Ijumaa, 1 Mei 2015

CCM YATOA TAHADHARI YA KUIBUKA KWA UGAIDI NCHINI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU.

Katibu wa siasa Itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusiana na kukamatwa kwa kiongozi wa Chadema.

 
CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya kimeitaka Serikali na mamlaka zinazohusika kukichunguza Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) katika harakati zake za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao.
 
Wito huo ulitolewa na Katibu wa siasa itikati na uenezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ofisi za Chama hicho Mkoa wa Mbeya.
 
Madodi alilazimika kutoa rai hiyo kufuatia Jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya kumkamata mmoja wa viongozi wa ulinzi wa Chama cha Chadema wilaya ya Momba akiwa na silaha mbali mbali ikiwemo sare za Jeshi la Wananchi.
 
Alisema Kiongozi huyo aliyemtaja kwa jina la Mathew Mwafongo alikamatwa juzi akiwa anaelekea Chitete kwa ajili ya kutoa mafunzo ya Red Briged kwa vijana wanaokadiriwa kufikia 200 ili kuweza kuwatishia ama kuwajeruhi wananchi ambao hawatakipigia kura Chama hicho.
 
Alisema lengo la Chadema ni kuhakikisha wananchi hawajitokezi kupiga kura katika uchaguzi ujao na ambao watakuwa wamejitokeza watawatishia ili wasikipigie kura chama kingine zaidi ya Chadema.
 
Aliongeza kuwa taarifa za uchunguzi ambazo Chama cha Mapinduzi kimebaini ni kuwepo kwa mkakati wa kuandaa vijana 50 kila kijiji nzima ambao watapata mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kufanya kazi katika uchaguzi ujao.
 
Madodi alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema inaweza ikaliingiza taifa katika machafuko jambo ambalo linaweza kupelekea vikundi vya kigaidi kujipenyeza na kuja kufanya mashambulizi.
 
Kwa upande wake Kamada wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa watu wawili wakiwa na silaha hizo lakini alisema uchunguzi bado unafanyika ili kubaini kama ni kiongozi wa Chama cha siasa.
 
Naye Mwenyekiti wa usalama wa Chadema, Aron Siwale alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alikiri kukamatwa kwa kiongozi wa Redbriged Wilaya ya Momba na kuongeza kuwa alikuwa akielekea kuhamasisha vijana kujiunga na Chama na sio inavyoolezwa.
 
Alisema kuhusiana na kukamatwa na silaha hawezi kulitolea ufafanuzi hadi hapo Jeshi la Polisi litikapothibitisha lakini wao wanachojua ni kukamatwa kwa kiongozi huyo akiwa anaelekea Chitete akitumia usafiri wa boda boda.

Na Mbeya yetu
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni