Mratibu wa kampeni ya Bwela Kuni, Raymund Mhenga (wa kwanza kushoto)
akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuzungumzia Kampeni
ya Bwela Kuni zinazotarajia kunadi fursa anuai zilizopo katika mkoa wa
Ruvuma.
Mhamasishaji wa Utalii na Maliasili katika Kampeni ya Bwela Kuni,
Bakari Likapo (wa pili kulia) akizungumza katika mkutano na wanahabari.
Produza C9 (katikati) akizungumza na wanahabari kuzungumzia Kampeni ya
Bwela Kuni na Wimbo Maalum aliouandaa kuzungumzia Mkoa wa Ruvuma.
Baadhi ya vijana na washiriki wa Kampeni ya Bwela Kuni katika mkutano na wanahabari.
Baadhi ya vijana wasanii walioimba wimbo maalum wa Kampeni ya Bwela
Kuni unaousifia Mkoa wa Ruvuma wakitoa kionjo cha wimbo huo katika
mkutano na wanahabari. Baadhi ya vijana na wasanii pamoja na viongozi wa Kampeni ya Bwela Kuni wakiwa katika picha ya pamoja.
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
BAADHI
ya Vijana kutokea Mkoa wa Ruvuma wakishirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo wameandaa kampeni maalum ya kunadi fursa anuai zilizopo katika
mkoa huo kupitia sanaa ya muziki kwa kuwashirikisha wasanii na vijana
wenye vipaji.
Kampeni
hizo zilizopewa jina la 'BWELA KUNI' neno la lugha ya Kingoni lenye
asili ya mkoa huo likiwa na maana ya 'njoo hapa' zitazinduliwa rasmi
mwishoni mwa Septemba, 2014 kwa tamasha kubwa litakalofanyika katika
Uwanja wa Maji Maji mjini Songea hivi karibuni.
Akizungumzia na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa kampeni
ya Bwela Kuni, Raymund Mhenga alisema kampeni hizo zilizo na lengo la
kunadi fursa anuai za uwekezaji zinazopatikana eneo hilo kwa
kushirikisha vijana wasanii zitashirikisha makundi anuai ya sanaa
ikiwemo sanaa muziki wa kizazi kipya, injili, uigizaji.
"...Hii
ni kampeni maalum iliyoanzishwa na vijana wanaotokea na wenye asili ya
Mkoa wa Ruvuma wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi kipya, wasanii
wamuziki wa injili, waigizaji na wasanii wengine wa kada tofauti tofauti
kwa madhumuni ya kuamsha ari na hamasa ya wananchi wa mkoa huu na wenye
asili ya mkoa huu na Watanzania kwa ujumla kuweza kutangaza sifa za
mkoa wetu...," alisema Mhenga.
Alisema kampeni hiyo pia itatangaza historia ya Mkoa wa Ruvuma, tamaduni
za watu wake na fursa mbalimbali zinazopatikana eneo hilo kwenye sekta
ya kilimo, utalii, biashara, elimu na uvuvi kupitia sanaa.
"...Hii
pia itakuwa ni fursa ya pekee kwa wasanii watakaoshiriki kwenye kampeni
kuweza kutangaza vipaji vyao na uwezo hivyo kutambulika kitaifa na
kimataifa," alifafanua Mhenga.
Alisema kampeni hiyo kwa kuanza imewaunganisha wasanii vijana wenye
asili ya Mkoa wa Ruvuma na kuandaa wimbo unaojulikana kama "Bwela Kuni"
ambao pia umeandaliwa na Produza mwenye asili ya mkoa huo maarufu kwa
jina la C9 Kanjenje na tayari umetolewa kuchochea kampeni hizo.
Aidha
Mhamasishaji wa Utalii na Maliasili katika kampeni hizo, Bakari Likapo
alisema kampeni hiyo imekusudia kubainisha vivutio na fursa za uwekezaji
zinazopatikana katika Mkoa wa Ruvuma ikiwemo vituo vya makumbusho ya
taifa (Vita vya Majimaji), Mbuga ya Wanyama Selous, utamaduni wa jamii
ya wakazi wa eneo hilo pamoja na kuhamasisha wawekezaji kutumia fursa
hizo.
Alisema
Mkoa huo una Ziwa Nyasa, upatikanaji wa madini mbalimbali na fursa za
kilimo kupitia ardhi yenye rutuba jambo ambalo likitangazwa na
wawekezaji kujitokeza linaweza kuchochea kasi ya maendeleo ambayo
yatawanufaisha zaidi wananchi wa eneo husika na taifa kiujumla.
Hata
hivyo, Likapo aliwataka viongozi wa Serikali na wanasiasa pamoja na
wadau wengine wapenda maendeleo kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo
za vijana wa Ruvuma na wasanii za kuchochea maendeleo kupitia sanaa ya
muziki.
Miongoni mwa wanamuziki vijana 15 ambao wameshiriki kuimba mwimbo wa
hamasa ya kampeni ya Bwela Kuni ni pamoja na Herieth Ndosi (toka muziki
wa injili), Single J, G Luck, Cammy Bway, Roby Songea, Gemy Rymez,
Fobyone, Bad H Badilika, G Van, Zero Wiz, FM, HDM, Full P, Tony na D
Pesa.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni