TBA WAPEWA WIKI MBILI KUKARABATI MAJENGO MAWILI
WAZIRI wa Ujenzi Dkt. John Magufuli ametoa siku 14, kwa Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), kuanza ukarabati wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Siha na Moshi baada ya kubainika majengo hayo kujengwa chini ya kiwango.
Dkt. Magufuli pia ameagiza aliyekuwa meneja wa TBA Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Ndossa kusimamishwa kazi mahali alipo ili arejee kujibu tuhuma na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri huyo alitoa agizo hilo wakati akikagua jengo la mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro baada ya kupewa taarifa za jengo hilo kujengwa chini ya kiwango hali iliyosababisha shughuli za mkuu wa Wilaya ya Siha kuhamishiwa kwenye ofisi za maji za halamashauri hiyo.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji mkuu wa TBA Elius Mwakalinga alisema wakala hao wanasikitishwa na kasoro za kiufundi zilizojitokeza katika jengo hilo na watawachukulia hatua wote waliohusika katika kuchangia majengo hayo kuwa chini ya kiwango.
Mwakalinga amesema tayari TBA imefanya tathmini ya gharama za ukarabati wa jengo la Wilaya ya Siha ambao utafanyika katika kipindi cha wiki 18 na kugharimu shilingi milioni 50.
Majengo ya ofisi za wakuu wa Wilaya za Siha na Moshi yalijengwa kwa usimamizi wa TBA ambapo wahusika walishindwa kuyatumia wakihofia usalama wao baada ya kuona dosari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni