Jumanne, 7 Oktoba 2014

DC DUMBA AWAASA WAKULIMA WA MITI KUACHA IPEVUKE


Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa Semina ya Programu ya Panda Miti Kibiashara iliyofanyika leo mjini Njombe kwenye ukumbi wa Kyando. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa PFP, Maria Tham na anayefatia ni Mwakilishi wa Balozi wa Finland ambao ni wafadhili wa mradi huo kwa kushirikiana na serikali ya Tanzanua, Mikko Leppanen


Mkurugenzi wa PFP, Maria Tham akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba wakati akiwasili kwa ajili ya ufunguzi wa semina ya Panda Miti Kibiashara mkoani Njombe leo


Meneja wa PFP, Sangito Sumari akiwa na Mwakilishi wa Balozi wa Finland Mikko Leppanen walipokuwa wakizungumzia jinsi nchi ya Finland inavyosaidia harakati za kuhimiza upandaji miti kibiashara nchini Tanzania.


Na Mwandishi Wetu, Njombe

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba amewaasa wakulima wa miti mkoani Njombe kuacha kwanza miti wanayoipanda ipevuke na hatimaye ivunwe ikiwa tayari imekomaa kwa ajili ya kuwaingizia kipato.

Akizungumza katika ufunguzi wa Semina ya Wakulima wanaojihusisha na upandaji miti kibiashara iliyoandaliwa na Taasisi ya PFP inayotoa mafunzo ya Programu ya Panda Miti Kibiashara mkoani Njombe, Dumba alikemea tabia ya wakulima wa miti kuachana na kasumba ya kuvuna miti ikiwa bado haijakomaa vyema kwa ajili ya shughuli za ujenzi na biashara.

“Nimefarijika kuwa lengo kuu la Programu ya Panda Miti Kibiashara ni kuongeza kipato katika ngazi ya Kaya kutokana na kupanda miti kitaalam, nachukua fursa hii kuwaasa wananchi wa Nyanda za Juu Kusini kuipokea Programu hii kwa mikono miwili, na kutekeleza yale yatakayofundishwa na wataalam ili waweze kupata manufaa makubwa kuliko yale wanayoyapata sasa kutokana na upandaji miti,” a;isema Dumba.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Njombe, alisema ni vyema wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuchangamkia fursa ya upandaji miti kibiashara kwa kuwa inakadiriwa kuwa mahitaji ya mazao ya misitu kutoka kwenye mashamba ya miti yaliyopo nchini yanategemewa kuongezeka kutoka mita za ujazo milioni 1.5 na kufikia 3.7 ifikapo mwaka 2025.

“Hii sasa ni fursa nzuri kwa wakulima wa miti, maana wakati wa kuvuna mashamba yao kutakuwepo na soko la uhakika, ni lazima wakulima wa miti kupanda miti kibiashara kwa kutumia mbegu bora, kutunza mashamba ya miti kitaalam na kuzuia moto usiiharibu ili mazao yatakayopatikana yaweze kukidhi mahitaji ya soko la hapa nchini nan chi za nje,” alisema Dumba.

Aliwataka wakulima wa miti kuwahimiza wenzao ambao bado hawajajiunga na vikundi vya wakulima wa miti (TGA) ili wasiachwe nyuma katika utekelezaji wa program hiyo ambapo Dumba alisema itasaidia sana kupanda miti kitaalam na kupata mipango thabiti ya kujikimu.

Aidha mkuu huyo wa wilaya alisema semina hiyo inayotolewa itasaidia sana kutoa elimu kwa wakulima hao kuachana na kasumba ya kuvuna mapema miti yao, na hivyo kusaidia kutoa mbao safi zitakazo wapatia uhakika wakulima.


“Ni matumaini yangu Programu hii inayotolewa mkoani hapa itazingatia uzoefu wa TASAF unaotolewa katika shughuli zake, hivyo nina waahidi kuwa ofisi yangu itashirikiana na program kuhakikisha kuwa utekelezaji wa shughuli za kuwawezesha wasiojiweza unafanikiwa, na manufaa ya TASAF sote tunayafahamu,” alisema Dumba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni