wengineo.

Mbali ya ndege hao pia wapo vipepeo, vinyonga, mijusi pamoja na vyura wenye sifa za kipekee ndani ya hifadhi hiyo.

Katika hifadhi hiyo hakuna wanyama wakali wakutisha zaidi ya kuwepo aina ya Tohe na Pofu ukilinganisha na hifadhi nyingine zilizopo Tanzania.

Vilevile, jamii mpya ya nyani (Lophocebus Kipunji) waligunduliwa mwaka 2003 ndani ya Kitulo. Hifadhi hii ina uwanda wa tambarare, mabonde, vilima na maporomoko ya maji. Ndani ya msitu, kuna miti aina ya cidar yenye urefu wa zaidi ya mita 50 na inakadiriwa kuwa mirefu kuliko yote duniani.

Hifadhi ya Kitulo inafikika kwa gari kutoka Chimala, kilometa 78 Mashariki mwa mji wa Mbeya. Reli ya TAZARA hupita karibu na hifadhi hiyo. Aidha kwa wasafiri wa barabara pia wageni wanaweza kutembelea hifadhi hiyo kwa kupitia Tunduma au Malawi ambapo utaweza kupitia mji wa Karonga.

Ni takribani  saa mbili kufika  katika makao  makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo kata ya Matamba, Makete ambapo inachukua mwendo  mfupi  tena  kufika hifadhini kwa barabara ya vumbi.

Ukubwa wa eneo la hifadhi ya milima ya Kitulo ni kilomita za mraba 412.  Na  uwepo wake  kijiografia katika Nyanda za Juu  Kusini  kunapelekea  hifadhi  hiyo hali yake  ya hewa kuwa ya baridi  na mwezi  wa Juni  na Agosti inakuwa  ni baridi  sana. Mvua ni nyingi na joto la kawaida ni la chini.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni