tRAFKI WALIONASWA WAKIWA KAZINI!
NA RENATHA
KIPAKA, BUKOBA
JESHI la Polisi mkoani Kagera
limewafukuza kazi askari wake watatu kwa kulifedhehesha jeshi hilo kutokana na
kitendo cha kupiga picha inayowaonyesha wawili kati yao wakinyonyana ndimi
wakiwa kazini.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, alisema kitendo
kilichofanywa na askari hao kimeshusha hadhi ya jeshi.
Aliwataja askari hao waliofukuzwa ni
F.7788 PC Mpaji Mwasumbi, G 2122 PC Fadhili Linga na WP.8898 Veronica Mdeme
ambao wote ni wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Misenyi.
Alisema PC Mpaji na WP Veronica
walipiga picha inayokwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Polisi wakiwa kazini,
huku PC Fadhili akiingia matatani kwa kuwapiga picha hiyo chafu askari wenzake
na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Kamanda Mwaibambe alisema picha hiyo
ilianza kuonekana katika mitandao mbalimbali ya kijamii mapema wiki hii.
Alisema askari PC Fadhili alipiga
picha hiyo mwaka 2012 kwa kutumia simu yake ya kiganjani na kuitunza, lakini
wiki hii aliamua kuisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kitendo
ambacho ni kinyume na kazi yake.
“Napenda kuthibitisha kuwa picha hii
iliyoonekana kwenye mitandao ya kijamii ni picha halisi ambayo
haijachakachuliwa kabisa.
“Maadili ya kijeshi yapo kisheria na
askari wetu wanafundishwa namna ya kuishi katika maisha ya utumishi wa jeshi na
si vinginevyo.
“Jeshi halikubaliani na vitendo hivi,
ikitokea askari kwenda kinyume lazima achukuliwe hatua kali,” alisema Kamanda
Mwaibambe.
Taarifa zaidi kutoka mkoani Kagera,
zinaeleza baada ya kusambazwa kwa picha hiyo na kuonekana katika mitandao ya
kijamii, WP Veronica alianguka ghafla na kupoteza fahamu kwa mshtuko wa tukio
hilo.
Kutokana na hali hiyo, majirani
waliokuwa karibu na nyumbani kwake walilazimika kumpatia msaada na kumkimbiza
hospitali kwa matibabu, ambako aliruhusiwa juzi jioni kabla ya kutiwa mbaroni.
DAR ES SALAAM
Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewahamisha askari wake, WP 5863 Quine
na WP 3548 Koplo Maeda kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Ilala kwa
kukiuka maadili ya kazi.
Taarifa ya ndani ya Oktoba 2, mwaka
huu ya Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu Dar es Salaam iliyosambazwa
kwenye mitandao ya kijamii, imesema askari hao walisimamisha gari dogo na baada
ya dereva kujitetea, waliendelea kutafuta makosa hali iliyosababisha abiria
aliyekuwa mgonjwa kufariki.
Kutokana na tukio hilo, makamanda wa
polisi wa wilaya zote za Mkoa wa Kipolisi wa Dar es Salaam wametakiwa kuwakumbusha
askari wao kuepuka kutolazimisha kutafuta makosa ambayo hayana madhara.
“Makosa ambayo hayana madhara katika
kusababisha ajali mfano ni vifaa vya kuzimia moto, rangi, kadi kutoandika
anuani, motor vehicle, leseni chini ya siku 30 na kadhalika,” lilisomeka agizo
hilo kwa makamanda hao wa polisi.
CREDIT: MTANZANIA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni