Hivi ndivyo ilivyokuwa shwari Makambako, hata Polisi huyu wa kike hakuweza kutumia nguvu nyingi kudhibiti vurugu kwenye mkutano wa Chadema
Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, John Mnyika akiwa na viongozi wengine wa Chadema alipokuwa kwenye mkutano mjini Makambako
John Mnyika akionyesha rasimu ya Jaji Warioba iliyopendekezwa na wananchi
Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu akizungumza kwenye mkutano mjini Makambako
Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Patrick Ole Sosopi akitambulishwa
Askari wa kike wa Jeshi la Polisi mjini Makambako akisimamia ulinzi kwenye mkutano
Na Mwandishi Wetu, Makambako
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) Tanzania Bara, John Mnyika, amesema hivi sasa
watakutana na wananchi mtaani kwa ajili ya kujadili rasimu mbili zilizopendekezwa
na Bunge Maalum la Katiba pamoja na ile Katiba ya Jaji Warioba iliyopendekezwa
na wananchi.
“Sisi tunasema tukiwa mtaani
tutajadili katiba zote mbili, rasimu ya katiba ya wananchi na ile rasimu ya
katiba ile katiba haramu, katiba ya mafisadi, sisi wengine tunaunga mkono
rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba inayoungwa mkono na
wananchi,” alisema Mnyika.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara
katika Halmashauri ya Mji Makambako, kwenye uwanja wa Jeshi la Polisi mjini
hapa Mnyika alisema kuanzia sasa Chadema itakwenda jimbo kwa jimbo eneo kwa
eneo kujadili katiba zote mbili. Na kuongeza kuwa Chadema wanataka katiba
iliyopendekezwa na wananchi iwe ndiyo katiba ya nchi na kuboreshwa kidogo.
“Warioba alisema hivi na nina
kubaliana nao, kwamba wao wanajiita wako wengi kule ndani ya bunge, tutakutana
nao mtaani, sasa ndiyo tumekutana nao mtaani, sawa sawa wananchi?” Mnyika
aliwauliza wananchi na wanachama wa Chadema waliokuwa wakimsikiliza huku
wakimshangilia.
Akihutubia mkutano huo ambao ukiwa
na ulinzi wa kutosha kutoka jeshi la polisi, Mnyika alisema kutokana na Bunge
la Katiba kuamua kupitisha rasimu ya katiba kwa ajili ya kuipeleka mtaani ili
wananchi waijadili, Chadema kuanzia sasa itapita mtaani nchi nzima kuwaeleza
wananchi kuipinga katiba hiyo iliyopitishwa na Bunge Maalum.
“Kwa sheria mbovu ya mabadiliko ya
katiba, kwa dhamira mbovu iliyokuwa mwanzo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo
haikuwa na dhamira ya kuandika katiba mimi naona ni jambo zuri ni jambo la
kheri pamoja na gharama zake kwetu wananchi, kwamba tumefikia hapa kuwa na
rasimu mbili,” alisema Mnyika.
“Tuna rasimu wanayoiita rasimu
iliyopendekezwa, Katiba haramu, tunayo katiba haramu ya Sitta (Samweli), Chenge
(Andrew Chenge) na wenzake, harafu
tunayo rasimu ya katiba ya wananchi, ni jambo zuri kwamba sisi Watanzania tunao
uwezo wa kuchagua katiba,” alisema Mnyika.
Alisema uamuzi uliofanywa na bunge
la Katiba chini ya Mwenyekiti wake Samweli Sitta wa kuipigia kura katiba na
kisha kuipitisha kumefanya Tanzania kuingizwa kwenye maajabu ya kupiga kura
duniani.
“Tuliwaambia tunahitaji mrekebishe
muundo wa bunge lenyewe linaloiandika katiba, kwa sababu sasa hivi bunge
limetengenezwa kutafuta kura za CCM, mamlaka makubwa ya Rais yalikuwa ni kuteua
wajumbe, nilibishana nao wakaongeza wajumbe 166 mpaka 201 lakini kuna kitu
hawakukifanya tulibishana nao sana,” alisema Mnyika.
Aliongeza, “Najua watu wa usalama
wanarekodi, Rais Jakaya Kikwete akaonyesha udhaifu mkubwa, akatumia madaraka
vibaya katiba lile kundi la 201 akateua makada wa CCM wengi, lengo kuu ni
kutafuta theluthi mbili, na theluthi mbili hiyo haikuanza kutafutwa kwa
kuchakachua hizi kanuni, kuingiza kifungu ambacho kina iingiza Tanzania kwenye
maajabu ya upigaji kura wa dunia nje ya bunge.”
Kufuatia maamuzi yaliyofanywa na
bunge la katiba kupitisha rasimu hiyo iliyopendekezwa, Mnyika aliwaambia
wananchi kwenye mkutano huo kuwa watanzania hivi sasa wanao uwezo wa kuchagua
hizo rasimu mbili.
“Wakati wanafunga Bunge Maalum la
Katiba, Pinda (Waziri Mkuu, Mizengo Pinda), Makinda (Spika wa Bunge la Jamhuri,
Anna Makinda), Kificho (Spika wa Bunge la Wawakilishi Zanzibar Pandu Ameir
Kificho), Sitta (Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba) na kila anayezungumza
anasisitiza kwamba, jamani mlio nje mkienda kwa wananchi rasimu ni moja tu,
katiba iliyopendekezwa ni moja tu msiwaambie wananchi kuhusu ile katiba
nyingine,” alisema Mnyika.
Mnyika pia aliwataka wananchi wakiwa
kwenye majimbo yao hivi sasa, kuwaambia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba na
Wajumbe waliopitisha rasimu hiyo ya
Katiba bungeni kurudisha fedha walizo kula.
“Kuna aina mbili za kuwataka
warudishe fedha za wapiga kura, aina ya kwanza ni kwamba, kila ukimuona mbunge
wa CCM na Mjumbe wa Bunge Maalum mwambie ‘haramia wewe rudisha fedha zetu’, kwa
sababu wamedhamiria kuzunguka nchi nzima kuwaeleza uzuri wa rasimu yao hiyo,
sasa wakija kwenye mikutano waambieni…’maharamia nyinyi rudisheni fedha zetu’
tumeelewana wananchi,” alisema Mnyika.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema
Tanzania Bara, alisema alipokuwa anahutubia mkutano wa hadhara mkoani Mwanza
alisema alitumia neno la uharamia kwa kuwa mwaka 1958 hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere aliwaambia wakoloni wakati anadai uhuru.
“Mwaka 1958 Mwalimu Nyerere
alishtakiwa mahakamani na mkoloni, alisema wakuu wa Wilaya ya serikali ya
kikoloni ni mashetani na maharamia kwa sababu hawasikilizi malalamiko ya
wananchi, kwa hiyo wakamfungulia kesi ya kuwaita mashetani na maharamia na
akashtakiwa mahakamani na kajijitetea mahakamani ni kweli nimewaita maharamia
na mashetani kwa sababu matendo yao ya kutosikiliza malalamiko ya wananchi ni
matendo ya kiharamia na mashetani,” alisema Mnyika akimnukuu Nyerere.
“Sasa Sitta, Chenge na wenzake
anasema kwa kuwaita maharamia ni jambo la kitoto, sisi kuwaita maharamia
tunafanya siasa za chuoni hatuwezi kuchukua nchi, Mwalimu alipokuwa anafanya
mkutano wa TANU alifanya mambo ya kitoto wakati ule, nilisema Nyerere akiwa
Mwenyekiti wa TANU alipokuwa anafanya mikutano, bahati nzuri aliweza kuchukua
nchi, sasa sisi kwa kuwaita jina lao harisi kwamba ni maharamia tunafanya watu
wengi zaidi walioko wajue kwamba hawa ni maharamia ili tufanye kazi ya
kuwaondoa kwenye uongozi wa nchi kuwa rahisi zaidi,” alisema Mnyika.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la
Vijana la Chadema, (BAVICHA), Patrick Ole Sosopi akizungumza kwenye mkutano huo
alishangazwa na hatua ya Marais wastaafu wa Tanzania kwa kuwa kimya wakati wa
msuguano uliokuwepo wa Chama cha Mapinduzi na Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) juu ya rasimu ya katiba wakati wa Bunge Maalum la Katiba lililopokuwa
likiendelea.
“Tuna rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi
(Awamu ya Pili), Rais Benjamin Mkapa (Awamu ya Tatu), tunaamini ni watu wenye
busara kubwa, tunaamini kama walifikia hatua ya kuliendesha taifa hili,
tunaamini ni washauri wazuri wakutuelekeza tuende wapi, nini tufanye kama
Taifa, lakini ni watu wamekuwa waajabu sana, tunaandika katiba ya watanzania
wote bila kujali itikadi, kuna msuguano mkubwa sana wa Ukawa na CCM,
wamenyamaza kimya, hatusikii wakizungumza lolote, leo anaonekana Warioba ndiyo
mtu mzalendo kwa wapinzani, lakini Mkapa na Mwinyi wako kimya,” alisema
Sosopi.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kwamba Katiba iliyopigiwa kura na Bunge
Maalum mjini Dodoma na kupelekwa kwa wananchi, Wazanzibar hawako tayari kuipitisha.
“Zanzibar wakituletea tutaulizana
tu, yakhee ya bara hiyo hapo waachieni wenyewe, haituhusu, hatuitaki kwa sababu
haibebi maslhai mapana ya Wazanzibar, hata kufunguliwa haitafunguliwa na
tumeshawaambia na Zanzibar tumeshapewa mwelekeo, katika taifa lolote duniani,
Mwanasheria Mkuu ndiyo msimamizi, mshauri wa masuala ya sheria na katiba katika
nchi husika na ndiyo maana mikataba yote ya Tanganyika lazima ipite kwa kwa
mwanasheria mkuu, huyo amepewa mamlaka
na katiba, sasa Zanzibar tulishamaliza kazi, kupitia kwa mwanasheria Mh.
Othman Masoud Othman,” alisema Mwalimu.
Alisema Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Othman amepiga kura ya wazi hadharani na kuuonyesha ulimwengu kwamba
wanachokiandika, wanachokijadili hakina maslahi kwa Mzanzibar na kwa kura ya
wazi akapiga hapana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni