Jumatatu, 23 Machi 2015

MAMA WA ALBINO ALIYEKATWA MKONO AJIFUNGUA, AHITAJI MSAADA


Bi. Prisca Shaaban Mpesya akiwa na binti yake Lucia (2) katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya huku naye akiuguza jeraha lake la kichwani. (Picha zote na brotherdanny5.blogspot.com).
Baraka Cosmas (5) aliyekatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiojulikana.


Ndugu zangu,
Licha ya kuuguza jeraha la kichwani pamoja na kumuuguza mtoto wake mdogo mwenye ulemavu wa ngozi (Albino) aliyekatwa mkono na watu wasiojulikana, Bi. Prisca Shaaban Mpesya (28) amejifungua usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Bi. Prisca, mkazi wa Kitongoji cha Kikonde, Kijiji cha Kaoze katika Kata na Tarafa ya Kipeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa, alifikishwa hospitalini hapo Machi 8 mwaka huu baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana waliomjeruhi kichwani kwa kitu kizito kabla ya kumkata kiganja mwanawe Baraka mwenye albinism Machi 7, mwaka huu majira ya saa 2 usiku.
Taarifa zilizoifikia brotherdanny5.blogspot.com zinaeleza kwamba, mzigo alionao Bi. Prisca ni mkubwa kwa sasa kwani ana watoto watatu hospitali ambao ni mwanawe majeruhi Baraka Cosmas Yoramu (5), Lucia Cosmas Yoramu (2) na huyo mchanga, huku akiwa hana msaada wowote.
Ndugu zangu, kwa hakika mama huyu anahitaji msaada wa hali na mali, kwani licha ya mzigo unaomkabili sasa wa jeraha la kichwani pamoja na ulezi wa watoto watatu hospitalini, lakini bado mazingira anayoishi huko kijijini ni magumu huku akiwa na jumla ya watoto wqenye albinism watatu ambao wako hatarini.
Mmoja wa watoto hao wenye ulemavu aitwaye Shukuru (8) amemwacha kijijini ambako mazingira pia siyo salama, huku mumewe akiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
Rai yangu kwa wanajamii ni kwamba tujitokeze kumsadia mama huyo na watoto wake na blogu hii bado inafuatilia taarifa zaidi ili kupata mawasiliano ya namna misaada inavyoweza kumfikia.
 Hii ndiyo nyumba ya Bi Prisca iliyoko katika Kitongoji ya Kikonde, Kijiji cha Kaoze wilayani Sumbawanga, ambako anaishi na watoto wake wanne huku watatu wakiwa na albinism.
 Mlango pekee wa nyumba hiyo ambao siyo imara
 Haya ndiyo mazingira ya ndani, hizo alama nyeusi juu na picha ya chini ni damu iliyotapakaa baada ya watu wasiojulikana kukata kiganja cha mtoto Baraka na kutoweka nacho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni