Jumamosi, 9 Mei 2015

MFAHAMU WAZIRI WA UJENZI: JOHN POMBE MAGUFULI



KWA UFUPI
Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978. 
Historia yake

Na Julius Mtatiro
John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 huko wilayani Chato Mkoani Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya mkoa mpya wa Geita) na atatimiza miaka 56 Oktoba mwaka huu.
Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Halafu alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 1981 – 1982.
Alipopata stashahada yake, moja kwa moja alikwenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983.
Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke, watoto na familia imara.
Mbio za ubunge
Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni