Papa Wemba
Na Daniel Mbega, www.brotherdanny.blogsport.com
Alikuwepo pia swahiba wa Franco, huyu si mwingine bali ni Joseph Mobutu Sese Seko Kuku Ndegbu Wa Zabanga.
Lakini ikiwa ulidhani ni hao watatu tu na kwamba hakuna mwenye jina refu tena, basi uko nje ya ukweli. Yupo, tena anaishi. Huyu si mwingine bali ni mwanamuziki nguli wa Congo ambaye wengi wanamfahamu sana kwa jina la Papa Wemba.
Jinale halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba aliyezaliwa mwaka 1949 huko Lubefu katika Mkoa wa Sankuru nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini wakati huo ikijulikana kama Congo-Leopoldville, baadaye Zaire.
Mwanamuziki huyu, ambaye wanamuziki vijana wanamwita 'Mzee Fula Ngenge' mkali wa lese rhumba (ambayo sasa inajulikana kama soukous) pamoja na Afro-pop, anatokea katika kabila la Watetela, mojawapo ya makabila takriban 250 ya nchini Congo.
Kwa faida yako tu ni kwamba, Watetela wanaishi katikati ya Mto Congo na Lusambo katika majimbo ya Sankuru na Maniema. Wanategemea zaidi uvuvi na kilimo hasa cha mihogo, migomba na kola. Hawa wanashabihiana na Wakusu na walitengana katika miaka ya 1800 kufuatia ujio wa Waraabu na Wabelgiji. Lakini Watetela na Wakusu wanatokana na Kabila la Wamongo. Hawa Watetela wanafahamika kwamba walikuwa wanatumiwa na Mwarabu Tip Tip kukamata watumwa katika kabila la Walunda. Neno Motetela linatokana na jina la mungu aliyeitwa Motetela, ambaye maana yake ni "yeye asiyecheka" au "yeye ambaye hupaswi kumcheka."
Waziri Mkuu wa kwanza aliyeuawa, Patrice Lumumba, alikuwa Mtetela. Pengine kutokana na kuuawa kwa Lumumba ndiyo maana mwaka 1975 serikali ya Zaire chini ya Mobutu Seseko Kuku Ndegbu Wa Zabanga ikaamua kuwaondoa jeshini Watetela wengi.
Naam. Tuendelee na simulizi yetu. Hapana shaka yoyote Papa Wemba anajulikana kila kona duniani kutokana na muziki wake, ambapo anajua kuwapa vionjo tofauti mashabiki wake. Akiwa Afrika na baadhi ya nchi za Ulaya hupiga soukous, na akienda nchi nyingine hupiga Afro-pop na kuleta ladha inayokubalika na kuchezeka na mashabiki kila kona.
Alianza muziki kwa kuimba kwaya kanisani, lakini historia yake kwa muziki wa kidunia, kama tulivyoona hapo mwanzo, ilianzia rasmi pale Zaiko Langa Langa mchana wa Desemba 24, 1969 bendi hiyo ilipoanzishwa rasmi. Wakati huo alikuwa na miaka 19 tu.
Kama tulivyoona awali, hapo alikutana na wanamuziki wengine wakali kutoka bendi za mitaani kama N’Yoka Longo Mvula ‘Jossart’, Felix Manuaku Waku ‘Pepe Felly’, Evoloko Lay Lay ‘Joker’, Teddy Sukami, Zamuangana Enock, Mavuela Simeoni ‘Somo’, na wengine.
Ndani ya Zaiko kulikuwa na vipaji, lakini Evolocko Jocker na Papa Wemba walikuwa nyota zaidi kutokana na sauti zao na ubunifu. Papa Wemba wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Jules ‘Presley’ Wembadio, wakimfananisha na mwanamuziki nyota wa Marekani, Elvis Presley. Sauti yake iliipaisha mno Zaiko ambayo sasa ilikuwa juu pamoja na kuibuka kwa bendi nyingine ndogo kama Les Grands Maquisards, Le Trio Madjesi, Bella-Bella na Empire Bakuba.
Kutokana na kujiona kwamba ni nyota, Papa Wemba na Evoloko Joker wakaona wananyimwa fursa ndani ya Zaiko, na kwamba walikuwa na uwezo wa kuanzisha bendi yao wenyewe.
Desemba 1974, wakati wa kilele cha umaarufu wao (na hapa ni baada tu baada ya pambano la Rumble in the Jungle kati ya Muhammad Ali na George Foreman jijini Kinshasa), Shungu Wembadio pamoja na Efonge Gina wa Gina, Evoloko Lay Lay, Mavuela Somo na Bozi Boziana aliyejiunga na Zaiko Langa Langa mwaka 1973, wakaamua kuondoka na kuanzisha bendi yao wenyewe waliyoipachika jina la Isifi Lokole (baadaye ikajulikana kama Isifi Melodia).
Isifi ni kifupi tu cha maneno "Institut du Savoir pour la Ideologique Formation des Idoles."
Waimbaji kwenye bendi hiyo walikuwa Evoloko Athsuamo Joker, Papa Wemba, Mavuela Somo na Bozi Boziana, mpiga solo alikuwa Chora Mukoko, mpiga bass Djo Mali, na mpiga drums alikuwa Biko.
Bila shaka, siyo kila kitu ambacho Wemba anadai kuwa ukweli kinaweza kuchukuliwa kama injili.
Unataka kujua alilipataje jina lake la sasa ambalo limekuwa maarufu zaidi duniani? Subiri nikusimulie. Wembadio ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa ambapo alikuwa na wadogo zake kadhaa. Wazazi wao walifariki katika miaka ya 1960, yeye akiwa bado mdogo tu. Jukumu la kuihudumia familia likabaki kuwa lake. Ikumbukwe kwamba hakuwa na kazi yoyote zaidi ya muziki, na hii ni moja ya sababu zilizochangia kuondoka kwake Zaiko kutokana na kutafuta maslahi zaidi ya kuitunza familia.
Sasa mnamo Julai 1975, kutokana na majukumu
ya familia aliyokuwa nayo, Wembadio akapachikwa jina la ‘Papa’ (yaani baba) na
wakalifupisha jina la Wembadio na kuwa ‘Wemba’.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni