Alhamisi, 12 Machi 2015

Jaji Mkuu aitaka dola ijipange kesi za mauaji ya albino

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amevitaka vyombo vya dola vinavyohusika na uhalifu, kujipanga kikamilifu kushughulikia kesi za mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Jaji Chande alitoa wito huo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya hafla ya kuwaapisha Manaibu Wasajili 43 wa Mahakama ya Tanzania kwenye Viwanja vya Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam.
“Taasisi zinazohusika na uhalifu zinapaswa zijiandae. Sisi Mahakama tumeshaanza kuchukua hatua na tutazipa kipaumbele kesi za mauaji ya albino na tutazipa kipaumbele hata katika ngazi ya rufaa,” alisema Jaji Chande na kuongeza:
“Bidii lazima zifanyike katika kufanya upelelezi mzuri na mashahidi wajitokeze. Sisi Mahakama tuko tayari kushughulikia mashauri hayo.”
Akionyesha jinsi ambavyo Mahakama imechukua hatua katika kushughulikia kesi hizo, Jaji Chande alisema kesi hizo zilikuwa zimeshafikia 90, lakini hadi sasa zimebaki kesi mbili katika Mahakama Tabora na tatu Mwanza.
Akizungumzia uteuzi wa manaibu wasajili hao, Jaji Chande alisema kuwa wameteuliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama, ikiwa ni hatua ya kutekeleza muundo mpya wa utendaji wa Mahakama baada ya kutenganisha shughuli za utoaji haki na shughuli za utawala.
Alisema manaibu wasajili hao watapelekwa katika vituo mbalimbali vya Mahakama, ambapo wawili kati yao ni manaibu Wasajili Waandamizi wa Mahakama ya Rufani.
Alisema wengine watapelekwa katika Masjala Kuu, Masjala za Divisheni za Mahakama Kuu na katika Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu katika kanda mbalimbali.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi Shabani Lila alisema vipaumbele ambavyo wateule hao watapaswa kuzingatia katika utendaji wao ni pamoja na kusikiliza na kuamua mashauri kwa wakati, kuwawezesha wananchi kuifikia Mahakama kwa urahisi na kupafanya kuwa mahali pa kukimbilia.
Alivitaja vingine kuwa ni kutoa kwa wakati huduma, ambazo mwananchi anahitaji, mfano nakala za hukumu, utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama na nyinginezo.
Naye mmoja wa wateule hao Hakimu Richard Kabate, alisema licha ya kupewa majukumu magumu, lakini watajitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni