Jumamosi, 11 Oktoba 2014

JAMBAZI SUGU LA KUPORA MAGARI WANAWAKE LAUAWA


Wakazi wa Jiji la Arusha wakiwa katika Kituo cha Polisi mkoani humo kushuhudia mwili wa mtu anayedaiwa kuwa jambazi sugu, Ramadhan Abdallah Jumanne (Rama Ndonga), aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi usiku wa kuamkia jana. Picha na Happy Lazaro.

picha ya juu na chini  wananchi wa jiji la Arusha  waliojitokeza kuuangalia mwili wa  jambazi huyo atari aliowawa na polisi usiku wa kuamkia leo.
 wananchi wakiendelea kushuhudia mwili wa jambazi hilo nje ya jengo la makao makuu ya polisi mkoani Arusha.


 baadhi ya vitu vilivyokutwa kwa jambazi hilo zikiwemo silaha mbalimbali
 kamanda wa polisi akionyesha moja ya kifaa cha kufanyia tageti kabla ya kupiga kijulikanacho kwa jina la Glock Fab Defence moja ambacho jambazi hilo lilikuwa likitumia.

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kumuua jambazi aliyekuwa akiutikisa mkoa huo kwa matukio ya kuteka na kuwapora wanawake wenye magari na kisha kuwapiga risasi.
Mtu huyo aliyefahamika kwa kwa jina la Ramadhan Abdallah Jumanne maarufu kama Rama Ndonga (37) Mkazi wa Moivo hatimaye ameuawa polisi baada ya kupigwa risasi katika majibizano na askari wa jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jambazi huyo aliuawa usiku wa kuamkia jana majira ya saa 2:04 usiku katika Kijiji cha Moivo, Kitongoji cha Enaboishu wilayani Arumeru.
Alisema baadhi ya matukio ya ujambazi aliyowahi kuhusika nayo ni lililotokea Agosti 6 mwaka huu saa 3:30 usiku maeneo ya Kwa Iddi ambapo walimpiga risasi sehemu ya shingo mwanamke Shamimu Rashid aliyekuwa Mkazi wa Sakini wakati akijiandaa kuingia nyumbani kwake na kumuua.
Kamanda Sabas alitaja tukio lingine ni la Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 1:00 huko maeneo ya Olasiti, jambazi huyo akiwa na mwenzake kwenye pikipiki walimjeruhi kwa kumpiga risasi ya mdomoni na kutokea kichwani mtoto Christen Nickson mwenye umri wa miaka mitatu na nusu na kisha kufanikiwa kupora Sh200,000 na baadaye majeruhi huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru.
Aidha, kukamatwa kwa jambazi huyo ni baada ya polisi kutumia mbinu za kisasa na kufika nyumbani kwa marehemu na polisi walimwamuru ajisalimishe lakini alikaidi na kuanza kuwarushia risasi hali iliyosababisha askari kujibu mapigo na hatimaye kusababisha kifo chake.
Alisema kuwa, baada ya upekuzi mwili wa marehemu ulipatikana na bastola aina ya Glock 19 yenye namba RLU 976 iliyotengenezwa nchini Australia ikiwa na magazine yenye risasi 14 ambayo alikuwa ameishika mkononi pamoja na maganda matano ya risasi.
Aidha, upekuzi zaidi uliofanywa katika chumba chake ulibaini magazine moja yenye risasi 15 na magazine mbili zenye uwezo wa kubeba risasi 30 kila moja, redio call moja yenye nembo ya ITSS/UNICTR, pikipiki aina ya Toyo Power King rangi nyekundu yenye namba za usajili T 507 BSU.
Upekuzi zaidi ulibaini kofia ngumu ya kuendesha pikipiki rangi nyekundu, plate number ya pikipiki yenye namba T 805 CVD, pingu moja, Glock Fab Defence moja na vifaa vya kusafishia bastola pamoja na koti jeusi.
Kamanda Sabas alisema polisi wanaendelea kumsaka mwenzake waliyekuwa wakitumia naye pikipiki hiyo, ili kuweza kuutokomeza mtandao huo ambao umekuwa tishio jijini Arusha.
Kutokana na tukio hilo, watu walifurika kituo cha polisi kushuhudia mwili wa marehemu ambaye aliutikisa mji huo.
CREDIT: MWANANCHI


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni