Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi
Na Michael Katona, Njombe
WANAFUNZI wa shule za Sekondari nchini wametakiwa kuwa na
utulivu wakati wakiwa Hosteli ili kupata muda mzuri wa kusoma na kuacha mara
moja kupigiana ‘story’ ambazo zitawafanya wasiwezeshwe na wasijiwezeshe.
“Wanafunzi wasichana mmejengewa hosteli ili muwe na utulivu,
muwe na muda mzuri wa kusoma, lakini sina uhakika sana hizo hosteli ‘story’
mnazopigiana ni za namna gani, Matron
inabidi uwe unapita unasikiliza vile vi ‘story’ vyao, hivi ni ‘story’ za
Jiography, Mathematics, Physics , Biology za Kiswahili, ni ‘story’ gani?”
alisema Dk. Rehema Nchimbi mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Akihutubia wananchi wakati wa kilele cha sherehe za Siku ya
Wanawake Duniani ambazo Kimkoa zilifanyika katika Kijiji cha Lole, Kata ya
Ikuna, Wilaya ya Njombe Vijijini, Dk. Nchimbi alisema mbali ya kuwawezesha
wasichana hao, bila shaka muda mwingi wanautumia kwa mambo ambayo yanafanya
wasijiwezeshe.
“Mnaweza mkawawezesha hawa wasichana, lakini muda mwingi
wanautumia kwa mambo ambayo yanafanya wasijiwezeshe na wasiwezeshwe, tumieni
vizuri sana muda wenu nyinyi wasichana mnapokuwa shuleni, jamii imewajengea
hosteli, wazazi wanachangia ili muweze kuishi vizuri, tulieni na kila dakika
muone mnathamani kubwa kwa ajili ya kuwezeshwa,” alisema Dk. Nchimbi.
Alisema haiwezekani mwanafunzi anayeishi katika hosteli kwa
miaka minne halafu anafeli jambo ambalo alisema linamshangaza.
“Haiwezekani kwa miaka mine unakuwa hosteli halafu unafeli,
kwa nini ufeli, na huko hosteli? Ukiwa nje ya hosteli unalalamika, unasema
unajua nikienda nyumbani ninachota maji mara na kwenda wapi, wavulana na pita
wananifinyia macho, sasa nani anakufinyia macho hosteli?,” aliuliza Dk.
Nchimbi.
“Kwa nini husomi vizuri wakati ukiwa hosteli, harafu badala
ya kufinyiwa macho, wewe mwenyewe ndiyo unafinyafinya macho, daftari,vitabu
huoni vizuri, halafu unaanza kusingizia wengine, tunaposema uwezeshaji wa
wanawake tuna maanisha kwamba ni haki kuwezeshwa, lakini wanawake sisi tunawajibu
kuhakikisha kwamba tunaheshimu, tunathamini, tunatambua na tunatendea haki kwa
uaminifu na uadilifu fursa mbalimbali, ” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Nchimbi aliendesha harambee ya
kuchangia ujenzi wa madarasa kwa ajili ya shule ya msingi Lole iliyojengwa
tangu mwaka 1976 ambayo iko katika hali mbaya ya uchakavu wa madarasa kwa
kukusanya jumla ya shilingi 1,320,000, ambapo ahadi zikiwa ni shilingi 830,000
huku fedha taslimu ni sh. 490,000. Pia jumla ya miche ya miti 500 ilipatikana
katika harambee hiyo huku bati 50 kwa ajili ya kuezekea darasa zikiahidiwa
kutolewa na Shirika la EADD.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni