Hashim Lundenga
Prashant Patel: Mwanzilishi wa Miss Tanzania
Na Mwandishi Wetu
MWANZILISHI wa mashindano ya urembo ya Miss
Tanzania, Prashant Patel, amefungua maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam akiomba mshirika wake, Hashim Ludenga, azuiliwe kuendelea
kuendesha mashindano hayo yanayotarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 11, mwaka
huu.
Patel amewasilisha maombi hayo katika hati ya dharura kupitia wakili wake,
Benjamin Mwakagamba, akidai Lundenga ana mpango wa kuendesha mashindano hayo
kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata
kumtaarifu.
Anaomba mahakama itoe zuio dhidi ya Lundenga, la kuendesha mashindano hayo hadi
shauri lake la msingi aliloliwasilisha litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika kesi yake ya msingi, Patel anadai pamoja na mambo mengine, utekelezaji
wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na malipo ya Sh milioni 19 ambayo
hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba na faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi
Septemba 23, mwaka huu.
Shauli hilo limepangwa kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Frank Moshi
leo, na Lundenga ametakiwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya siku 21, na
akishindwa kufanya hivyo, mahakama itaendelea kutoa hukumu dhidi yake.
Katika hati ya kiapo inayounga mkono maombi yake, Patel anadai kuwa yeye pamoja
na Lundenga ndio waanzilishi, waongozaji na waendeshaji wa mashindano ya Miss
Tanzania na wamekuwa katika hali hiyo kwa miaka 20 sasa, tangu mashindano hayo
yaliyoporuhusiwa tena mwaka 1994.
Kwa kipindi chote hicho, wamekuwa wakisaini makubaliano ya namna ya kuendesha
mashindano hayo na mara ya mwisho walisaini makubaliano Februari 20, 2012.
Hata hivyo, Lundenga alikataa kusaini makubaliano kwa mwaka 2013 na 2014 na
ameshindwa kumlipa fedha zake Sh milioni 19.
Patel anadai badala yake Ludenga ameshirikiana na wadhamini wengine kuendesha
mashindano hayo.
Kwa mujibu wa makubaliano, Lundenga pia alipaswa kulipa pauni za Uingereza
30,000 kama malipo ya kibali kwa mwendeshaji wa shindano hilo duniani, Miss
World, deni ambalo limekuwa la muda mrefu, hivyo kuchafua hadhi yake.
Patel anadai kuwa Ludenga alipelekewa taarifa na wakili wake kulimaliza suala
hili bila kushirikisha hatua za kisheria, lakini alikaidi na kukataa. Hivyo
Patel anadai kuwa hakuwa na njia nyingine zaidi ya kulipeleka suala hilo
mahakamani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni