Duru la Pili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linalotarajiwa kuanza leo Jumamosi Desemba 17 kwa michezo minne kabla ya michezo mingine minne kufanyika siku ya Jumapili Desemba 18, mwaka huu.
Katika mechi za leo, Mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans SC ya Dar es Salaam itakuwa mgeni wa JKT Ruvu ya Pwani kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Licha ya kwamba mwenyeji wa mchezo huo ni JKT Ruvu ambayo uwanja wake wa nyumbani mara nyingi huwa ni Mabatini ulioko Mlandizi, lakini kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi Kuu Bara, mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba, Young Africans na Azam FC, hufanyika Uwanja wa Uhuru.
Michezo mingine ya kesho ni Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting ya Pwani itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani ilihali Mwadui ya Shinyanga itaikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
Jumapili, Desemba 18, mwaka huu Mbao FC ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Ndanda itakuwa mwenyeji wa Vinara wa Msimamo katika Ligi Kuu ya Vodacom, Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
African Lyon ya Dar es Salaam itaikaribisha Azam FC pia ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Uhuru jijijini siku hiyo ya Jumapili wakati Majimaji ya Songea itakuwa Mbeya kucheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, limetoa masharti kadhaa likitaka klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kufuata.
Masharti hayo, ni kwa klabu kutumia makocha wenye sifa kwa mujibu wa kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom. Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) na kwa mujibu wa kanuni hiyo, makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi la Ligi kuu kwa msimu huu wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.
Pia kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza na Pili, masharti ni lazima makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo ambazo zimeanishwa kwenye kanuni za ligi husika.
Kadhalika, tunaagiza klabu kutotumia wachezaji wa kigeni au makocha kama hawana vibali vya ukaazi na kufanya kazi kutoka Idara ya Uhamiaji nchini iliyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni