Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Fulgence Ngonyani akitazama gari dogo ambalo ni la mwalimu Benard Nyamahonga lililovunjwavunjwa vioo vyake na wanafunzi hao.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe, Fulgence Ngonyani akiangalia bweni la wanafunzi wa shule ya sekondari Njombe ambalo limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo.
Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Njombe wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Njombe (Njosi) wakati wakisubiri kupelekwa kituo cha polisi leo.
Askari akimwangalia mmoja wa wanafunzi ambaye anapelekwa kupakizwa kwenye gari kwa ajili ya kwenda kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Na Michael Katona, Njombe
SHULE ya sekondari Njombe (Njosi) leo imefungwa rasmi kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia vurugu kubwa zilizofanywa na wanafunzi wa shule hiyo za kuchoma moto bweni, karakana na kuharibu mali mbalimbali za shule hiyo.
Tamko la kuifunga shule hiyo limetangazwa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyasiro ambapo sasa itafunguliwa rasmi Novemba 8, mwaka huu huku wanafunzi hao wakitakiwa kuja shuleni hapo na kiasi cha shilingi 150 ndipo atakapo pokelewa.
Katika tukio hilo, askari polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya vurugu, wanaosoma Kidato cha Tano na Sita, ambao walifanya uharibifu wa kuchoma moto eneo la shule linalozunguka lenye miti na kuharibu pia gari dogo Toyota Carina namba: T809 BBX la Mwalimu wa Nidhamu, Benard Nyamahonga kwa kulivunjavunja vioo kwa mawe.
Kama hiyo haitoshi, wanafunzi hao walikwenda katika nyumba ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, Benard William na kurusha mawe yaliyovunja vioo vya madirisha ya nyumba hiyo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani pamoja na maofisa wa Upelelezi kutoka jeshi hilo alithibitisha kutokea tukio hilo na kufanya ukaguzi wa kutembelea maeneo yaliyoharibiwa, sambamba na kupata taarifa za awali kutoka kwa walimu wa shule hiyo.
Kamanda Ngonyani ambaye alikataa kuzungumzia kwa undani juu ya tukio hilo, ambapo alisema bado wanachukua maelezo, alisema taarifa rasmi ya juu ya upelelezi wa tukio hilo itatolewa.
Hata hivyo askari wa Jeshi la Polisi, walikuwa wamezunguka katika eneo lote la shule ya Sekondari Njombe kwa ajili ya kuweka ulinzi kuhakikisha hakuna wanafunzi yeyote anayetoroka kwa ajili ya hofu ya kukamatwa.
Askari hao ambao walikuwa wamevaa dhana zao za kudhibiti fujo wakiwemo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) pamoja na askari wa upelelezi, katika hatua ya awali ya kuwabaini wanafunzi waliofanya uharibifu huo, waliitisha paredi ya wanafunzi wote na kufanya uhakiki wa kubaini waliohusika na tukio hilo.
Katika zoezi hilo la utambuzi, zaidi ya wanafunzi zaidi ya 40 walitambulika awali kuwa vinara wa vurugu hizo, ambapo walipandishwa kwenye magari mawili ya polisi kupelekwa kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo lilivyotokea, Isabela Malangalila, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mpechi na Joshoni ambako ndiko shule hiyo ilipo, alisema vurugu za wanafunzi kuanza kuchoma moto mabweni hayo zilianza mnamo saa 5 usiku jana.
“Kabla ya tukio hilo, jana kulikuwa na kikao cha Wazazi na Walimu wa shule ya sekondari Mpechi ambacho kilikuwa kinawahoji wanafunzi 29 waliokuwa wamekwenda kwenye disko katika chuo cha Maendeleo ya Jamii bila ya kupata ruhusa,” alisema Malangalila.
Alisema katika kikao hicho, wanafunzi waliobainika kwenda kwenye disko hilo akiwemo pia mwanafunzi mmoja aliyekutwa na simu ya mkononi waliambiwa waandike maelezo, lakini jambo la kushanga baadaye jana usiku wanafunzi zaidi ya 1000 wanaosoma shule hiyo waliandamana na kuanzisha vurugu huku wakirusha mawe hovyo na kutishia kuchoma moto shule hiyo.
“Kufuatia vitisho hivyo niliwasiliana na kikosi cha zima moto kufika haraka kwenye eneo la shule, na hapo ndipo moto ulipoanza kuwaka kwenye bweni namba nane, baadhi ya wanafunzi walijitahidi kuzima moto uliokuwa ukiwaka katika bweni hilo,” alisema Malangalila.
Mtendaji huyo wa Mtaa alisema pia, wanafunzi hao waliendelea kufanya uharibifu zaidi kwa kuvunja duka la shule, kung’oa mboga zilizopandwa kwenye bustani, kisha kuwasha moto eneo la shule na kwenda kuharibu gari dogo la mwalimu wa nidhamu ambalo walilivunjavunja kwa mawe vioo vyake pamoja nakuvunja vioo vya nyumba ya mwalimu huyo.
“Hali hii inatisha na kusikitisha, wanafunzi hao walipofanya huo uharibifu walikwenda pia katika shule ya Msingi Kilimani na kuvunja madarasa pamoja na kuchanachana madaftari ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wako darasa la pili, huku wakiwa wameandika maandishi ukutani yakisema ‘Sisi wanafunzi wa Njosi tumekuja kulala tu’,” alisema Malangalila.
Naye Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Benard William akizungumzia tukio hilo, alisema bweni ambalo limeathirika sana kwenye tukio hilo ni lile la namba nane ambalo linauwezo wa kuchukua wanafunzi 102.
Aidha mwalimu William alisema kwamba chanzo cha wanafunzi hao kufanya vurugu hizo zinatokana na madai yao kwamba wamechoshwa kunyanyaswa ikiwemo kuonewa kwa wanafunzi wenzao 30 ambao walisimamishwa masomo.
“Huu ni utukutu usiositahili kuvumiliwa, unakatisha tamaa sana kwetu sisi walimu, madai yao ambayo wanayalalamikia kimsingi hayajitoshelezi, kwani walipotoroka kwenda kucheza disko katika chuo cha maendeleo ya jamii mmoja wao alivunjika mguu na hadi sasa anatembelea magongo,” alisema William.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Maria Mdee akizungumzia tukio hilo alisema haamini kilichofanywa na wanafunzi hao, na kuliita tukio hilo kuwa ni miongoni mwa matukio mabaya yaliyogusa sana maisha yake.
“Inasikitisha sana hasa ikizingatiwa kwamba wanafunzi ambao walikuwa wakiwahoji jana walikuwa bado hawajafukuzwa shule, bali wasimamishwa tu masomo mpaka hapo watakapo waleta wazazi wao, na Oktoba 7 tulikutana na wazazi na wanafunzi hao kwa ajili ya kuwaeleza makosa yao,” alisema Mdete.
Alisema kufuatia tukio hilo zima, athari itakuwa kubwa hivi sasa katika shule hiyo kwa baadhi ya wanafunzi ambao hawakuhusika na tukio hilo, kwani mwezi Novemba walikuwa wanatarajia kufanya mtihani wa mkoa kabla ya kufanya mtihani wa Taifa.
Mwenyekiti huyo alisema kufuatia tukio hilo, uongozi wa shule hiyo utasubili tamko la Afisa Elimu wa mkoa wa Njombe kama shule hiyo itafungwa ili wanafunzi warejee majumbani hadi hapo baadaye.
Wakati huohuo, Afisa Elimu wa mkoa wa Nkombe, Said Nyasiro akiwa na Ofisa Elimu wa shule za Sekondari mkoani hapa, Venance Msungu walifika katika eneo la shule hiyo na kutembelea kuangaria uharibifu uliotokea na kufanya mkutano wa ndani na walimu wa shule hiyo ambao ulichukua zaidi ya saa mbili, ambapo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia.
Wanafunzi wa shule ya sekondari wakiwa kwenye paredi ya utambuzi
Afisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Halmashauri ya Mji Njombe, Venance Msungu aliyevaa skafu akiwa na viongozi wa Wizara ya Elimu kutoka mkoani Njombe walipofika kwenye shule ya sekondari Njombe kuangalia uharibifu uliotokea.
Mmoja wa askari kanzu wa jeshi la polisi mkoani Njombe akisoma majina ya wanafunzi katika zoezi la utambuzi kwenye shule hiyo.
Vilevile, Kamanda wa Polisi, Ngonyani akiwa na maofisa wake, pamoja na walimu na viongozi hao wa wizara ya Elimu walifanya mkutano wa ndani, lakini alipotoka kwenye mkutano huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo atalizungumzia mara baada ya kufanya tathimini ili kubaini thamani ya mali zilizotekea.
Kutokea kwa tukio hilo la kuchoma moto bweni la shule hiyo, lina kuwa ni tukio la pili hivi sasa kutokea kwa shule hiyo ya sekondari Njombe, ambapo mwaka mmoja uliopita, wanafunzi wa shule hiyo walichoma moto bweni ambalo hivi sasa lipo kwenye ujenzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni