Jumatano, 27 Mei 2015

Wasomi wachambua kauli ya Lowassa

Wasomi wachambua kauli ya Lowassa

SHARE THIS
TAGS
LOWASSAAAGRACE SHITUNDU NA MICHAEL SARUNGI,
DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuweka wazi majaliwa yake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu yale anayoaamini na kuyasimamia katika taifa, wasomi na wadau wa siasa nchini wamechambua kauli ya kiongozi huyo.
Lowassa juzi alizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Dodoma na kutangaza msimamo wake wa siasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na vipaumbele vyake, elimu, kupambana na umaskini.
Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema vipaumbele alivyovitoa Waziri Mkuu wa huyo wa zamani vitafanikiwa endapo kiongozi huyo ataishi kwa kutekeleza kwa vitendo kauli zake.
Profesa Ngowi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi, alisema masuala yote yaliyotamkwa na Lowassa ni mazuri endapo yatapata utekelezaji na usimamizi unaotakiwa na yanahitaji ushirikishwaji wa wananchi bila kutanguliza masilahi ya siasa.
Alisema kwa miaka mingi sasa nchini Tanzania, wanasiasa wamekuwa na kauli mbalimbali nzuri kila nchi inapokaribia katika Uchaguzi Mkuu huku uetekelezaji wake ukikosa tija.
Alisema tatizo kubwa inalolikabili taifa sasa ni umasikini unaoendelea kuwahangaisha watanzania wengi hasa maeneo ya vijijini ambako wengi wao wanaishi kwa kupata mlo mmoja kwa siku.
“Kiongozi yeyote atakayebahatika kuchaguliwa kuliongoza taifa hili ni lazima ajue kuwa taifa letu linapita katika kipindi kigumu cha mgawanyiko ndani ya jamii hasa udini, ukabila na pengo kati ya walionachao na wasionacho,” alisema Profesa Ngowi.
Dk Bana
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema urais ni taasisi hivyo ni jambo ambalo mtu binafsi anaweza kwa kuzingatia ilani ya chama chake .
Alisema mambo yaliyazungumza ya kuhusu elimu, ajira kwa vijana hali ya uchumi na umaskini wa watanzania si mageni katika jamii ya Tanzania na yamekuwa yakizungunzwa mara kwa mara bila kutafutiwa ufumbuzi.
“Kutokana na hali hiyo, kiongozi yeyote atakayechaguliwa katika nafasi ya juu anapaswa kuyatafutia ufumbuzi na kutoa mfano wa suala la ajira ya vijana kuwa lisipofanyiwa kazi mapema kama alivyosema Lowassa, linaweza kulipuka wakati wowote.
“Tunahitaji kuwa na mjadala wa taifa na kuja na makubaliano ya pamoja na kuamua nini kitakuja kuwa kipaumbele chetu cha kwanza kwa awamu ijayo kuliko kuviachia vyama kuamua vyenyewe,” alisema Dk. Bana.
Bashiru Ally
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema hakubaliani na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa na itikadi ya kuweka vyama vyao mbele badala ya masilahi ya taifa kwanza.
“Masuala yaliyoyaongelewa na Lowassa yatakuwa na msingi endapo yatapata utekelezaji wa kweli kuliko kuishia kwenye majukwaa ya siasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kutafuta kura kwa wananchi,” alisema Ally.
Mgaya
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Nicholaus Mgaya, alisema suala la urais kila mmoja ana mtazamo wake wa kutimiziwa mambo yanayomuhusu.
Alisema TUCTA kama shirikisho halishabikii Chama au mgombea yeyote bali kinahitaji Rais atakayeweza kuwatatulia matatizo ya maslahi ya wafanyakazi.
Askofu Niwemugizi
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge mkoani Kagera, Seveline Niwemugizi, alisema Tanzania ilipofikia inahitaji kiongozi jasiri atakayekuja na mfumo thabiti ukaoweza kuwatoa Watanzania katika lindi la umaskini.
Alisema wakati wa kushabikia ahadi hewa umepitwa na wakati hivyo watanzania wa sasa wanataka kiongozi jasiri atakayekuwa na uwezo wa mbinu na mikakati mbadala.
“Huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kufanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwa manufaa ya mtanzania wa leo na kizazi kijacho” alisema Askofu Niwemugizi.
Wakati huo huo, Utafiti uliofanywa na Kituo cha Samunge (Samunge Social Research Center), uimempaisha tena Lowassa kwa kuongoza kwa asilimia 20.7 akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa kwa asilimia 11.7.
Mbali na hayo utafiti kwa vyama vya siasa unaonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kinaongoza kwa asilimia 53.5 na kufuatiwa na Chadema kwa asilimia 34.4.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mtafiti Mkuu wa Kituo hicho, George Nyaronga alisema utafiti huo ulianza Desemba 2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni