Dar es Salaam. Yanga imeshinda
vita ya nje ya Uwanja baada ya kuipata saini ya kiungo Deus Kaseke
aliyekuwa akiwaniwa na watani wao, Simba kwa muda mrefu.
Usajili huo wa Kaseke umekamilika jana saa 6:35
mchana katika zoezi lililochukua takribani saa tatu za mazungumzo ya
mwisho baada ya klabu zote mbili kukimbizana usiku kucha juzi
wakimuwinda mchezaji huyo aliyemaliza mkataba na klabu yake ya Mbeya
City.
Kaseke alifanikiwa kusaini mkataba wa miaka miwili
kuichezea Yanga, hata hivyo kabla ya kusaini na mabingwa hao wa Tanzana
Bara ililazimika kumuongezea malipo kufuatia Simba kuwa katika harakati
za kutaka kumbadilisha mawazo.
Kaseke alitua jijini Dar es Salaam Ijumaa Mei 22,
akiletwa na Yanga waliomkatia tiketi hiyo, lakini Simba ilijipanga na
kutaka kumtorosha katika hoteli moja iliyopo eneo la Kariakoo kabla ya
mabingwa hao kushtukia zoezi hilo na kumhamisha katika hoteli nyingine
iliyopo Sinza Kumekucha jijini Dar es Salaam.
Yanga imelazimika kutumia Sh 35 milioni badala ya
ile ya awali Sh 30 milioni kufuatia Simba kutoa ofa ya mwisho wakitaka
kumpatia Sh 45milioni pamoja na mshahara wa Sh2milioni na gari.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha alisema klabu yake imefanikiwa kushinda vita muhimu kwa kumsajili Kaseke.
“Usajili wetu umetokana na mahitaji ya kocha wetu
(Hans Pluijm), ambaye amekuwa akisisitiza anahitaji huduma ya Kaseke
katika kikosi chake, kazi yetu kama uongozi ni kuhakikisha tunayafanyia
kazi matakwa ya kocha na sasa tumempata Kaseke tutakuwa naye hapa kwa
miaka miwili,” alisema Tiboroha.
Kaseke alisema Yanga haitajuta kumsajili na kuomba ushirikiano wa Wanayanga kwa kipindi chote atakachokuwa kwenye timu hiyo.
“Sitarajii kujutia kujiunga Yanga wala klabu
kujutia kunisajili, nitajituma na kuhakikisha nakuwa miongoni mwa
wachezaji watakaoipa mafanikio Yanga,” alisema Kaseke.
Mshambuliaji wa FC Platinum ya Zimbabwe, Donald
Ngoma anawasili jijini leo jioni baada ya majadiliano, atasaini mkataba
huo tayari kujiunga na Yanga.
Dk Tiboroha alisema kimsingi wameshakubaliana na
FC Platinum kuhusiana na usajili wa mchezaji huyo mwenye kila aina ya
ufundi katika kufunga mabao.
“Ujio wake ni kukamilisha yale tuliyokubaliana na
uongozi wa klabu na yeye binafsi, nini kitafanyika, tusubiri matokeo ya
majadiliano hayo ya mwisho,” alisema Dk Tiboroha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni