Okwi alisema aliomba likizo ili kukamilisha masuala yake ya kifamilia na uongozi wa Simba ulimruhusu na wakati anaondoka hakuambiwa anatakiwa kurudi lini kujiunga na timu yake.
“Sikupewa muda wa kurudi, nashangaa watu wanavyosema nimechelewa kurudi, ni kweli niliomba kupumzika mara baada ya kusaini mkataba na uongozi ukaniambia sawa,” alisema Okwi.
“Nafurahi kuwa hapa tena na wenzangu kwa sasa nipo tayari kuanza kazi ya kuisaidia timu yangu kwa nguvu, mwili wangu umepumzika sasa nataka kucheza.
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema alikutana na uongozi wa klabu hiyo na kumtaka kuwa mpole kidogo kwa kuchelewa kwa Okwi kutokana na wao kujichanganya na kumpa likizo hiyo.
“Nimekutana na uongozi wa juu wameniambia kwamba natakiwa kupunguza jazba kwa kuchelewa kwa Okwi, wameniambia kwamba nimvumilie kidogo atakuja,” alisema Mserbia huyo ambaye alitoa saa 24 kwa Mganda huyo kujiunga na kambi yake.
“Huu ni uamuzi uliochukuliwa huko nyuma, lakini namtaka atambue kwamba umuhimu wake utatoka katika maeneo, mawili kuifungia Simba au kutengeneza nafasi za mabao.” Awali, Makamu wa Rais wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alimsema kutokuwapo kwa Okwi katika timu hiyo kunatokana na ruhusa maalumu aliyopewa ya kwenda kumalizia taratibu za ndoa yake aliyoifunga wiki mbili zilizopita.
“Tuna taarifa kamili juu ya kutokuwapo kwa Okwi, aliutaarifu uongozi kwamba anakwenda kumalizia taratibu nyingine za ndoa yake ambazo huko nyuma alizikatisha.” Simba kesho itashuka uwanjani kuikabili Mtibwa Sugar katika fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni