Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Rehema Nchimbi wakipokea maandamano ya kilele cha Siku ya Ukimwi Kitaifa
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal akihutubia
Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga akiwa na mkuu wa mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi akicheza muziki pamoja na wana kwaya wa KKKT Makambako
Na Michael Katona, Njombe
MKUU wa Mkoa wa Njombe, Dk.
Rehema Nchimbi amemweleza Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal na wananchi
wa mkoa wa Njombe kuwa anapenda kufanya kazi katika mkoa ambao hauna maambukizi
ya VVU.
“Hili ndilo tukio langu la
kwanza la kitaifa tangu ni hamie kuwa mkuu wa mkoa wa Njombe, wananchi wa
Njombe nimefika Njombe, naipenda Njombe, na niko tayari kufanya kazi Njombe,
lakini ni Njombe ambayo haitakuwa na Ukimwi,” alisema Nchimbi.
Mkuu huyo wa mkoa alikuwa
akitoa salamu zake kwa mgeni rasmi Makamu wa Rais wakati wa maadhimisho ya siku
ya Ukimwi Duniani, ambapo Kitaifa yalifanyika mkoani hapa kwenye uwanja wa
Sabasaba.
“Wakati kiwango cha
maambukizi ya VVU kikishuka Kitaifa kutoka asilimia 5.7 mwaka 2007/08 hadi
kufikia asilimia 5.1 mkoa wa Njombe mwaka 20011/12 mkoa wa Njombe kiwango cha
maambukizi kiliongezeka hadi kufikia asilimia 14.8,” alisema Nchimbi.
“Mh. Makamu wa Rais hali hii
haikubaliki na haikubaliki kabisa na hasa kwa Njombe hii ya sasa, mkoa umeandaa
mpango wa utekelezaji kwa miaka mitatu ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu mwezi
Julai mwaka jana, na mpango huo ulianza kutekelezwa mwezi huo huo mwaka jana,”
alisema Dk. Nchimbi.
Mkuu huyo wa mkoa alitaja
mpango huo ulipojikita zaidi kuwa ni katika suala la kinga dhidi ya maambukizi
ya virusi vya Ukimwi, kupunguza mila na desturi potofu zinazoweza kuchangia
kasi ya maambukizi ya Ukimwi, kudhibiti kasi ya maambukizi ya VVU kwa vijana,
pia kutoa tiba na msaada kwa wagonjwa wa Ukimwi majumbani na wengine wanaoishi
na VVU na utoaji wa dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa ukimwi na wale
wanaoishi na maambukizi ya VVU,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Aidha Nchimbi alisema katika
mkakati huo, kwa mkoa wake wa Njombe umeanza kuonyesha mafanikio makubwa,
ambapo idadi ya vituo vya huduma inavyotoa huduma ya tohara kwa wanaume
vimeongezeka kutoka vituo 7 hadi kufikia vituo 13 Juni mwaka huu.
Sambamba na hilo, Dk.
Nchimbi alisema asilimia ya maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yamepungua kwa
kasi kutoka asilimia 12.5 hadi asilimia 9.6 na kueleza kuwa tangu mkoa wa
Njombe ulipoanza kuadhimisha maadhimisho hayo kuanzia Novemba 24 na kufikia
kilele chake Desemba Mosi, kumekuwa na upimaji wa hiari kwa wananchi, na kwamba
lengo lilikuwa ni kupima watu 3,000, lakini hadi kufikia Novemba 30, mwaka huu jumla ya
watu 6,367 waliopimwa kati yao watu 328 walionekana kuwa na virusi vya ukimwi
na hiyo ni sawa na asilimia 5.2.
Nchimbi alisema katika
takwimu za TACAIDS zimeonyesha wilaya ya Makete ndiyo inayoongoza kwa
maambukizi ya VVU ambapo ina asilimia 7.2, na Ludewa ina maambukizi machache ya
asilimia 2.5.
“Hakika tukiamua inawezekana
na tunaweza kabisa kuwa na Njombe isiyo na maambukizi mapya ya Ukimwi, Njombe
isiyo na unyanyapaa na tunaweza kabisa kuwa na Njombe ambayo haina vifo
vinavyotokana na Ukimwi,” alisema Nchimbi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Njombe alimwomba Makamu wa Rais kuwe na
mkakati na dhamira ya kweli ya kufikia mahali kusiwe na siku ya ukimwi
Tanzania.
“Inawezekana kabisa kuwa na mfumo wa kitaifa wa kuiondoa
Njombe yenye sifa ya muda mrefu yakuwa kinara wa maambukizi ya ukimwi, hii ni
Njombe yenye hadhina kubwa sana ya madini ya Chuma, Makaa ya Mawe na
inayostawisha mazao mengi, sasa lazima tufike mahali tuwe na Njombe ambayo
haina jina la kuwa kinara wa maambukizi ya Ukimwi, hivyo Njombe inatakiwa iwe
ni lango kuu lenye rasilimali kwa uchumi wa Tanzania,” alisema Dk. Nchimbi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni