Mbowe aliyasema hayo jana katika mkutano wa chama
wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe
jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine alizindua kitabu cha
mambo aliyoyafanya mbunge wa jimbo hilo, Halima Mdee na wimbo maalumu
wa msanii wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha.
Akizungumza katika mkutano huo uliorushwa moja kwa
moja na ITV, Mbowe alisema katika maeneo yote ya nchi, watu wamekata
tamaa ya maisha kutokana na uongozi mbaya wa chama tawala, hivyo wako
tayari kufanya mabadiliko ya mfumo wa utawala.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu matamanio ya
Mwalimu Nyerere yanaenda kutimia. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo
wameyakosa ndani ya CCM. Nimezunguka nchi nzima na kubaini kuwa wananchi
wanazo sababu na uwezo wa kuyaleta mabadiliko kutokana na kiu
waliyonayo,” alisema.
Mbowe aliyeanza mkutano huo kwa kukagua gwaride la
kikundi cha Red Brigade, alitoa kauli hiyo akimnukuu Mwalimu Nyerere
aliyepata kusema kuwa, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata
ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia mchakato wa
uandikishaji wapigakura kuwa unahitaji kutazamwa kwa namna nyingine ili
kuwatendea haki wananchi ambao wana shauku ya kutimiza haki hiyon ya
kikatiba.
“Juzi nilikuwa Mbeya, nimeshuhudia wananchi
wakilala katika vituo vya kuandikishia kutokana na hofu waliyonayo
kukosa uchaguzi mkuu. Namkumbusha Jaji Lubuva (Damian, mwenyekiti wa
Tume ya uchaguzi) aongeze muda na isiwe siku saba kama ilivyopangwa
awali. Kutofanya hivyo atakuwa anajitafutia lawama ambazo hakutakuwa na
kiongozi yeyote wa CCM atakayesimama kumtetea pindi wananchi
watakapokuwa wanamlaumu hapo baadaye,” alisema.
Mwenyekiti huyo mwenza wa umoja wa Katiba ya
wananchi (Ukawa), pia alibainisha mkakati wa umoja huo kugomea na
kuipinga rasimu inayotaka vyombo vyote vya habari kujiunga na Shirika la
Habari Tanzania (TBC) kwa taarifa ya habari ya saa 2.00 usiku.
“Tutaleta vurugu. Tutasimamisha Bunge kupinga
sheria hiyo kwa sababu hiyo ni hujuma ambayo wananchi hawaikubali na
mimi kama kiongozi wa upinzani nitalisimamia hilo,” alieleza.
Akimakaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge
wa Ubungo, John Mnyika alisema mkutano huo ni muhimu na chama
kimeuandaaa ili kuthamini umuhimu wa wanawake katika jamii.
“Mwenyekiti fikiria kama wewe unabeba mimba miezi
tisa, ujifungue na kumlea mtoto. Hayo ndiyo wanayoyafanya wanawake hawa.
Ni lazima tukubali ujasiri wao kwa kuyajali majukumu yao,” alisema
Mnyika.
Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Mabere
Marando alisema Chadema kimejipanga kuwaleta viongozi wake wote jijini
hapa kufanya kampeni ya uandikishaji katika daftari la kudumu ili
wapigakura wafike milioni 3.5 na kuiondoa CCM madarakani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni