Watoto wa kituo cha chekechea wakisoma risala yao mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe
Na Michael Katona, Ludewa
MBUNGE wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe akiwa
katika kituo cha watoto wa chekechea kilichopo Kata ya Madilu, wilayani Ludewa,
mkoani Njombe alijikuta akitokwa na machozi kufuatia watoto wanaosoma kwenye
kituo hicho kusoma risala yao huku ikimkumbusha msiba wa baba yake.
Filikunjombe ambaye alitembelea kituo hicho chenye
watoto wenye umri usiozidi miaka minne Agosti 16, mwaka huu kufuatia kuombwa
kufanya hivyo na mlezi wake anayeishi nchini Italia, Usula Mtewele.
Akiwa kwenye kituo hicho, Mbunge Filikunjombe
alikaribishwa na watoto hao kwa risala iliyosomwa na watoto hao, ambapo jambo
ambalo lililovuta hisia na kumkumbusha mbali mbunge huyo ni pale watoto hao walipomkabidhi
shada la maua na kumuomba alipeleke na kuliweka juu ya kaburi la marehemu baba
yake, Florian Haule Filikunjombe aliyefariki mwezi Mei, mwaka huu.
“Watoto wa Mungu asanteni sana, kuna kitu hamjasema
hapa kwenye risala yenu, mmesema vitu vingi mmenipa pole nimetoa machozi kwa
msiba wa baba yangu, nilikuwa na furaha, mmeniharibia furaha yangu,
nimehudhunika kwa sababu wamesema watoto,” alisema Filikunjombe.
Katika risala yao waliyoisoma watoto hao, walisema wanampa pole mbunge huyo kwa
kuondokewa na babu yao marehemu mzee Florian Filikunjombe.
“Tunakupa pole sana kwa kuondokewa na baba yako mzazi,
kwetu sisi alikuwa babu yetu, Mungu
ailaze mahari pema peponi,” walisema watoto hao kwenye risala yao hiyo.
Aidha katika risala yao hiyo, watoto hao walimwambia
mbunge Filikunjombe kwamba kituo chao kinakabiriwa na changamoto kubwa ikiwepo ya
wazazi wa kata hiyo kushindwa kuwapeleka watoto wenzao kwenye kituo hicho, na
badala yake wamekuwa wakicheza katika sehemu mbalimbali za hatari hususan
barabarani, huku wazazi hao wakidai ni gharama kubwa kusomesha watoto kwenye
kituo hicho.
Mbali na kilio chao hicho, pia walisema kituo chao
hakina vifaa vya michezo kama vile, bembea, na kudai wazazi wao wameshindwa
kuwanunulia wakidai wanakabiriwa na ujenzi wa jengo la Kanisa Katoliki kigango
cha Madilu na tayari wameshajenga msingi sambamba na kununua mbao. Kanisa hilo
mara litakapo kamilika lita gharimu shilingi milioni tano.
Pia watoto hao kwenye risala hiyo, walimuomba Mbunge
Filikunjombe mwakani agombee kiti cha Ubunge kwenye Jimbo la Ludewa na baadaye
mwaka 2020 wananie kinyang’anyiro cha kiti cha Urais.
Naye Filikunjombe akijibu maombi ya watoto, aliahidi
kuwasaidia huku akiwasifu watoto hao kwa bidii yao kubwa ya kusoma, huku akiwataka
watoto hao wakawaambie wazazi wao wasigombee ubunge kwa sababu yeye bado
hajachoka kuongoza wananchi wa jimbo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni