Alhamisi, 4 Septemba 2014

Mwenyekiti Wanging’ombe aburutwa Mahakamani kwa kutishia kuua


Yono Stanley Kevela


Na Michael Katona, Njombe
  
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wanging’ombe Anthony Mahwata leo amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu wa wilaya ya Njombe kwa kosa la kumtishia kumua mbunge wa zamani wa Njombe Magharibi, Yono Kevela.

Akisomewa mashtaka na wakili wa serikali, Atu Mwakasitu mbele ya hakimu Mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Njombe, Samwel Obas, Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wanging’ombe, Mahwata ilidaiwa kuwa mnamo Februari 5, 2013 akiwa katika uwanja wa mpira wa miguu wa kijiji cha Igwachanya wilayani Wanging’ombe alimtishia kwa maneno kutaka kumua Yono Stanely Kevela na pia kusababisha uvunjifu wa amani kabla ya mchezo wa soka uliozikutanisha timu ya Yanga Veteran ya Dar es Salaam dhidi ya Timu ya kijiji cha Igwachanya Wilayani Wanging’ombe.

Wakili Mwakasitu aliiambia mahakama kuwa, mtuhumiwa Mahwata (49) na mwenzake Evarist Makurumbi (32) kwa pamoja wakiwa katika uwanja wa shule ya sekondari ya Igwachanya na baadaye kuhamia kwenye uwanja wa mpira wa miguu wa kijiji cha Igwachanya, walihatarisha uvunjifu wa amani kwenye uwanja huo baada ya kudaiwa kuweka magari yao mawili kwenye magoli ya mpira wa uwanja huo wakizuia mchezo usifanyike.

Akitoa ushahidi dhidi ya mashtaka aliyofungua ya kutishiwa kuuawa na Mwenyekiti Mahwata, mbunge wa zamani wa Njombe Magharibi, Kevela aliiambia mahakama hiyo kuwa, mnamo Febriari 5, 2013 akiwa ni mwenyekiti wa chama cha soka wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe aliialika timu ya Yanga Veteran kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya kijiji cha Igwachanya katika uwanja wa shule ya sekondari Igwachanya.

Kevela alisema kuwa wakati timu hizo zikiwa kwenye uwanja wa soka wa shule ya sekondari Igwachanya zikijiandaa kuingia uwanjani, Mahwata ambaye pia ni diwani wa Kata ya Igwachanya alizuia kuchezwa mchezo huo sambamba na kukodi kundi la vijana ili kufanya fujo kwenye uwanja wa mpira kuzuia mchezo usichezwe.

Aliieleza pia mahakama kuwa kufuatia hali hiyo ya kuzuiwa kufanyika, Kevela na wenzake waliamua kuelekea kwenye uwanja wa soka wa kijiji ambao uliruhusiwa na mtendaji wa Kijiji cha Igwachanya, Belisheza Mhanga kufanyika.

Kevela alisema Mahwata na Makuumbi walitangulia kwenye uwanja wa kijiji wakiwa na magari aina ya RAV 4 namba T 749 AYU na gari aina ya NOAH namba T973 BGG na kwenda kuyaweka katikati ya magoli ya mpira kwenye uwanja huo kuzuia mchezo huo usichezwe.

Kevela aliieleza mahakama kwamba Mahwata alizui mchezo usichezwe kwa sababu mtuhumiwa alidhani kuwa muktadha wa mchezo huo ni kumchafua kisiasa kaka wa mshtakiwa ambaye alimshinda katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo kwenye kura za maoni ndani ya chama cha mapinduzi (CCM).

Kevela aliongeza kuwa wakati timu hizo za mpira wa soka zikiwa katikati ya uwanjani, Mahwata aliamuru timu ya Igwachanya ivue jezi za kuchezea pamoja na viatu kwa sababu jezi hizo zimetolewa na mbunge wa sasa wa Njombe Magharibi Gerson Lwenge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Miundombinu.

“Mbona unanifatilia sana, nimezuia msitumie uwanja wa shule ya sekondari Igwachanya, mmehamia kwenye uwanja huu wa kijiji ambapo bado pia ni eneo langu, nitakufanya kama nilivyomfanya kaka yako au umesahau alichofanyiwa.”Alisema Kevela

Kevela ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Jimbo la Njombe magharibi (CCM) mwaka 2005-2010 alidai kuwa kaka yake aliuwawa kwa kukatwa mapango sambamba kutolewa sehemu za siri na kutenganishwa kichwa na kiwiliwili.

Kesi hiyo itaendelea tena Septemba 9, mwaka huu kufuatia kutolewa samansi ya kuitwa mashahidi upande wa utetezi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni