Walemavu wakuongea na kutokusikia (viziwi) wakifurahia kuangalia noti halali ya Tanzania wakati wa Semina ya kutambua noti halali iliyotolewa mjini Njombe jana na Maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Na Mwandishi Wetu, Njombe
Taasisi za Fedha na Benki mbalimbali nchini
zimelaumiwa kuwa zimekuwa zikifanya unyanyasaji kwa walemavu wasiojiweza pindi
wanapokwenda kupata huduma za kifedha.
Malalamiko hayo yatolewa juzi mkoani Njombe wakati wa
semina iliyokuwa ikiendwa na Benki Kuu Tanzania (BOT) kwa walemavu viziwi na
wasioweza kuzungumza kutoka shule ya Viziwi ya mkoani hapa kwa ajili ya kuwapa
uelewa wa kuzitambua noti halali na bandia.
Wakizungumza kwenye semina hiyo iliyofanyika katika
hoteli ya Miriam, baadhi ya washiriki wa semina hiyo walidai kwamba, wamekuwa
hawafurahishwi na tabia ya baadhi ya watoa huduma kwenye benki hizo wakati
kwenda kupata huduma za kifedha au kutaka kufungua akaunti kufuatia wafanyakazi
wa vitengo hivyo kuwapa majibu yasiyoyakistaarabu.
“Nilipoomba kufungua akaunti katika benki moja hapa
mjini Njombe (jina la benki tunalihifadhi) walisema kwa sisi hatuwezi
kukufungulia akaunti, kwa sababu wewe ni kiziwi, nililia niliumia kweli,”
alidai mshiriki huyo na kukataa kutaja jina lake.
Alisema kufuatia hali hiyo ilimbidi amtufate bosi wake
kwa ajili ya kwenda kuzungumza na wafanyakazi wa benki hiyo ili wamsaidie
kufungua akaunti hiyo.
“Alipokuja bosi wangu, niliwauliza wafanyakazi hao wa
benki, kama asingekuja bosi huyu, je walemavu wengine ambao ni bubu na
wasiosikia wangepataje huduma zenu?” alisema mshiriki huyo.
Mlemavu huyo ambaye ni kiziwi aliwataka maofisa hao wa
BOT waliokuwa wakitoa mafunzo hayo kuwasiliana na benki na Taasisi za fedha
nchini kuondoa kero ambayo wamekuwa wakikutana nayo walemavu mbalimbali hususan
vipofu, walemavu wa miguu na wasiosikia ili kupata haki sawa kama raia wengine
nchini.
“Naomba mabenki yote ya binafsi au taasisi za serikali
waelimishwe kuhusu kuwapokea viziwi, kwa sababu wote ni binadamu au sisi viziwi
hatukupenda kuwa hivi,” alisema.
Akizungumzia juu ya malalamiko hayo, Meneja Msaidizi
wa kitengo cha Sarafu kutoka BOT, Abdul Dollah alisema anakubaliana na madai
hayo kwa kuwa katika sehemu nyingi duniani kuna baadhi ya majengo yanayokuwa na
ofisi za kifedha kutokuwa rafiki kwa walemavu.
“Majengo mengi hapa nchini yaliyojengwa wakati huo
hayakuwa rafiki kwa walemavu wanaotumia baiskeli za miguu mitatu, hivyo ni
vyema hivi sasa mabadiliko yafanyike ili kuweza kuwasaidia wenye tatizo la
kufika kupata huduma,” alisema Dollah.
Awali akifungua semina hiyo ya mafunzo kwa viziwi,
Meneja Msaidizi kutoka kitengo cha Sarafu BOT Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
iliyopo Mbeya, Grolia Mwaikambo alisema Mkurugenzi wa Kikundi cha Sanaa na
Viziwi Tanzania, Habib Mrope aliomba ufadhili wa kupata pesa kutoka BOT kwa
ajili ya kutoa mafunzo kwa viziwi ili yaweze kuwasaidia kutambua noti halali na
zile za bandia.
“Lengo letu ni kuisukuma serikali kutoa elimu ya
mafunzo kwa hawa walemavu wa viziwi kufahamu na kutambua pesa halali na pesa
bandia, ndiyo maana tumeanza kufanya semina hii katika mkoa wa Njombe, lakini
pia tunakwenda kwenye mikoa ya Ruvuma na Singida kwa ajili ya kutoa elimu hiyo,”
alisema Habib Mrope kwenye semina hiyo.
Naye Vicky Msina ambaye ni Meneja Uhusiano Msaidizi
kutoka Idara ya Uhusiano wa Umma (BOT), alisema wameanzisha semina hiyo kusaidia hasa walemavu wasioona na ambao
hawasikii kuweza kugundua utapeli wowote utakaokuwa ukifanywa na watu wenye nia
mbaya dhidi ya walemavu hao kwa kuwa wao pia baadhi yao wanafanyabiashara
mbalimbali hapa nchini.
“Semina hii itasaidia sana kuweza kuwakamata watu
wanaotawanya pesa za bandia, na vilevile itawasaidia walemavu kuwabaini wadanganyifu
wanaotumia pesa zisizo halali kwenye maeneo yao ya biashara,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni