Jumatano, 27 Mei 2015

UTEUZI WA WACHEZAJI: Kocha Nooij akumbuka shuka kumekucha...

UTEUZI WA WACHEZAJI: Kocha Nooij akumbuka shuka kumekucha...


Kocha wa tifa Stars, Mart Ignatius Nooij 
Dar es Salaam. Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kuweka bayana kuwa kibarua cha kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij kitasitishwa iwapo timu hiyo itashindwa kufuzu mashindano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN), Mdachi huyo ameamua kuwaita wachezaji waliopendekezwa na baadhi ya wadau wa soka nchini.
Uamuzi wa kocha huyo ni kama amekumbuka shuka asubuhi baada ya kuwaita kikosini wachezaji vijana ambao alitakiwa kuwaita tangu alipopewa kibarua cha kuinoa Stars.
Kamati ya utendaji ya TFF, iliyokutana mwishoni mwa wiki ilikuja na azimio kwa kocha Nooij kama atashindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu Chan 2016, kibarua chake kitafikia mwisho.
Pia, kamati ya ufundi wa TFF ilipewa jukumu la kuangalia kocha mwingine endapo Mdachi huyo atashindwa kufikia malengo ya kufuzu Chan 2016.
Kutokana na presha hiyo, Kocha Nooij jana alitangaza kikosi cha wachezaji 16, huku akiwaita kwa mara ya kwanza wachezaji Mohamed Hussein ‘Tshabalala’,  Jonas Mkude (Simba), Mudathir Yahya, (Azam), Rashid Mandawa, (Kagera Sugar) na Malimi Busungu (Mgambo JKT).
Kuitwaa kwa wachezaj hao kunatokana na shinikizo la wadau waliohoji uteuzi wa kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Cosafa na kutolewa raundi ya kwanza baada ya kufungwa mechi tatu.
Mjadala mkubwa ulikuwa ni kuachwa kwa kiungo wa Simba, Mkude wanahabari wengi walihoji kwa nini mchezaji huyo ameachwa, lakini kocha Nooij alijibu Tanzania ina wachezaji zaidi ya 300, Mkude ni nani. Mbali ya kiungo huyo, pia kuachwa kwa mshambuliaji Mandawa wa Kagera Sugar na Busungu wa Mgambo JKT kulizua mjadala kutokana na uwezo waliouonyesha katika Ligi Kuu msimu uliomalizika kulinganisha na John Bocco ambaye ndiye kwanza amerejea kutoka bechi alipokuwa majeruhi.
Hata hivyo, ni kama Nooij ameutua mzigo na lawama alizobebeshwa baada ya kuwachagulia Watanzania wachezaji wanaowataka watakaoungana na aliowaita yeye mara ya kwanza kwa ajili maandalizi ya kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Africa (Afcon) na zile za kufuzu kwa wachezaji wa ndani(CHAN).
Wachezaji hao wataingia kambini leo kwa ajili ya kupimwa afya zao na  kujua maandeleo yao kabla ya kuwajumisha katika kikosi cha pamoja kitakachokua kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri. Nooij amewajumuisha kikosini wachezaji Mohamed Hussein, Peter Manyika, Jonas Mkude (wote Simba), Juma Abdul (Yanga), Mudathir Yahya, Kelvin Friday (wote Azam), Rashid Mandawa, Atupele Green (Kagera Sugar), Malimi Busungu (Mgambo JKT) na Emmanuel Simwanda (African Lyon).Wengine ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela (Yanga), Frank Domayo, Aishi Manula (Azam), Haroun Chanongo (Stand United), Hassan Isihaka (Simba), ambao walikuwapo katika kikosi cha awali cha Nooij, lakini hawakusafiri  kwenda Afrika Kusini kutokana na kuwa majeruhi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Baraka Kizuguto alisema timu hiyo itaanza kambi rasmi Juni Mosi kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri ugenini, huku wachezaji wanaocheza soka la kulipwa TP Mazembe, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wakitarajiwa kujumuika na wenzao siku hiyo.
Alisema kabla ya kwenda Misri, Stars itaweka kambi Addis Ababa Ethiopia kwa wiki moja kuanzia Juni 4, kabla ya kuelekea kwenye mchezo huo. 
Kizuguto alisema Juni 20, Taifa Stars itakuwa wenyeji wa Uganda kwenye Uwanja wa Aman Zanzibar katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Chan 2016, nchini Rwanda 2016 na mchezo wa marudiano kufanyika baada ya wiki mbili nchini Uganda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni