Jumamosi, 11 Oktoba 2014

KIKWETE MWELEDI PEKEE MCHAKATO WA KATIBA MPYA



Rais Jakaya Kikwete akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein wakiwa wameshikilia rasimu ya Katiba Mpya

Na Profesa Kitila Mkumbo

Mchakato wa kuandika Katiba Mpya umeingia katika hatua muhimu baada ya marais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein kukabidhiwa rasmi Katiba inayopendekezwa.

Kisheria, mchakato huu upo hatua ya mwisho ambapo sasa imebaki hatua moja tu ya Katiba inayopendekezwa kukubaliwa au kukataliwa na wananchi katika kura ya maoni. Hata hivyo, kisiasa, mchakato huu unaweza ukawa ndio mwanzo wa mwisho wake.

Wakati kisheria mchakato huu unaonekana kwenda kama ratiba ilivyopangwa na bila misukosuko mikubwa, kisiasa mchakato huu umepitia na unaendelea kukumbwa na misukusuko mingi.

Mkanganyiko huu umetokana na wanasiasa wa vyama vikubwa nchini kushindwa kukubaliana na kujenga mwafaka katika mambo ya msingi kuhusu mchakato na maudhui ya Katiba Mpya.

Pamoja na kwamba harakati za kudai Katiba Mpya zina historia ndefu, kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi, uhalisia wake ulianza kuonekana mwaka 2010 wakati Rais Kikwete alipotangaza kuwa alikuwa anakusudia kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya.

Wakati Rais anatoa tangazo hili, viongozi waandamizi ndani ya Serikali wakiwamo Waziri wa Sheria na Katiba wa wakati huo Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema walitoa kauli kwamba hapakuwa na haja ya Katiba Mpya.

Hata hivyo, mara baada ya Rais kutoa kauli yake viongozi hao ndio waliokabidhiwa jukumu la kusimamia mchakato mzima kisheria kutokana na nafasi zao serikalini.

Mpaka hapa tunaona mchakato huu ulikuwa ni mradi wa Rais Kikwete pekee katika serikali na chama chake. Hili linathibitishwa na kauli za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye kuwa Katiba siyo jambo la msingi kuliko maji kwa wananchi.

Kwa hiyo hapa tunamuona Rais Kikwete kama mtu aliyejitoa mhanga na kujivalisha ujasiri kwa kufanya jambo ambalo halipo katika chama chake na ambalo haliungwi mkono na wanasiasa wenzake katika chama na serikali.

Mara baada ya mchakato huu kuanza rasmi kwa kutungiwa muswada wa sheria, Rais Kikwete alikumbana na kizingiti kingine pale sheria hiyo ilipokataliwa na wanasiasa wa upinzani kwa maelezo kwamba ilikuwa haikidhi haja.

Kama kawaida, wanasiasa wa CCM na viongozi waandamizi wa serikali wakalazimisha muswada kuingia bungeni.

Kutokana na wingi wa wabunge wa CCM, muswada ule ulipita kama ulivyo na Rais Kikwete akausaini kuwa sheria bila kujali kelele nyingi zilizokuwa zikiupinga.

Hata hivyo, wanasiasa wa upinzani walitishia kususia mchakato mzima kama sheria iliyopitishwa isingerekebishwa.

Pamoja na mambo mengine, madai makubwa ya wanasiasa wa upinzani na baadhi ya wanaharakati ilikuwa ni kwamba Rais asiwe na mamlaka ya kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kwa mara nyingine, wakati wanasiasa wa CCM wakiisifia sheria iliyopitishwa, Rais Kikwete akawaita wapinzani ili kujadiliana kuhusu matakwa yao.

Wakakutana Ikulu mara kadhaa na baadaye kuutangazia umma kwamba wamefikia mwafaka na sasa mchakato wa Katiba ungeendelea baada ya sheria kufanyiwa marekebisho. Hata hivyo, marekebisho yaliyofanyika yalikuwa ni ya kisarufi zaidi kuliko maudhui.

Hii ni kwa sababu mambo yote makubwa ambayo wanasiasa wa upinzani walikuwa wanayadai hayakubadilishwa.

Rais Kikwete aliendelea kuwa na mamlaka ya kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Kilichobadilika pekee ni kwamba vyama vya siasa na wadau wengine wangependekeza majina kwa Rais Kikwete lakini yeye ndiye ambaye angeteua wajumbe. Kwa mara nyingine tena Rais Kikwete akawa ameibuka ‘mweledi’ kwa kufanikiwa kuwashawishi wanasiasa wa upinzani kukubaliana na mchakato bila madai yao ya msingi kutekelezwa.

Kwa hiyo, tangu mwanzao mchakato wa Katiba ulishatekwa na CCM kwa muswada wa viongozi wa upinzani ambao waliubariki utekaji huo kwa gharama ndogo ya kukutana na Rais Kikwete.

Rais Kikwete anaelekea kuibuka shujaa tena kwa kuacha suala la kura ya maoni likielea. Utabiri wangu ni kuwa katika kipindi cha sasa na Bunge kukaa Novemba, CCM watafanya tafakuri kuangalia mazingira mazuri zaidi kwao ya kupitisha Katiba kupitia kura za wananchi. Wanasiasa wetu wangekuwa na nia njema na dhamira ya kweli wangerekebisha sheria ya mabadiliko ya Katiba ili kuruhusu mambo mawili.

Mosi, kuruhusu kura ya maoni ifanyike baada ya uchaguzi mkuu tukitarajia kwamba katika kipindi hiki tutapata nafasi ya kutibu majeraha ya kisiasa yaliyojitokeza.

Pili, kuruhusu kuundwa kwa tume ya kitaalamu itakayohusisha wajumbe kutoka ndani na nje ya nchi. Kazi ya tume hii ingekuwa ni ‘kusafisha’ Katiba inayopendekezwa kwa kupitia kwa makini hoja zilizojitokeza kwenye Rasimu na ambazo zimetupwa na zile zilizojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba.

Tume hii pia ingeweza kukaa na wanasiasa wa pande mbili zinazosigana ili kuwasuluhisha na kufikia mwafaka katika mambo ya msingi bila kuvuruga mchakato. 

Yote haya yatategemea na hatua zitakazochukuliwa na Rais Kikwete ambaye, kwa maoni yangu, ndiye mweledi pekee aliyekwishaonekana katika mchakato huu miongoni mwa wanasiasa wetu.

Chanzo: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni