Na Beatrice Lyimo, Maelezo-DSM
WAZIRI wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika Harambee ya kuchangia kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu vyumba vya
madarasa na ununuzi wa samani katika shule ya Sekondari ya Enaboishu iliyopo
mkoani Arusha.
Hayo yamesemwa na
Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, Bw. Emmanuel Munga wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi leo jijini Dar Es Salaam.
Munga amesema kuwa
Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya tarehe 25 Oktoba mwaka huu katika
shule hiyo wilayani Aremure mkoani Arusha ambapo Kauli mbiu ya harambee hiyo ni
‘penye nia pana njia’.
Alisema kuwa,
katika harambee hiyo wamewashirikisha wanafunzi wote waliosoma katika shule
hiyo wakiwemo wazazi, viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya siasa,
Mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau, shule za jirani na wananchi kwa ujumla.
“katika harambee
hii tunatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 na fedha
zitakazopatikana zitatumika kutatua changamoto zinazozikabili shule”,
alisisitiza Munga.
Akizungumzia kuhusu
changamoto zinazoikabili shule hiyo alisema kuwa, shule hiyo yenye mchanganyiko
wa wanafunzi wa kike na wakiume iliyoanza mwaka 1966 inakabiliwa na changamoto
za nyumba za walimu, nyumba za madarasa, mabweni ya wanafunzi na maabara.
Ameongeza kuwa
shule hiyo imetoa baadhi ya viongozi wakubwa waliopo serikalini wakiwemo Naibu
Waziri wa Tamisemi Mhe. Agrey Mwanri na Naibu Katibu wa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni