Ijumaa, 22 Mei 2015

TAARIFA KUHUSU KAMPENI YA UGAWAJI WA DAWA ZA KUKINGA NA KUTIBU MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU KAMPENI YA UGAWAJI WA DAWA ZA KUKINGA NA KUTIBU MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE   KATIKA MKOA WA MWANZA

Ndugu Wananchi,
Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, hususan Kichocho na Minyoo ya tumbo yameathiri sehemu kubwa ya jamii katika mkoa wetu wa Mwanza. Magonjwa haya huleta mahangaiko makubwa kwa wananchi  hasa kwa watoto ikiwemo upungufu wa damu, kuzorotesha ukuaji, kupunguza mahudhurio ya watoto shuleni na pia kutofanya vizuri katika masomo yao. 

Ugonjwa wa Kichocho husababisha Saratani ya Kibofu cha mkojo ambayo haina tiba hadi sasa. Minyoo ya tumbo inaweza kusababisha Utumbo kuziba na mtu kulazimika kukatwa utumbo, Minyoo ikiingia kwenye ubongo huleta dalili  kama za kifafa vilevile minyoo huathiri Ini na  endapo muathirika hatawahi kupata  matibabu, dalili zote hizi husababisha Mauti. 

Magonjwa haya ni moja kati ya vyanzo vikuu vya umasikini katika familia, jamii, na taifa kwa ujumla. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa wagonjwa walioathirika kwa saratani ya kibofu cha mkojo na hasa wakazi wa kanda ya ziwa kwa asilimia kubwa chanzo chake ni maambukizi ya kichocho.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia tamko la Shirika la Afya Duniani linalokusudia kudhibiti au kutokomeza magonjwa haya ifikapo mwaka 2020, na ili kutekeleza azma hiyo. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetengeneza mpango kazi wa miaka mitano wa Utekelezaji wa shughuli mbalimbali za udhibiti wa magonjwa haya.
Ndugu Wananchi,

Tafiti zilizofanyika mwaka 2005 zimeonyesha uwepo wa maambukizi ya ugonjwa wa  Kichocho mkoani Mwanza yapo juu kuliko maeneo mengine nchini. Utafiti huo ulionyesha maambukizi ya Kichocho yapo kati ya asilimia 12.7 hadi 87.6 nchini. Utafiti huo unaonesha kwamba ugonjwa wa kichocho umeenea zaidi maeneo ya kando kando ya ziwa Viktoria na kiwango cha maambukizo ni zaidi ya 80% na kwa minyoo ya tumbo ni hadi 100%.

Na katika jamii za watoto wenye umri wa kwenda shule, tafiti kwa njia ya parasitologia, maambukizi ya ugonjwa huu ni zaidi ya 50%. Kwa kiwango hicho cha maambuzi, kwa mujibu wa tafiti na maelekezo ya kitaalam ya Shirika la Afya Duniani (WHO), jamii inapaswa ipewe dawa za kukinga na kutibu.

Tangu mwaka 2009 wizara ilizindua mpango wa udhibiti wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika mikoa ya mitano kwa kuanzia, na hadi mwaka 2012 mpango huu tayari ulikuwa umetekelezwa katika mikoa 14 na hadi mwishoni mwa mwaka jana (2014) umekuwa ukitekelezwa  katika mikoa 17 ikiwemo Mwanza iliyoingia katika mpango mwaka 2013. 

Hadi sasa, mpango huo unaratibu shughuli zake katika mikoa 21 ikiwemo Kilimanjaro, Arusha, Simiyu na Geita iliyoingizwa katika mpango mwaka huu wa 2015. Lengo la mpango kwa sasa ni kuifikia mikoa ya Shinyanga, Mara na Kagera mapema iwezekanavyo ili kudhibiti magonjwa haya ifikapo mwaka 2020.


Ndugu Wananchi,

Mkoa  unawajulisha wananchi na wakazi  wote wa mkoa wa Mwanza  kuwa tarehe 26   na 27 Mei 2015 tutaendesha kampeni ya  ugawaji  dawa za kukinga na kutibu magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya Tumbo. Walengwa wa kumeza dawa hizi ni watoto  wote wenye umri wa kuanza shule ya msingi walioandikishwa na wasioandikishwa.

Kampeni hii itaendeshwa na watalaam wa huduma za afya wakishirikiana na Walimu katika shule zote za msingi waliopatiwa mafunzo maalumu ya ugawaji wa dawa hizi. Kabla ya unywaji wa Dawa hizi Mtoto anatakiwa ale chakula na katika muda usiozidi  masaa 2 baada ya kula awe amepatiwa dawa hizi; chakula hicho kitaandaliwa shuleni.

Hivyo kila Mzazi  katika mkoa wa Mwanza  anaombwa  amruhusu mtoto wake aende kumeza dawa hizi muhimu ili ajikinge na kupata tiba ya magonjwa haya hatari kwani huduma hii  ya dawa za kinga tiba inatolewa bila malipo kwa kila mtoto.

Dawa hizi zimethibitishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa ni salama, na hazina madhara yoyote kwa afya ya binadamu zinapomezwa kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wahudumu wa afya na Walimu waliopatiwa mafunzo.

Dawa zitakazohusika ni za Praziquantel za kudhibiti Kichocho na Albendazole za kudhibiti  Minyoo ya tumbo ambazo zitatolewa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule, walioandikishwa na ambao hawakuandikishwa.

Ndugu Wananchi,
Ni matumaini yetu  kuwa Wazazi mtawaruhusu watoto wajitokeze kwa wingi ili kumeza dawa hizi kwa maendeleo ya afya za watoto wetu na Jamii kwa ujumla. Nawaombeni sana, muendeleze sifa nzuri ya Mkoa wetu kwani umekuwa ukifanya vizuri miaka yote katika suala zima la chanjo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

IMETOLEWA NA OFISI YA MKUU WA MKOA MWANZA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni