Jumapili, 7 Juni 2015

Msafara wa Makongoro 

Nyerere Wapata Ajali

Mpekuzi blog

MSAFARA wa Makongoro Nyerere, mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, umepata ajali wakati mwanasiasa huyo akiwa katika harakati za kutimiza masharti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kutafuta wadhamini ili aweze kuwania nafasi ya urais.
 
Ajali hiyo iliyojeruhi watu watano waliokuwa kwenye msafara huo, ilitokea jana katika eneo la Tekniko, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma baada ya gari aina ya Land Cruiser lenye namba T 188 BXG walilokuwamo kupinduka.
 
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ferdinand Mtui, alisema ilitokea saa 10:30 asubuhi wakati msafara huo ukiongozwa na Makongoro ukielekea Kigoma mjini.
 
Kamishna Mtui aliwataja waliojeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo kichwani na mabegani  kuwa ni dereva wa gari hilo Julius Kambarage, ambaye ni mtoto wa Makongoro na mwandishi  Evans Magege.
 
Wengine ni Katibu Mwenezi wa CCM, Musoma Mjini, Fikiri Marumba na Ally Tesha ambao wote walipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu na kuendelea na msafara.
 
Majeruhi mwingine ni Cyprian Msiba ambaye ni mwandishi wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten ambaye alibaki hospitalini hapo kwa ajili ya huduma ya X-Ray kutokana na kuumia sehemu za bega.
 
Makongoro ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki, anazunguka mikoa mbalimbali nchini kwa nia ya kutafuta wadhamini ili kuomba ridhaa ya CCM kumpitisha kugombea nafasi ya urais.
Mpekuzi blog

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni