MKUU wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi
akizungumza na Daina Mangula ambaye ni mshindi wa ufugaji bora Afrika Mashariki
na kwa nchi 133 barani Afrika juu ya ufugaji bora wa Ng’ombe wa Maziwa. Kushoto
ni Mkurugenzi wa Shirika la Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika ya
Mashariki (EADD) Mark Tsoxo.
Mkurugenzi wa Shirika la Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika ya
Mashariki (EADD) Mark Tsoxo akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi wakati alipotembelea na kukagua banda la maonyesho la EADD.
Na
Michael Katona, Njombe
MKUU
wa mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanawake mkoani Njombe kuchangamkia
fursa zinazotolewa sasa na mashirika ya misaada ya kimataifa katika suala la ufugaji
wa Ng’ombe wa Maziwa, ambao utasaidia kupata kipato na kuboresha maisha yao kwa
ujumla.
“Katika
suala la uwezeshaji wanawake, Shirika la Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa
Afrika ya Mashariki (EADD), Mkurugenzi, Afisa Mifugo, Afisa Biashara ninataka
ndani ya mwaka huu mmoja muwe mmetuwezesha kuonyesha kila dalili ya Njombe
kuuza maziwa na kutawala soko la maziwa hapa Tanzania,” alisema Dk. Nchimbi.
Akizungumza
katika kilele cha siku ya wanawake Duniani, sherehe hizo Kimkoa zilifanyika
katika Kijiji cha Lole, Kata ya Ikuna, Tarafa ya Makambako wilaya ya Njombe
Vijijini, aliupongeza mradi wa EADD awamu ya pili unaondelea hivi sasa wa kopa
Ng’ombe lipa Ng’ombe katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ya Njombe, Iringa na
Mbeya utaweza kuboresha maisha bora endelevu kwa watu milioni moja katika nchi
za Uganda, Kenya na Tanzania ifikapo mwaka 2018.
Mkurugenzi wa Shirika la Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika ya
Mashariki (EADD) Mark Tsoxo akiwa na wafanyakazi wenzake wakati wakizungumza na
wananchi wa Kijiji cha Lole, Kata ya Ikuna mkoani Njombe.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba akipata maelezo kutoka
kwa wafanyakazi wa Shirika la Mradi wa Uendelezaji Sekta ya Maziwa Afrika ya
Mashariki (EADD) alipotembelea banda la maonyesho kwa ajili ya kutoa darasa la
ufugaji bora wa Ng’ombe wa maziwa.
“Msingi
mkubwa wa ufugaji ni wanawake, kwa hiyo ndugu zangu wa EADD, Serikali ipo
tayari kushirikiana nanyi, lakini lazima tushirikiane kwa malengo, ninachotaka nikuona
mkoa wa Njombe unaachwa kusemwa semwa sasa kwa mambo ambayo si yake, Njombe ni
nzuri, hali ya hewa ni nzuri, ardhi na mazingira yake ni mazuri,” alisema Dk.
Nchimbi.
“Nataka
iwe Njombe ambayo inasafirisha Maziwa nchi nzima, na Tanzania nzima ibadilike
na kunywa maziwa ya Njombe, msingi mkubwa wa ufugaji ni wanawake na katika
mnyororo huo wa thamani kuna wakina mama ambao nataka maafisa Kilimo, Biashara,
Ufugaji tuwasaidie kulima na kuzalisha malisho,” alisema.
Mkuu
huyo wa mkoa wa Njombe aliitaka EADD kwa kushirikiana na maafisa hao kuyatumia
kuwa kauli mbiu yao tekelezeki ambayo inatekelezwa sasa.
“Katika
kauli mbiu ya siku ya wanawake inasema “Wezesha wanawake, tekeleza wakati ni
sasa” hivyo mwaka huu mwishoni tutakutana tukae tufanye tathimini kuona
tumefikia wapi katika kufanikisha hilo, wakulima wakubwa wa malisho wawe ni
wanawake, wafugaji wakubwa wazuri na waaminifu wawe wanawake,” alisema Dk.
Nchimbi.
Alimpongeza
mwanamke Daina Mangula ambaye alikuwa
mshindi wa ufugaji bora katika nchi 133 akitoka kijiji cha Ibumila, Kata ya
Kichiwa mkoani Njombe, kwa kuwa mfano mzuri wakuigwa na wanawake wengine katika
suala la kujifunza ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa.
“Wanawake
ni waaminifu sana katika shughuli zozote zile na hasa zinazohusiana na chakula
na afya, wanawake hawawezi kuuza maziwa ambayo wameambiwa wakati wake wa kuuza
haujafika, lakini wengine kwa tamaa ya fedha wanakamua kabla ya siku,” alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa EADD, Mark Tsoxo aliishukuru serikali kwa
kushirikiana nao kuboresha maisha ya wafugaji wanawake kwenye mikoa ya Njombe,
Iringa na Mbeya na katika kutekeleza hilo, EADD imekubali kumsaidia mwanamke
Wema Kingimbwiti mkazi wa Ikuna ambaye mlemavu na mwimbaji wa kwaya, mtaji wa
shilingi milioni moja katika eneo la ufugaji.
“Tutakwenda
na wataalamu wetu anakoishi kufanya tathimini na kuona kipi ambacho anakiweza,
sisi tutamtayarishia mpango wa biashara, tutahakikisha anapata mtaji usiopungua
thamani ya shilingi milioni moja,” alisema Tsoxo.
Naye
Lightness Munisi, Afisa Maendeleo ya Jamii na Jinsia wa Mradi wa EADD, alisema
malengo ya mradi ni kusaidia wafugaji 35,000 wa ng’ombe wa maziwa nchini
Tanzania, katika maeneo yenye fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji.
Akielezea
mradi wa EADD ulivyoanza na mafanikio makubwa, Afisa Mawasiliano Rachael Singo
alisema ulianzishwa mwaka 2008 kwa ufadhili wa Bill & Millinda Gates
Foundition na umeweza kutoa mafunzo ya ufugaji bora kwa nchi za Uganda, Kenya
na Rwanda huku kwa upande wa Tanzania mradi huo unategemewa kuongeza wigo na
kuunganisha nguvu ya pamoja ya wafugaji na usawa wa kijinsia katika kaya 36,000 nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni