Wanafunzi wakiwa chini ya ulinzi wa polisi
Na Michael Katona, Njombe
KUFUATIA wanafunzi wa shule
ya Sekondari Njombe (NJOSS) kufanya vurugu kubwa juzi ikiwemo ya kuchoma moto
bweni na kuteketeza jengo hilo, Jeshi la Polisi Mkoani Njombe limetaja majina
ya wanafunzi 15 ambao wanashikiriwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Kamanda wa Jeshi la Polisi
mkoani hapa, Fulgence Ngonyani jana ametoa taarifa yake na kuwataja majina
wanafunzi ambao watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo mara upelelezi
utakapokamilika.
Ngonyani aliwataja wanafunzi
hao wanaosoma kidato cha tano na sita kwenye shule ya Njombe Sekondari kuwa ni
Juma Maganga, Seme Charles, Riwad Ngowi, Martin Mhagama, Kenedy Kibangali,
Jimmy Mkadenge na Shukuru Kilingo.
Wanafunzi wengine ni Linos
Lindu, Kalvin Kisiga, David Swela, Francis Emmanuel, Timothy Minga, Ezra
Charles, Johson Mbelele na Ndanga Obadia.
Katika taarifa hiyo ya jeshi
la polisi, Kamanda Ngonyani amesema wanafunzi hao walichoma moto karakana ya
shule, vifaa mbalimbali vya wanafunzi, walivunja duka la shule ambalo lilikuwa
na bidhaa mbalimbali zikiwemo soda na kunywa, kisha wakavunja chupa na kumwaga
soda hizo chini.
Pia wanafunzi hao walivamia
nyumba mbili za mwalimu mkuu wa shule na mwalimu wa nidhamu na kuvunja vioo vya
nyumba hizo sambamba na kuharibu gari namba T809BBX Toyota Carina.
Kamanda Ngonyani alitaja
thamani halisi ya mali zote zilizoharibiwa katika vurugu hizo ni Shilingi
113,050,000 Milioni. Alisema kiini cha tukio hilo ni kusimamishwa masomo kwa
wanafunzi 29 waliodaiwa kutoroka shuleni hapo mnamo Septemba 6, mwaka huu usiku
na kwenda kucheza disko katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Njombe
kilichopo jirani na shule hiyo.
Alisema wanafunzi hao wakiwa
kwenye ukumbi wa disko walifanya vurugu zilizosababishwa na kugombea wanawake,
kutokana na vurugu hizo mmoja wa wanafunzi hao alitoka ukumbini na kukimbia
ndipo alipoingia kwenye shimo na kuvunjika mguu.
“Wakati anahojiwa na uongozi
wa shule ni wapi aliumia mguu alijieleza kuwa alitoroka na wenzake kwenda disko
ndipo wakati anarudi akatumbukia kwenye shimo na kuvunjika mguu huo, lakini
wanafunzi wengine waliotajwa kwenda disco walikataa,” alisema Ngonyani.
Wanafunzi hao Oktoba 7,
mwaka huu walisimamishwa na uongozi wa shule hiyo, lakini siku hiyo majira ya
saa 3.00 usiku baadhi ya wanafunzi hao waliosimamishwa masomo na wengine ambao
hawajasimamishwa masomo wakaanzishaa vurugu hizo wakipinga maamuzi ya uongozi
wa shule hiyo.
Kufuatia vurugu hizo, Afisa
Elimu wa mkoa wa Njombe, Said Nyasiro juzi alitangaza kuifunga rasmi shule hiyo
hadi Novemba 8, mwaka huu, ambapo wanafunzi wote wametakiwa kurudi na fedha
shilingi 150,000 pamoja na barua yakujieleza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni