Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) inadaiwa kuwa unakusudia kumsimamisha Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba kuwania urais mwaka huu dhidi ya wagombea wa vyama vingine, kikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM).
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Ukawa vimeeleza kwamba, uamuzi wa kumsimamisha Jaji Warioba unazingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo kuepuka mvutano baina ya vyama hivyo vinne vinavyounda umoja huo.
Hata hivyo, pendekezo hilo linaweza kugonga mwamba kwani Jaji Warioba amesema amemaliza kazi aliyotumwa ya kusimamia ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya ambayo aliifanya kwa uadilifu mkubwa.
Akizungumza na Gazeti hili kwa njia ya simu akiwa nje ya nchi, Jaji Warioba aliomba kutohusishwa na masuala ya siasa kwa sasa, kwani anahitaji kupumzika baada ya kumaliza wajibu wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Warioba ambaye mwaka 1995 aliwahi kuwania urais kabla ya kushindwa katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi, alisema kama angekuwa na haja hiyo, basi angegombea kupitia CCM na si vinginevyo.
“Nahitaji kupumzika sasa, nimemaliza kazi jamani. Kama ningeutaka urais, basi ningegombea kupitia chama changu cha CCM,” alisema.
Ukawa wanatarajiwa kukutana Jumanne hii kujadili mambo mbalimbali, ukiwemo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, ingawa haijajulikana kama ajenda ya pendekezo la kumsimamisha Jaji Warioba itakuwa mojawapo.
“Wanataka kuepuka mvutano wa nani miongoni mwao atakayegombea, kwani imebainika huko nyuma umoja kama huo, ambao haukuwa rasmi, uliwahi kuvunjika kutokana na kila kiongozi wa chama kutaka agombee urais,” kilisema chanzo hicho.
Kikaongeza: “Warioba kwa sasa ni mtu huru, bado yuko CCM, lakini anaweza kuombwa aje huku kwani pande zote zinamkubali na anaweza kuwa chaguo sahihi kuliko viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa kwa sasa.”
Chanzo kingine kimeeleza kwamba, sababu nyingine inayowapa nguvu Ukawa kumsimamisha Warioba ni kutokana na mchango wake mkubwa alipoiongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuandaa rasimu inayotajwa kwamba ingeweza kuondoa kero nyingi kama siyo kudaiwa kuchakachuliwa wa wabunge wa CCM katika Bunge Maalum la Katiba mwaka jana.
Inaelezwa kwamba, akiwa Mwenyekiti wa Tume hiyo pamoja na wajumbe wake, Jaji Warioba alifanya kazi nzuri, lakini CCM wakampuuza, kumtukana na hata kunusurika kupigwa na kundi la wanachama, achilia mbali kuichakachua rasimu hiyo na kupinga muundo wa Muungano wa Serikali Tatu uliopendekezwa.
“Uchakachuaji wa rasimu hiyo ndio uliozaa Ukawa, kwa hiyo Jaji Warioba anakubalika kwa asilimia zote na ikiwa uamuzi huo utafikiwa na yeye akakubali, basi ataeleta ushindani wa kutosha dhidi ya mgombea wa CCM.
“Jaji anakubalika hata na wananchi wengi ambao wanaamini Tume yake ilikuwa inawaletea tiba ya changamoto zao za miaka mingi, hata wanaCCM wanamkubali,” kiliongeza chanzo hicho.
Oktoba 26, 2014, vyama vinne; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, vilifikia makubaliano saba ya muungano wao ambayo ni pamoja na kuhusisha sera zao na kuchukua yote yanayofanana ili viwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.
Pili; kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye chaguzi zote kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge, uwakilishi na urais kwa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Tatu; kuweka utaratibu wa namna gani vyama hivyo vingeshirikiana kwenye uchaguzi wa mitaa uliofanyika Desemba 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nne; kushirikiana kuelimisha umma kupiga kura ya ‘Hapana’ katika mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalum la Katiba.
Tano; kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za msingi zenye maslahi kwa Watanzania.
Sita; kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya kimaslahi kama ilivyojitokeza kwenye katiba inayopendekezwa, na mwisho, kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja baina yao na asasi nyingine.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alizitaja taarifa hizo kama propaganda za CCM kutaka kuharibu harakati za wapinzani nchini.
“Hizi ni taarifa za uongo uliopitiliza na propaganda za CCM, hatuna haja ya kuzungumzia suala hilo kwa sababu mara nyingi wamemhusisha Jaji Warioba na Ukawa wakati syo kweli,” alisema.
Aliongeza kwamba, Watanzania wanatakiwa kuelimishwa kuhusu mambo ya msingi kama kura ya maoni ya katiba, daftari la kudumu la wapiga kura, kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na mambo mengineyo ya msingi badala ya propaganda.
Akizungumza na gazeti moja la kila siku mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alithibitisha kuwepo kwa kikao hicho kesho Jumanne akisema kutakuwa na ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda nyingine zitakazojadiliwa ni kura ya maoni ya Katiba, changamoto za uandikishaji wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka jana.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta majibu ya changamoto zilizopo kwa sasa.
Kiongozi huyo pia alithibitisha taarifa kuwa kila chama ndani ya Ukawa kupitia vikao vyake kitateua majina ya wagombea ambao watashindanishwa ndani ya umoja huo, na kwamba kabla ya Machi, jina la mgombea urais ndani ya chama chake litakuwa limeshapendekezwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni