Alhamisi, 9 Oktoba 2014

MAKABIDHIANO YA RASIMU YA KATIBA DODOMA: RAIS KIKWETE: CCM WALINIPINGA KATIBA MPYA!


Rais Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Wetu,

Rais Jakaya Kikwete amesema mchakato wa katiba mpya kabla ya kuanza mwaka 2011, ulipingwa vikali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi, viongozi na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), baada ya zoezi la kukabidhiwa katiba inayopendekezwa na kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, mjini Dodoma Oktoba 8, mwaka huu.

Alisema alipata wakati mgumu, lakini alisimama imara kuhakikisha mchakato huo unaanza.“Jambo, ambalo wengi hawalifahamu, makundi pia yalikuwapo ndani ya Chama Cha Mapinduzi, walikuwapo baadhi walionihoji kuwa jambo hili umelizua kutoka wapi, hii siyo ajenda ya CCM, bali ya watu wengine.

Nikasema ni ajenda ya Watanzania na mimi ndiye mwakilishi mkuu. Baada ya mjadala mkali, tulielewana, ingawa wapo walioondoka shingo upande,” alisema Rais Kikwete.

Alisema baadhi ya wana-CCM waliokuwa wakali kwenye Halmashauri Kuu (Nec) na Kamati Kuu (CC) aliwateua kuwa wajumbe wa BMK na kwamba, walitoa msaada mkubwa na mchango ambao umewezesha kutungwa kwa katiba inayopendekezwa.

Rais Kikwete alisema mchakato ulianza mwaka 2011 na kwamba, safari hiyo ilikuwa na changamoto nyingi.Alisema mjadala ulikuwa mkali bungeni na nje na baadhi ya wajumbe walitoka nje.

Rais Kikwete alisema wakati anafungua BMK, aliwakumbusha wajibu wa wajumbe kuwa Watanzania wanategemea wawatungie katiba inayokubalika na wengi, itakayoimarisha Muungano, inayotekelezeka, itakayoondoa changamoto kwenye Muungano, kuimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

“Katiba inayosimamia demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu katika jamii, itakayoweka mazingira mazuri ya uchumi wa nchi kukua na kunufaika sawia na maendeleo yanayopatikana,” alisema Rais Kikwete.

Aliwapongeza wajumbe wa BMK kwa kuyatendea haki matarajio ya Watanzania kwa kuwa katiba inayopendekezwa inajumuisha maslahi ya makundi yote, inajali anayotaka kila mtu katika nchi yake, utu unaheshimiwa na haki zinazingatiwa.

KURA YA MAONI
Kuhusu kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa Katiba mpya, alisema kumekuwa na maoni tofauti lakini wanaendelea kutafakari ikiwamo kupitia vikao vya wawakilishi wa vyama vya siasa, na endapo itakubalika kura ya uamuzi ifanyike baada ya uchaguzi mkuu kutakuwa na ulazima wa kufanya marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

DK. SHEIN
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema katika kila hatua hadi kupatikana kwa katiba inayopendekezwa, Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu.

“…wananchi kwa ujumla walikuwa wakifuatilia majadiliano bungeni, wakitutia moyo. Ustahamilivu mkubwa wa rais na serikali ya Zanzibar umewezesha kufika hapo.

Tulistahamili, kutumia busara na kuvumilia sana ili tupate katiba,” alisema Dk. Shein.

Alisema jambo linalohusu maendeleo ya Watanzania na hatma yao halitakiwi kufanyiwa mchezo na kwamba, katiba ndiyo uhai wa Taifa.

Dk. Shein alisema katiba inayopendekezwa itajenga mustakabali mzuri wa maendeleo ya Watanzania na taifa na pia inajenga matumaini kwao.

Alisema zipo ibara, ambazo zitaondoa kero za Muungano na kwamba, la kufurahisha ni kuandika katiba kwa kuhakisha Muungano unashamiri, ambao ni kinga kwa Bara na Zanzibar.

Dk. Shein alisema katiba hiyo ni msingi wa dhati wa kuendeleza Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliwataka wananchi kutobabaishwa na wale wasiokubali malengo na misingi ya Muungano na hawaridhiki na jitihada za viongozi.

MWENYEKITI BMK:
Mwenyekiti wa BMK alisema Bunge hilo limetumia siku 125 kati ya 130 zilizotengwa na kwamba kati yake, 67 ni za Februari hadi Aprili na 58 za Agosti hadi Oktoba, mwaka huu.

Alisema katiba inayopendekezwa imeambatana na taarifa za kamati moja hadi 12, taarifa ya kamati ya uandishi, bango kitita kuhusu kamati zote na taarifa fupi ya kuwasilisha katiba inayopendekezwa.

MWENYEKITI KAMATI YA UANDISHI:
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema asilimia 81.8 ya ibara za katiba inayopendekezwa zime tokana na rasimu ya katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema ibara 42 hazikufanyiwa marekebisho, 200 zilifanyiwa marekebisho ya kiuandishi na maudhui, 29 ambayo ni sawa na asilimia 10.7 zimefutwa na 54 ambayo ni sawa na asilimia 18.2 za katiba inayopendekezwa ni mpya kutokana na mapendekezo ya wajumbe wa BMK.

ATETEA MUUNDO WA MUUNGANO:
Chenge alisema muundo wa Muungano umedumu kwa zaidi ya miaka 50 na amani, mshikamano wa kitaifa umekuwapo na kwamba, katiba inatoa uhuru kwa Zanzibar kuanzisha uhusiano na taasisi, au jumuiya za nje, kuomba na kupata ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ili kufanikisha ushirikiano huo, ikiwa ni pamoja na kukopa.

HAKI NA WAJIBU WA MAKUNDI MBALIMBALI:
Alisema katiba inayopendekezwa pia inatambua haki za wenye ulemavu, haki za vijana pamoja na kuundwa kwa baraza la vijana, haki za wanawake, uzazi salama na miliki, kusimamia na kutumia ardhi kwa masharti yaleyale kama ilivyo kwa mwanaume, haki ya mtoto, ambaye anatambuliwa ni mtu wenye umri chini ya miaka 18, mtoto na haki za wazee.

Haki nyingine ni za wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji madini na makundi madogo, kutumia kuendeleza na kuhifadhi ardhi, kupata taarifa na maarifa kwa lengo la kuboresha shughuli zao.

Alizitaja sura mpya zilizoongezwa kuwa ni ardhi raia wa Tanzania pekee ndiye mwenye haki ya kumiliki ardhi, mgeni kuendeleza na kutumia, maliasili na mazingira.

HAKI ZA HUDUMA ZA AFYA NA MAJISAFI NA SALAMA:
Alisema katiba hiyo imenyambua haki ya wananchi kupata huduma bora ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.

Mengine ni uhuru wa kushirikiana katika mambo yanayoendeleza sanaa, ubunifu, utafiti na ugunduzi katika sanaa na sayansi na teknolojia na kwamba, italinda haki miliki.

MWAKILISHI WA WANAWAKE:
Jesca Msambatavangu alisema wanawake wa Tanzania wameendelea kuteseka katika mila potofu, lakini wamepambana na kuendelea kulea familia na kwamba, hadi sasa wamefikia asilimia 50 kwa 50.

MWAKILISHI WA ZANZIBAR:
Hamad Rashid Mohammed alisema Zanzibar kuvaa koti la Muungano limeshugulikiwa ipasavyo na mfumo wa serikali mbili katika ibara ya saba sura ya 75.

Alisema pia muundo wa Muungano na misaada kutoka nje vimeshughulikiwa na kwamba, Zanzibar sasa wana haki ya kujiunga na taasisi yoyote ya kimataifa baada ya kuwasiliana na Jamuhuri ya Muungano na kukopa bila idhini ya serikali ya Jamhuri na iwapo kutakuwa na masharti ndiyo lazima.

Hamad alisema masuala ya gesi na mafuta yatasimamiwa na serikali ya Zanzibar bila kuingiliwa na serikali ya Muungano na kwamba, hakuna mahali katiba inaweza kupatikana nje ya Bunge.

DK. FRANCIS MICHAEL:
Alisema katiba imezungumzia masuala ya ardhi kwa upana na kwa undani, haki ya elimu na elimu bora ili kila Mtanzania apate elimu ya kushindana kwenye ushindani wa ajira na kujiajiri.

Dk. Francis alisema jambo jipya kwenye katiba hiyo ni uhuru wa taaluma, kufundisha, kufanya tafiti na gunduzi zao zipate haki na haki kumiliki ya mali isiyoshikika kama ubunifu.

Alisema tume ya ualimu imetambulika kwenye katiba na kutoa nafasi kwa walimu kujadili na kutolea uamuzi masuala mbalimbali yanayowahusu.

MWAKILISHI WA WAKULIMA:
Dk. Nzigula Maselle alisema miaka 50 iliyopita wakulima hawakuwa na haki zao kwenye katiba na kwamba, katiba inayopendekezwa imewakumbatia wakulima kwa kuwawekea ibara mpya inayotaja haki ya wakulima kumiliki ardhi, kupata taarifa sahihi, masoko na sheria zinazogusa kundi hilo.

MWAKILISHI WA WAFUGAJI:
Doreen Maro alisema haki za wafugaji zimetambuliwa, ambazo ni haki ya kumiliki, kuiendeleza na kuitumia na kwamba, ibara ya 13 imezungumzia malengo yanayoeleza viwanda mama kwa lengo la kuchakata na kusindika mazao yanayotokana na mifugo.

MWAKILISHI WA WAFANYAKAZI:
Mbaraka Igangula alisema katiba hiyo imeainisha haki mbalimbali za wafanyakazi na waajiri, ikiwamo haki ya kugoma, ambayo imeingizwa kwenye katiba na kwamba, haitaruhusu walioko kwenye sekta nyeti kufanya majadiliano na waajiri.

MWAKILISHI WA WAVUVI:
Issa Ameir Suleiman alisema katiba imezingatia mambo yote yaliyokuwa na changamoto kwa wavuvi, migogoro baina ya wavuvi na wawekezaji, lakini wamepewa umiliki wa maeneo ya fukwe, ambayo yatamilikiwa na wavuvi.

MWAKILISHI WA WAISLAMU:
Sheikh Thabit Jongo alisema katiba hiyo ni ya Watanzania ina mchango ya jamii zote zilizo ndani na nje ya Bunge.

Alisema Mahakama ya Kadhi ilileta msuguano, lakini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alimaliza kwa kusema sheria za kadhi zitatungiwa sheria na Bunge ili zikubalike kwenye jamii na kwamba, kilio cha Waislamu ilikuwa ni hiyo, lakini ibara ya 41 imeleta faraja.

“Tuwe mbele kuitetea na kupiga kura ya ndiyo..tunajua wenzetu watatangulia mtaani, lakini nasi tusibaki nyuma, tutakwenda bega kwa bega kuhakikisha inapigiwa kura ya ndiyo,” alisema Sheikh Thabit.

MWAKILISHI WA WAKRISTO:
Askofu Amos Muhagachi alisema katiba imetambua uchaguzi wa imani ya dini, imani au kutokuwa na imani, kutangaza dini, kufanya ibada itakuwa huru na jambo la hiari almradi muumini hakiuki sheria na ili hayo yatekelezwe, lazima kuwa na amani na utulivu.

Aliwaomba waumini wa dini zote kuisoma katiba na kuielewa na Watanzania kuipokea kwa kuwa imezingatia maslahi yao kwa kuwa imewapa uhuru wa kuabudu kwa amani na utulivu.

MWAKILISHI WA SEKTA BINAFSI:
Godfrey Simbeye alisema wawekezaji wanapenda kuona nchi yenye amani na utulivu, katika malengo makuu, uwezeshaji na fursa za uwekezaji wa ndani na nje, umuhimu wa wawekezaji wa nje kushirikiana na wa ndani, umuhimu wa kupingana na rushwa kwa Takukuru kutajwa kwenye Katiba.

Alisema suala la manunuzi ya umma likitumika vizuri linaweza kuleta mabadiliko katika nchi.

MWAKILISHI WA WALEMAVU:
Amon Mpanju alisema katiba ya mwaka 1977 imetaja walemavu mara moja katika hali ya kupewa msaada, lakini inayopendekezwa imetaja katika ibara zaidi ya nane, lugha ya alama na alama mguso, njia mbadala kwa watu wenye ulemavu katika sehemu za umma na vyombo vya habari vinavyotangaza kitaifa.

Sherehe hizo zilipambwa na shamrashamra mbalimbali, ikiwamo viongozi wa dini kutoa sala.

Viongozi mbalimbali, akiwamo Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, mabalozi, wakuu wa mikoa, wilaya, wadau na wananchi.

MCHAKATO ULIKOANZIA:
Mchakato wa katiba mpya ulianza baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitaka kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Rais aliteua wajumbe wa tume hiyo Aprili 6, mwaka 2012, waliapishwa Aprili 13 na kuanza kazi Mei 2, mwaka huo huo, ikiwa na wajumbe 34 na hadi rasimu ya pili inakabidhiwa, walikuwa 32 baada ya Mjumbe Dk. Sengondo Mvungu, kufariki na John Nkolo, kupata matatizo ya kiafya.

Tume hiyo chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, ilikusanya maoni ya wananchi, kuyachambua na kuandaa rasimu ya kwanza iliyojadiliwa na mabaraza ya katiba.

Bunge lilianza Februari 18 na kukamilisha awamu ya kwanza Aprili 25 kwa kupisha Bunge la Bajeti na baadaye liliendelea Agosti 5, mwaka huu hadi katiba inayopendekezwa ilivyopitishwa.

Wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitoka ndani ya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, baada ya kudai kuna uchakachuaji wa rasimu ya tume kwa kuingiza mambo mapya.

Bunge hilo liliundwa na wajumbe 629, wakiwamo kutoka kundi la 201 walioteuliwa na rais, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Baada ya katiba inayopendekezwa kukabidhiwa kwa Rais Kikwete na Rais Shein, hatua itakayofuata ni wananchi kupiga kura ya maoni ya ama kuikubali au kuikataa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni