Jumatatu, 25 Mei 2015

TAFRANI BURUNDI: Hofu yatanda kuuawa kiongozi wa upinzani

Aliyekuwa kiongozi wa chama cha upinzani cha UDP, marehemu Zedi Feruzi akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kuelezea mikakati ya chama chake juu ya uchaguzi mkuu. Picha na mtandao. 


Bujumbura, Burundi: Huku Serikali ikikanusha kuhusika katika mauaji ya kiongozi wa upinzani wa Burundi, baadhi ya makundi ya kisiasa yameanza kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na hatima ya kisiasa ya nchi hiyo, wiki moja baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusogeza mbele tarehe uchaguzi wa wabunge.
Aliyeuawa ni Zedi Feruzi, aliyekuwa mkuu wa Chama cha Umoja wa Amani na Demokrasia (UPD). Aliuawa mwishoni mwa wiki  kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiwa nyumbani kwake.
Mauaji ya kiongozi huyo aliyeuawa pamoja na mlinzi wake, yamechochea hisia za mgawanyiko miongoni mwa wanasiasa ambao wanaendesha shinikizo kumtaka Rais Nkurunziza kutowania muhula mwingine wa tatu wa uongozi.
Mwili wa Feruzi ulipatikana nje ya nyumba yake huku watu walioshuhudia wakisema walisikia milio 20 ya risasi kabla ya wahusika wa shambulizi hilo kutoweka kwa gari maalumu waliokuwa wakitumia.
Kiongozi mwandamizi wa upinzani, Agathon Rwasa alisema kuwa hakuna taarifa rasmi kuhusu ni nani aliyetekeleza mauaji hayo ingawa alisema kuwa mwanasiasa huyo alikuwa mstari wa mbele kupinga mkakati wa  Rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Baada ya Feruzi kuuawa, vijana wa eneo hilo waliandamana na kufunga barabara za mtaa huo kama sehemu ya kuonyesha kutoridhishwa kwao na tukio hilo. 

Kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayohatarisha usalama na mshikamano wa taifa ikiwamo maandamano yanayoendelea kushuhudiwa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuongeza muda wa kutaka kutawala.
Zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano mwishoni mwa mwezi uliopita.
Shambulio la mwanasiasa huyo limetokea siku moja baada ya shambulizi la bomu katika soko moja mjini Bujumbura lililosababisha mauaji ya watu watatu na wengine takriban 40 kujeruhiwa.
“Tulisikia milio takriban 20 ya risasi, kila mtu akalala chini, watu waliona gari aina ya Toyota likiondoka kwa kasi,” alisema mkazi wa Ngagara ambaye hata hivyo, hakushuhudia mauaji ya Feruzi.
Katika shambulio hilo, ofisa aliyekuwa miongoni mwa waliopewa jukumu la kumlinda kiongozi huyo wa upinzani, alipata majeraha mabaya.
“Tulikuwa tunarejea kwa miguu wakati gari aina ya Toyota liliposimama karibu na sisi na wanaume waliokuwa ndani kuanza kutufyatulia risasi,” alisema ofisa mwingine ambaye hakutaja jina lake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni