Sitti Mtemvu akipunga mkono
Miss Tanzania Sitti Mtemvu mara baada ya kushinda taji hilo akiwa na mshindi wa pili na watatu
Maureen Godfrey
Na Michael Katona, Njombe
MSICHANA Maureen Godfrey, ambaye ni
mrembo wa Nyanda za Juu Kusini, akitokea Mkoa wa Njombe, amefunguka na kudai
kuwa ni vigumu kwa warembo kutoka kanda hiyo kuweza kufika hatua ya fainali
kwenye shindano la Mrembo wa Tanzania.
Akizungumza baada ya kushindwa
kufanya vyema kwenye mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, yaliyofanyika Oktoba
11, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Maureen alisema wakati akiwa anashiriki
shindano la 'Miss Nyanda za Juu' mkoani Iringa, aliambiwa na mmoja wa majaji,
ambaye anatoka ndani ya Kamati ya Miss Tanzania, kwamba ni ndoto kwa warembo
kutoka mikoa ya kusini kuweza kushinda taji hilo.
“Hakuna warembo wazuri na wenye
sifa kutoka kanda hiyo, hivyo si rahisi kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini
kuweza kutoa mrembo atakayeweza kutwaa taji hilo,” alisema Maureen akimnukuu
jaji huyo (jina tunalo).
Mrembo huyo alisema kwa jinsi
ambavyo ameona mashindano ya mwaka huu yalivyoendeshwa na Sitti Mtemvu kuvishwa
taji la Miss Tanzania, haoni sababu kwa warembo wengine watakaotaka kushiriki
mashindano hayo kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuungana na warembo
wengine katika kambi ya Miss Tanzania mwakani.
“Kwa warembo wengine ambao watataka
kuja kushiriki kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini, siwashauri washiriki
mashindano haya. Niliwahi kumuuliza jaji mmoja ni kwa nini Nyanda za Juu Kusini
mtu akijitihadi sana, anaishia 15 bora? Alinijibu kwa sababu huko kwenu hamna
warembo wazuri, na alidai eti wasichana wazuri wako Mwanza, Dar es Salaam na Arusha,”
alisema Maureen.
Maureen, ambaye
hakuingia hatua ya 15 bora kwenye mashindano ya mwaka huu, yaliyowashirikisha
warembo 30 kutoka nchi nzima, alisema warembo wenzake wanaotoka mikoani
wamekuwa hawapewi nafasi kama warembo wengine wanaotoka kwenye mikoa ya Dar es
Salaam, Arusha na Mwanza.
“Nilipotangazwa kuwa mshindi wa
urembo wa mkoa wa Njombe na Nyanda za Juu Kusini, wapo baadhi waliniona ni
mshamba na nisiyekuwa na sifa za kuuwakilisha mkoa kama mrembo, wengine walidai
sisi warembo tunaotokea huku Nyanda za Juu Kusini eti tunatokea porini, hatujui
lolote,” alisema Maureen.
Mrembo huyo alida wakati akiwa
kwenye kambi ya Miss Tanzania, vipaumbele walikuwa wakipewa zaidi warembo
kutoka Kanda ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
“Mambo
mengi nilikuwa naona, wanapewa vipaumbele warembo wanaotoka Arusha, Mwanza,
Shinyanga na Dar es Salaam, tena kwa kila kitu, hasa katika suala la mahojiano
kwa kila mshiriki, tuliambiwa tutafanyiwa (interview) mara tatu ili tuonekane
kwenye luninga, lakini nilimuuliza muongozaji filamu, inakuwaje mtu mmoja
anakuwa ni yeye tu anayerekodiwa huku wengine hatupigwi picha za video?
“Muongozaji wa
picha alikuwa anamchukua mtu mmoja pekee yake kwa kuanzia mguuni mpaka
kichwani, lakini wengine tulikuwa hatupewi nafasi hiyo. Nilimuuliza mbona
wengine hatuchukuliwi kama huyo, akasema wengine siyo lazima kuchukuliwa.
Kama
mnasema picha si lazima, basi mngekuwa mnachukua warembo kumi tu ndiyo
wanaotakiwa waonekane, kuliko kufanya ubaguzi wa picha na mahojiano kwa warembo
wengine, ili hali wakiwa na matumaini ya kufanyiwa interview, lakini imekuwa ni
tofauti,” alilalamika mrembo huyo.
Mwakilishi huyo kutoka mkoani
Njombe pia aliyakosoa mashindano hayo kwa waandaji kuwanyima warembo wengine
nafasi ya kujitambulisha jukwaani, kama ambavyo miaka mingine imekuwa
ikifanyika,badala yake ilitumika njia ya kurekodiwa na kurushwa katika luninga
kwa kila mshiriki kuonyeshwa anakotoka na vitu ambavyo anapendelea kufanya
katika jamii.
“Tulipokuwa
tunatoka Moshi kwenda KIA (uwanja wa ndege wa Kilimanjaro), nilihoji ni kwa
vipi hatufanyiwi mahojiano sisi baadhi ya warembo huku wengine tayari
wamefanyiwa zaidi ya mara tatu. Lakini picha ambayo nilipigwa mimi ni ile ya
kujitambulisha unauwakilisha mkoa gani,” alisema mrembo huyo.
Alipoulizwa kama anakubaliana na
uamuzi wa majaji kumtangaza Sitti, alisema hakustahili kabisa kuwa mshindi na
tayari kulikuwa na dalili za upendeleo za kumtangaza mshindi huyo.
“Huyu dada hakustahili kuwa mshindi
wa taji hili la Miss Tanzania, labda pengine alistahili kuwa mshindi wa kawaida
kati ya warembo watano bora, mimi napinga yeye kuwa mshindi, kwa sababu tangu
awali dalili za upendelo zilishafanyika na alikuwa amepangwa,” alisema Maureen.
"Jambo la kushangaza ni kwa
vipi kila mara, mrembo huyo apite katika kila hatua na hata zaidi muda mwingi
kamera zilikuwa zikimuonyesha yeye, hii si sawa, matokeo yalipotoka wapo watu
waliangua kilio na wengine walipoteza fahamu kwa mshituko mkubwa, ambao
hawakuutarajia,” alisema.
Aliwashauri waandaaji a Miss
Tanzania, chini ya Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga,
kuepuka lawama hivi sasa ni bora mashindano hayo yakawa yanafanyika katika miji
mingine kuliko miaka yote kufanyika Dar es Salaam pekee.
“Rai yangu ni kwa waandaaji hawa
wadogo kwamba wasikatishwe tamaa na haya yaliyotendeka katika shindano hili,
lakini pia haki haikutendeka kwa washiriki wengine waliokwenda kushindana. Kama
Nyanda za Juu Kusini imeonekana hawana warembo wazuri, nashauri mashindano ya
urembo yatakayofanyika kwenye kanda hiyo, yaishie hapo hapo na si kupelekwa
kwenye shindano la Miss Tanzania,” alisema Maureen.
"Ni vyema mshindi
atakayeshindanishwa kutoka kwenye kanda, apewe zawadi sawa na zile zinazotolewa
kwa Miss Tanzania. Hakuna maana ya sisi warembo tunaotoka mikoani,
kushirikishwa kwenye fainali hizo. Tumekuwa tunaonekana sisi ni washamba na
hatuna sifa zinazostahili,” alilalamika.
Tayari ushindi wa Sitti umeshaanza
kulalamikiwa na wadau wa mashindano hayo, ambapo inadaiwa kuwa, ameghushi umri
wake.
Sitti katika fomu za kujiandikisha
kuingia katika mashindano hayo, alijaza ana umri wa miaka 18,
wakati
umri wake halisi unadaiwa kuwa ni miaka 25. Sifa za mshiriki wa Miss Tanzania
anatakiwa awe na umri wa miaka 18 hadi 23, awe raia wa Tanzania, awe hajaolewa,
awe na ufahamu wa kutosha kujieleza, awe hajazaa na asiwe mwanafunzi wa shule
ya msingi au sekondari.
Kwa upande wake, Maria Itala,
ambaye ni mama mzazi wa Maureen, ambaye alikwenda kushuhudia fainali hizo
jijini Dar es Salaam, akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake, alionya kwamba
endapo waandaaji hawatakuwa makini, mashindano hayo yatapoteza sifa zake na
jamii kuyachukulia kuwa ya kihuni.
“Kufanya mashindano ya kikanda
zaidi bila kwenda Taifa, kutasaidia sana washiriki hususan wazazi wanaowakilishwa
na watoto wao kwenye fainali hizo, wasipate hasara kubwa kama ambavyo mimi
mzazi wa Maureen nilivyopata,” alisema Itala.
Aliishauri Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, kuangalia uwezekano wa kuyasimamia ili kuepuka
utata, ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara, ikiwemo harufu ya rushwa na
upendeleo.
“Mashindano haya ni ya kitaifa,
ambapo baadaye mwakilishi anapeperusha bendera ya Tanzania kwenye taji la
dunia, ni vyema yakadhaminiwa na serikali yenyewe. Rushwa hivi sasa ni kubwa
sana kwenye mashindano haya, ni vyema serikali ikachukua jukumu la kudhamini
Miss Tanzania, kama ambavyo wanavyofanya nchi za Nigeria, Ghana na nyinginezo,
ndiyo maana wenzetu wanapata wawakilishi wanaofanya vizuri kwenye shindano la
dunia,” alisema.
“Endapo serikali itayachukua,
kwanza itaingiza pato kubwa na vilevile itakuwa inagharamia kila kitu, lakini
si kama hivi sasa, wenzetu wanatushangaa, iweje mpaka kwenye mashindano makubwa
kama hayo, mzazi aendelee kutoa gharama kubwa za kuchangia maandalizi ya mshiriki?
Hapana, hili siyo sahihi, mtoto anapata manyanyaso na kubaguliwa, kweli mzazi
unaweza kuugua,” alisema Itala.
Alidai tangu
mtoto wake ashiriki kwenye kambi hiyo ya Miss Tanzania, jambo kubwa ambalo
amejifunza ni kuona baadhi ya wazazi wenzake wanashindwa uwezo wa kifedha
kwenye maandalizi hayo, na hasa kwa baadhi ya warembo wanaotoka katika mikoa
hiyo mipya kwa sababu hawafahamiki na hivyo warembo wanaopewa nafasi kubwa ni
wale wanaotoka katika kanda fulani.
“Ni vigumu kwa mrembo anayetoka
katika hii mikoa mipya kuweza kushinda. Kwanza hajulikani, mashindano ya sasa
yanaonekana kuegemea zaidi kwenye kanda fulani, sikubaliani na waandaaji
kujikita zaidi kutangaza vivutio vya kanda ya kaskazini, kwani hata nyanda za
juu kusini inapaswa kupewa nafasi ya kutangazwa zaidi, pia zipo fursa,”
alisema.
Itala pia alitoa
tahadhari kwa waandaaji kuachana na kasumba ya upendeleo inayoanza kuonekana
hivi sasa kwa mashabiki kutengeneza vipeperushi vya ushabiki kwa mrembo ambaye
wanaona atashinda.
“Mtizamo wangu kwa
sasa, mashindano haya yameanza kuingizwa na siasa, watu wanakuja na mabango,
wengi tumeona wamekuja na vipeperushi vinavyoonyesha tayari mrembo fulani
atakuwa mshindi, na hatimaye akawa mshindi, hiyo tayari ni siasa, hatufanyi
mashindano ya urembo yakaingizwa siasa,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni