Jumanne, 20 Desemba 2016

MHANDISI NGONYANI AITAKA TANROADS MOROGORO KUKARABATI BARABARA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (Kushoto), akifafanua jambo kwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mhe. Suzani Kiwanga (Wa tatu kulia), wakati alipokagua barabara ya Ifakara, Taweta hadi Madeke (KM 225) Mkoani Morogoro.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani ameutaka uongozi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanafanya matengenezo katika barabara zao ili ziweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka.

Mhandisi Ngonyani ameyasema hayo mara baada ya kukagua barabara ya Ifakara, Taweta hadi Madeke (KM 225) ambapo amesema barabara ya Ifakara –Kihansi (KM 130) imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unaendelea ili kipindi cha miaka mitano iweze kujengwa kwa lami.

“Katika miaka hii mitano tutahakikisha maandalizi ya awali ya kuwezesha barbara hii kujengwa kwa kiwango cha cha lami yanakamilika na hivyo kutuwezesha kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi rasmi”. amesema Mhandisi Ngonyani.

Amesema kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Ifakara na Kilombero kwa kuunganisha na Mkoa wa Njombe na hivyo kukamilika kwake zitafungua fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi hao.

Mhandisi Ngonyani amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kutekeleza ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi kwa kuunganisha mikoa mbalimbali kwa ujenzi wa barabara bora kwa viwango vya lami ili kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.

“Serikali ya awamu ya tano ipo madarakani kwa ajili ya wananchi bila kujali itikadi zao,tumewahaidi kuwaletea maendeleo hivyo tutajenga barabara zote tulizozihaidi kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya serikali yao”.amesisitiza Mhandisi Ngonyani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (aliyenyoosha kidole), akizungumza na wananchi wa Mlimba wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro wakati alipokagua barabara ya Ifakara, Taweta hadi Madeke (KM 225).

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake itaboresha huduma za mawasiliano katika shemu mbalimbali za nchi ili kuwawezesha wananchi kuwasiliana wakati wowote ili kukuza mahusiano yao kiuchumi, kibiashara na hivyo kukuza pato lao na la taifa.

“Tumeuomba uongozi wa kila wilaya utuletee maeneo ambayo huduma za mawasiliano hazijafika au zinasumbua ili sisi tuweze kuzishghulikia na kuzipatia huduma bora za mawasiliano”. Amesistiza Mhandisi Ngonyani.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mhe. Suzani Kiwanga ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuiweka barabara hiyo katika mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami kwa kuwa itafungua fursa mbalimbali kwa wananchi ambo wataweza kusafirisha mazo yao kwenda katika masokoni kwa urahisi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yupo Mkoani Morogoro katika ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Madaraja na Reli.
Wanakijiji wa kata ya Msagati wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro wakicheza ngoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani baada ya kuhakikishiwa barabara ya Ifakara –Kihansi (KM 130) itajengwa kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (Wa tatu kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mbunge wa Mlimba Mhe. Suzani Kiwanga (Wa pili kushoto) kabla ya mkutano na wanakijiji wa Msagati Mkoani Morogoro.
Wanakijiji wa kata ya Msagati wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (hayupo pichani) wakati wa mkutano na wanakijiji hao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni