IGP Ernest Mangu
NA MWANDISHI
WETU, NZEGA
WIMBI la mauaji ya kutisha
limeendelea kutikisa nchini, baada ya watu wasiojulikana kuwaua mama na watoto
wake wawili kwa kuwakatakata kwa mapanga usiku wa kuamkia juzi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea
katika Kijiji cha Nata wilayani Nzega mkoani Tabora.
Akizungumza na MTANZANIA jana,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, aliwataja waliouawa kuwa ni
mama Leticia Thomas, Marietha Nicolaus ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili
katika Shule ya Msingi Mwanaruru na Magreth Nicholas ambaye umri wake
haukutambulika.
“Mama wa watoto hao aliuawa kwa
kukatwakatwa kwa mapanga sehemu za kichwani na bega la kushoto, hali
iliyosababisha apoteze maisha hapo hapo kutokana na majeraha mengi.
“Lakini pia watoto Marietha na
Magreth nao walikatwakatwa hivyo hivyo… mauaji haya ni mabaya, tunaendelea na
msako mkali wa kuhakikisha wahusika wanatiwa nguvuni,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema mpaka sasa chanzo cha mauaji
hayo ya kinyama hakijajulikana, ingawa kuna taarifa kuwa inawezekana
yamesababishwa na masuala ya mapenzi.
“Polisi tunaendelea na uchunguzi wetu
wa kina, hatujapata chanzo cha mauaji haya, tunaomba mtupatie muda wakati huu
ambao askari wangu wanaendelea na kazi,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema mpaka jana hakuna mtu hata
mmoja aliyetiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.
“Kwa vile polisi tunafanya kazi zetu
kisayansi, naamini tutafanikiwa ingawa mpaka sasa hakuna mtu aliyetiwa
mbaroni,” alisema Kamanda.
Alisema taarifa za kugundulika kwa
miili hiyo zilitolewa na majirani ambao walilazimika kwenda kumwangalia mama
Magreth baada ya kuona amechelewa kuamka.
“Inaonekana baada ya tukio lile
kulipopambazuka asubuhi, mama Magreth alikuwa hajafungua mlango majirani
wakaamua kwenda kugonga mlango walipoona kimya wakaamua kuvunja mlango na
kukuta familia yote imeuawa,” alisema Kamanda.
Matukio ya watu kuchinjwa yamekuwa
yakitokea kila mara ambapo Septemba 16 mwaka huu, mfanyabiashara aliyefahamika
kwa jina la Melasi Ndabi aliyeuawa kwa kuchinjwa na watu wanaodaiwa kufika
nyumbani kwake katika Kijiji cha Lisu wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora.
CREDIT: MTANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni