Ijumaa, 6 Machi 2015

JK azindua kituo cha Azam TV, ataka kuboreshwa kwa maslahi ya waandishi wa habari

JK azindua kituo cha Azam TV, ataka kuboreshwa kwa maslahi ya 

waandishi wa habari


Rais Jakaya Kikwete amewataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuwajengea uwezo waandishi wa habari kwa kuwapatia mafunzo kila mara, pamoja na kuboresha maslahi yao kwani wakishindwa kuwalipa vizuri, waandishi hao watalipwa na watu wa mtaani jambo ambalo linaweza kupunguza weledi.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua rasmi kituo cha Televisheni cha Azam kinachomilikiwa na Kampuni ya Said Salim Bhakresa(SSB) huku akimmwagia sifa Mwanyekiti wa Kampuni hiyo Said Salim Bakresa kwa kueleza kuwa uwekezaji alioufanya utaongeza ushindani katika sekta ya habari.
Aidha amekitaka chombo hicho kuweka mbele maslahi ya utaifa kwa kuchuja habari zinazotakiwa kutangazwa kwani hata mashirika makubwa ya habari duniani kama vile BBC na CNN nao wanazingatia utaifa wao kwanza.
“Tanzania ni moja ya nchi zilizofanya vizuri katika kuhama kutoka kwenye mfumo wa habari wa analogia kwenda digiti kwa ubora wa hali ya juu hivyo kuzinduliwa kwa Studio za Azam TV kutaendeleza kuongeza ufanisi wa ubora wake,”Amesema Rais Kikwete.
Amesema sekta ya habari ni moja ya mhimili mkubwa hapa nchini ambao kazi yake ni kuhakikisha kuwa suala la Demokrasia linaendelea kukua na kuthaminiwa, hivyo Serikali itaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari kwa kutunga sheria zisizo kandamizi.
Amesema ubora wa vipindi, teknolojia sahihi na waandishi na watangazaji wenye weledi mkubwa utakuwa chachu katika kuifanya Azam tv iweze kutoa bidhaa bora hivyo kuongeza ushindani .
Aidha amesema uwekezaji wa ndani kwa Mtanzania unaleta heshima kwa Taifa la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuongeza pato la mtanzania na kupunguza adha ya ajira inayoendelea kukua kila siku nchini.
"Siku zote penye bidii penye maarifa penye mipango ya uhakika hakuna kisichowezekana, hawa jamaa wameanzia mbali sana bidiii imewafanya wafikie mahali hapa walipo:- aliongeza, Tumezoe kula vitu vya Azam, kunywa vitu vya Azam, kushabikia timu ya Azam na sasa tutasikiliza Azam, hii ni kazi nzuri kwa taifa hili alipongeza Rais Kikwete"
Amesema kampuni ya Said Salim Bhakres (SSB) ni moja ya kampuni inayoongoza kwa kutoa ajira mbalimbali kwa watanzania hapa nchini, pia wanaongoza katika kulipa kodi stahiki za mapato hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi.
Aidha Rais Kikwete amewataka wafanyakazi wote wa kampuni hiyo kuendelea kusimamia sera ya ubora wa bidhaa, hivyo hata kwenye bidhaa ya utangazaji wajikite katika suala hilo la ubora.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni