Jumapili, 7 Juni 2015

Wabunge Wamtoa Jasho 

Simbachawene

Mpekuzi blog

WAZIRI wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amepata wakati mgumu bungeni, kutokana na wabunge wengi kutoridhishwa na utekelezaji wa mipango ya wizara yake.
 
Simbachawene alikumbwa na hali hiyo jana baada ya kuwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake ya Sh bilioni 536.960 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, huku wabunge wengi wakizungumza kwa hisia kutokana na kusuasua kwa miradi ya umeme.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, alisema kamati yake hairidhishwi na mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa na kuwataka wabunge kuibana Serikali iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.
 
Alisema wizara hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni kutopelekwa kwa wakati fedha za miradi ya umeme vijijini na kuiwezesha Tanesco licha ya fedha hizo kuidhinishwa na Bunge.
 
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Misanga (CCM), alishangazwa na hatua ya Serikali kusambaza umeme katika vijiji vya majimbo yote ya Mkoa wa Singida, isipokuwa jimbo lake pekee na kusema kuwa huo ni ubaguzi wa wazi.
 
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisimama na kujibu hoja hiyo akimtaka mbunge huyo kutokuwa na wasiwasi na kusema anatambua jimbo hilo litapatiwa umeme wa vijiji chini ya mradi wa MCC.
 
Lakini Misanga alikataa kukubaliana na majibu ya Serikali. “Majibu haya sijaridhika nayo, huu ni ubabaishaji mwingine, waziri anajua kabisa Singida tupo katika mpango wa REA, leo anasema tutapata umeme wa MCC, ni uongo,” alisema Misanga.
 
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, Davidi Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema inashangaza kuona miradi mingi inakwama kutekelezwa kwa kigezo cha ukosefu wa fedha, huku Serikali ikiendelea kulipa Sh bilioni tano kwa mmiliki wa Kampuni ya IPTL kila mwezi kinyume cha maazimio ya Bunge.
 
“Katika kashfa ya Escrow, tulipitisha maazimio humu ndani, kwamba Serikali isitishe malipo ya shilingi bilioni tano yanayotolewa kila mwezi kwa mmiliki wa IPTL.
 
“Haiwezekani wabunge tunalia miradi ya umeme imekwama huko vijijini halafu wakati huo huo singasinga mmoja anachukua bilioni tano azalishe umeme asizalishe, hizi fedha zingezuiwa zingeenda kutekeleza miradi hii iliyokwama.
 
“Mimi nashangaa wizara imeendelea kukaidi azimio la Bunge, kiti cha spika kinayumba. Katika moja ya maazimio tulikubaliana Serikali ilete majibu ya utekelezaji, hadi leo wamekaa kimya na spika anachenga,”alisema Kafulila.
 
Akijibu hoja hiyo, Simbachawene alisema katika maazimio ya Bunge hakuna kipengele kinachosema malipo hayo yazuiliwe na kusema Serikali haiwezi kufanya hivyo kwa kuwa hilo ni jambo la kisheria.
 
 “Mimi simjui singasinga anayesemwa hapa, ila ninachojua mimi ni kwamba kuna mkataba baina ya Tanesco na IPTL, sasa unajiuliza tunaufutaje huu mkataba, ni vigumu, unaufutaje?
 
“Sheria ya kampuni, ‘a company is a person, IPTL is a person’, huyo mwingine anayetajwa naye ‘is a person’. Huyu ‘person’ anayeitwa IPTL hawezi akaathiriwa hivi hivi tu, tutashitakiwa kama taifa, tutalipa gharama kubwa kuliko hizo unazosema.
 
 “Na mifano mnaifahamu, tumepoteza fedha nyingi kwa kulipa kutokana na maamuzi mabaya, sasa mimi naomba Bunge lituambie tutekelezeje? Bunge lituambie sasa nyinyi kutokana na jambo hili liko hivi fanyeni hivi, ili likitokea jambo huko tusijekuulizwa.
 
 “Mimi nilikuwa mjumbe wa kamati na Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki), hilo azimio analosema Kafulila kila siku la kusimamisha haya malipo ya ‘capacity charge’ halipo katika maazimio nane, labda kiti kitusaidie, kama hilo azimio lipo huko kwenu tupeni,” alisema Simbachawene.
 
Hata hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azan Zungu kabla ya kumruhusu Kafulila kufunga hoja yake, alisema hawezi kuruhusu mjadala huo uendelee kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani.
 
“Hili suala lipo mahakamani, najua ‘concern’ (dhamira) ya Kafulila ni ‘very banning’ (nyeti), lakini kuna masuala ya kisheria na mimi kama refa nafuata taratibu za kibunge.
 
“Naelewa sana hoja yako Kafulila, nimeiacha ili upate ‘comfort’, lakini kiti hakiwezi kuruhusu mjadala huu uibuke upya wakati mambo haya tulishafanyia uamuzi, na kwa mujibu wa kanuni zetu jambo likishafanyiwa uamuzi haliwezi kurudiwa,” alisema Zungu.
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni