Jumatatu, 10 Aprili 2017

MJANE GRACE: SINA HISIA ZA MAPENZI KWA MIAKA KUMI SASA, NAISHI NA VVU, WANAUME WANANITONGOZA


 Grace Kambindu alipokuwa akihojiwa na waandishi

Na Michael Katona, Njombe

Mwanamke Grace Kambindu “maarufu mama Rose” ni muathirika anayeishi na virusi vya ukimwi mkoani Njombe kwa miaka kumi hivi sasa toka alipogundulika kuwa na ugonjwa huo, lakini pamoja na kuwa na maambukizi ya VVU amesema bado wanaume wamekuwa wakimtongoza kwa nia ya kufanya naye mapenzi.

“Ni wanaume wengi sana wanaonihitaji nifanye nao mapenzi, lakini huwa nawaeleza hisia za mapenzi kwangu mimi zilishatoweka, nafanya kazi nzito hapa nilipo tofauti na uwezo wangu,” anasema Grace.


Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya, Grace anasema tangu ajitambue kuwa yeye ni muathirika wa VVU, wanaume wamekuwa hawakubaliani naye kwa namna anavyowaambia kuwa anaishi na maambukizi ya ukimwi, na badala yake wamekuwa wakimtongoza mara kwa mara, jambo ambalo ameonyesha kuwashangaa.

 “Hesabu zangu za kufanya mapenzi mimi na wanaume hazipo, isipokuwa wanadamu wengi niliowaona bado wanakuwa na mawazo ya kufanya ngono, nawashauri wafanye kazi kadiri ya muda wao unaoruhusu na si kufanya ngono kwa kutegemea kondomu itawasaidia,” anasema Grace.

“…Wahisani pamoja na Serikali nawaomba kwamba muathirika wa VVU apewe Lishe japo kikombe kimoja na siyo kumpatia kondomu wakati anapokwenda hospitali kuchukua dawa za kumuongezea siku za kuishi ulimwenguni, kufanya hivyo inaishiria muathirika wa VVU anakuwa anapangiwa akafanye ngono kwa kuwa amepewa kondomu,” anasema.

Mwanamke huyo amekwenda mbali zaidi pale alipozungumzia suala zima la kujilinda na ngono zembe kwa wakazi wa mkoani Njombe na kuwataka kuacha kujitumbukiza kwenye mchezo huo hasa ikizingatiwa Njombe ndiyo inayoongoza kwa maambukizi ya VVU kitaifa ikiwa na asilimia 14.8 kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), huku akiwataka kuchukua maamuzi yanayosisitiza kuacha kabisa kufanya ngono au kuwa na mpenzi mmoja.

“Utachukua kondomu ya bure na kwenda kufanya tendo la ngono, matokeon yake wote walioshiriki wanatoka wakiwa taabani, kwa nini basi mfadhili unayetoa kondomu usitoe tunda la ndizi, kuliko kumpa kondomu ambayo itamuongezea maumivu na uchovu, hakika hapo utamfanya ashukuru milele daima,” anasema Grace.

Katika hatua nyingine Grace amebainisha kuwa tangu agundulike kuwa na maambukizi ya VVU, bado wanaume wamekuwa hawaamini kama ni miongoni mwa wanaoishia na maambukizi na hivyo kumshawishi afanye tendo la ngono, jambo ambalo amelizungumzia kuwa limekuwa likimpa wakati mgumu.

“Ni wanaume wengi sana wanaonihitaji nifanye nao mapenzi, lakini huwa nawaeleza hisia za mapenzi kwangu mimi zilishatoweka, nafanya kazi nzito hapa nilipo tofauti na uwezo wangu, ni mjasiliamli mdogo sana hapa nilipo, nafuga ng’ombe Mkoani Njombe, lakini maji ya kuwapa ng’ombe ni haba, ninao ng’ombe wawili, kila mmoja anakunywa ndoo tatu, sina mtu wakunisaidia kubeba ndoo, hivyo nafanya kazi zote za kuteka maji kutoka visimani hivyo pamoja na maji ya matumizi yangu inaniradhimu niteke ndoo tisa kwa siku,” anasema Grace.

Mwanamke huyo anasema kutokana na kazi hizo za kuteka maji pamoja na kutafuta malisho ya ng’ombed wake, muda wa kukumbuka kufanya tendo la ngono kwa upande wake halipo maishani mwake hivi sasa, kwa sababu anarudi muda wote amechoka kutokana na nguvu kubwa anayoitumia kufanya kazi kwa ajili ya maisha yake ya kila siku.

“Kutokana na kazi ninayoifanya siku nzima, hunifanya usiku nikiwa nimelala kushituka na kupiga yowe mithili ya mtu niliyevamiwa, hii yote inatokana na uchovu ninaolala nao usiku hivyo muda wa kukumbuka masuala ya kuwa na wanaume kwangu mimi sina hilo,” anasema.

Anawashauri wanawake waliobainika kuwa na maambukizi Mkoani Njombe kuachana na kasumba ya kujikita kufanya ngono ikiwa ni sehemu ya kupunguza mawazo na badala yake wafanye kazi zitakazowasaidia kupunguza mambo mengi ikiwa ni pamoja na tendo hilo.

“Kwa wenzangu wenye maambukizi na hata ambao hawana maambukizi, nawashahuri wafanye kazi ili wasahau mambo ya ngono, hili litasaidia sana kupunguza maambukzi katika mkoa wa Njombe, kutokana na mwili wangu kukosa hisia najigundua muda wa kufanya tendo na mwanamme haupo ,” anasema.

“…Nimekuwa nikitafakari mwanamme atakayefanya tendo la ngono na mimi atanilipa shilingi ngapi ili ziweze kukidhi mahitaji yangu, kwa sababu mimi mwenye najigundua ninaweza kwa kuwa mume wangu aliniwezesha kuwa na vyanzo vya mapato kama mjasiliamali, umuhimu wa kuwa na mpenzi kwangu mimi haupo, hivyo na waambia wanawake wangu kuwa mwanamke yeyote akiwezeshwa anaweza tusiwe tegemezi, hivyo mimi nalia kila siku kuwa watu wasitegemee kondomu kama ndiyo kinga ya matumaini,” anasema Grace.

Akiuzungumzia Unyanyapaa unaofanywa dhidi ya wananchi waliobainika kuwa na maambukizi, Grace anasimulia kuwa kipindi alipofariki mume wake, jamii iliyokuwa inamzunguka alipokuwa naishi katika eneo la Kibena Mkoani Njombe ilikuwa ikimtenga kuwa ni miongoni mwa waathirika hivyo angeweza kuwaambikiza VVU.

“Kuna siku kulikuwa na msiba kwa jirani yetu hapa Njombe, nilinyanyuka kwenda mahali walipokuwa wanachambua mboga, wanawake wenzangu walitoa lile sufuria tulilokuwa tunachambua mboga na kusema mboga inatosha, lakini mbele waliendelea kuchambua,hapo ndipo nilipogundua wanawake hao walikuwa na Unyanyapaa dhidi yangu,” anasema Grace.

“…Watu walivumisha uvumi kuwa mume wangu aliyepata ajali hakufariki kwa hilo bali alikufa akiwa na yeye ana maambukizi, sita isahau ile siku kwani huwa machozi yananitoka nikiikumbuka, kibaya zaidi nilipokuwa nimeshika mwiko nasonga ugali, alikuja mama mmoja akanipora mwiko ule ili nisisonge ugali, na kunifukuza kwa kuniambia ondoka wewe huwezi kusonga ugali,” anasimulia Grace katika nyuso ya majonzi na masikitiko.

Anasema kutokana na kasumba ya jamii kuendeleza kuwa na dhana ya kunyanyapaa waathirika, kwa upande wake hadi sasa amekosa rafiki wa karibu wakuweza kumfikishia matatizo yake au hata kumtembelea na kumfariji kwa machungu aliyonayo.

“Wakati nafanyiwa vituko vya Unyanyapaa sikuwa na dalili zozote za kutokwa na utandu wa vidonda mdomoni au vipele, lakini bado jamii iliendelea kuwa na fikra kwangu mimi ni muathirika hivyo naweza kuwaambukiza pia, kadri miaka inavyosonga mbele na elimu inavyozidi kutolewa na mashirika ya kupambana na maambuziki kikiwemo Chama Cha Waandishi Wanawake Tanzania (TAMWA) na mtandao wa TGNP baadhi yao wananchi wamekuwa wakionesha kuamini kuwa hakuna sababu ya kuwanyanyapaa waathirika,” anasema Grace.

“Huwa nawauliza mbona huko nyuma mlikuwa mnanitenga, lakini najitahidi kuwasogelea na kuwaambia ngoja niwape elimu dhidi ya unyanyapaa kwa waathirika, hivyo wengi wamekuwa wakiniamini kwa yale ninayowaeleza kuhusu kuepuka maambukizi, na wananiita mimi ni mkufunzi, waliokuwa walevi na wanaofanya ngono pasipo njia salama wamekuwa wakiachana na tabia hiyo,” anasema.

Wakati Grace akizungumzia hali harisi anayokumbana nayo, naye Justine Mwinuka Mwenyekiti wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini anasema wao kama wananchi wanaoishi na virusi vya ukimwi ndiyo mashahidi namba moja juu ya janga hilo hapa nchini.

“Mkakati wetu wa msingi ni kufuata sera ya taifa ni kuhakikisha unafanikiwa wa unyanyapaa sifuri, maambukizi mapya sifuri na vifo kutokana na ukimwi sifuri,” anasema Mwinuka.

Anasema katika Baraza la Watu wanaoishi na VVU tayari upo mkakati uliowekwa kati ya watu wanaoishi na VVU hapa nchini kumtaka kila mmoja abadili mtazamo na ajipange.

“Ombi langu kwa serikali ni kutuingiza kwenye mifumo ya kisheria kupitia bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiwe ni chombo ambacho kauli yake isikike bayana na ikiingize kwenye sheria, hivyo mtazamo wetu tunafikiri ukiingizwa kwenye sheria, kwa sababu suala la ukimwi ni janga linaloua nguvu kazi, lakini janga hili lilikuja pabaya mahali ambako hapaepukiki, kwa sababu limekuja katika mahitaji yetu ya kimwili, watu wanaoa na kuzaa, mtu hawezi kukwepa,” anasema Mwinuka.

“…Katika utafiti wetu tumeshuhudia hata wale wanaokwepa kuoa wana maambukizi ya virusi vya ukimwi, tunatakiwa kujipanga kwa kina wanaoishi na VVU, wadau mbalimbali, Asasi, Taasisi pamoja na serikali, hili lote tutashinda, tukiwa na umoja, umoja ukikosekana kati ya wanaoishi na VVU na wadau  na serikali hili jambo litaendelea kuwa la kimyakimya,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa madhehebu ya Kikiristo wilayani Makete, Mchungaji Ayub Haule ametoa rai kwa serikali pamoja na wadau kuwa ili jamii iweze kukabiliana na maambukizi ya VVU.

“Kama janga hili ni letu sisi wenyewe, basi elimu ianzie nyumba kwa nyumba, kila familia kama mkuu wa kaya ahakikishe anaielimisha familia yake, makanisa yaendelee kutoa elimu juu ya jambo hili,” anasema.

Mratibu wa Tume ya kudhibiti Ukimwi mkoani Njombe (TACAIDS), Abubakar Majige anasema endapo watu watakubali kubadili tabia, basi mkoa wa Njombe na nchi kwa ujumla watakuwa wamefanikiwa kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi nchini.

“Hata ukiangalia vichocheo vyote vinavyosababisha maambukizi ya ukimwi vinahusu mila potofu, ulevi wa kupindukia na matumizi ya kondomu, serikali inajitahidi kuhimiza kutumia kondomu kwa kutaka wananchi wajikite zaidi kwenye matumizi ya kondomu, serikali inafanya jitahidi kondomu zitumike zaidi,” anasema Majige.

“…Kama taifa tumeanzisha mfuko wa ETF ambao utaratibiwa tueya kudhibiti ukimwi, lakini pia katika mkoa tumejiwekea mkakati wa kukabiliana na AFUA zote za ukimwi tunazifanya kutokana vipato vidogo vitakavyopatikana, lengo likiwa kuwashawishi wafadhili wazidi kujitolea katika kukabiliana na mambo ya ukimwi,” anasema Majige.

Dokta Godfrey Baragona mwakilishi wa mratibu wa Ukimwi mkoa wa Njombe anasema vituo vya kutoa tiba endelevu (CTC) mkoani Njombe vimefikia vituo 49 na kwamba ni zaidi ya wagonja 57,000 walioandikishwa lakini hadi sasa ambao wanaendelea kutumia huduma hiyo ni asilimia 54, huku asilimia nyingine zinaonyesha ni aidha ya wale waliohama vituo bila taarifa au wamefariki kwa sababu hakuna mtu anayetoa ushirikiano wa kutoa taarifa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni