Na Nickson Mahundi, Ludewa
Wakulima wa Matunda
wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wameanza kujipanga na kilimo cha mazao
hayo ili kuwauzia wawekezaji wa machimbo ya Chuma cha Liganga na Makaa ya mawe
Nkomang’ombe ambao wanatarajia kuwasili wilayani humo hivi karibuni.
Akizungumza na mwandishi
wa habari, mmoja wa wakulima hao ambaye anaishi katika kijiji cha Mkongobaki
wilayani hapa mzee Edward Mligo (69) alisema kutokana na hali inavyoonesha ya
upanuzi wa barabara za maeneo ya migodi inavyoendelea wakulima wengi
wamehamasika kujiandaa kwa biashara.
Mligo alisema mpaka sasa
yeye binafsi ameweza kupanda miti ya matunda aina ya Machenza na Machungwa
ipatayo mia tatu ambayo tayari imeshanza kuzaa matunda na ameshaandaa shamba
jingine lenye ukubwa wa hekari 5 kwa ajili ya kupanda miche ya matunda hayo
ambayo imeshandaliwa.
Hata hivyo amewataka
vijana kuacha tabia ya kukaa vijiweni bila kazi badala yake wajikite katika
shughuri za uzalishaji mali ikiwemo kilimo cha matunda na ufugaji ambao utawapa
utajiri wa miaka mingi ijayo tofauti na wanavyotarajia.
“Tunaishukuru Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuikumbuka wilaya ya Ludewa kwani tumeanza
kuona dalili za kufanikisha machimbo ya madini yetu kutokana na barabara
zinazoelekea migodini kuanza kupanuliwa tofauti na awali tulikua tukipewa
maneno matupu pasipo vitendo”, alisema Mligo.
Hivi karibuni Serikali
kupitia wakala wa barabara nchini TANROAD wameweza kutiliana saini na wakandarasi
wanne kwa gharama ya kiasi cha shilingi 7.8 bilioni ili kuzipanua barabara za
wilaya ya Ludewa na kuweka changalawe kwa ajili ya upitishaji wa mitambo ya
migodini.
Ukarabati wa barabara hizo
umewaamsha wakulima na wafugaji walioko wilayani Ludewa kujianda na ugeni wa
wawekezaji ambapo baadhi ya wakulima wa matunda akiwemo mzee Mligo wamekuwa
wakishinda mashambani ili kuhakikisha wanatumia fulsa ya kilimo kujipatia
kipato kwa wawekezaji hao.
Aidha wadau mbalimbali wa
maendeleo wilayani Ludewa akiwemo Huruma Mgaya wamesifu mpango wa Serikali
pamoja na Mbunge wa jimbo la Ludewa Mh. Deo Filikunjombe kwa kazi nzuri ya
ujenzi wa barabara za lami katika mitaa ya Ludewa mjini na upanuzi wa barabara
kuu kutoka Njombe hadi Ludewa.
Mgaya alisema hali ya
upanuzi wa barabara kuu hutaharakisha maendeleo wilayani humo ingawa wananchi
walio wengi wanashauku ya kuwa na barabara ya lami itakayounganisha wilaya ya
Ludewa na ile ya Njombe kwani msimu wa mvua kiwango hicho cha changalawe
huharibika vibaya.
Aliwataka wanaludewa
wanaoishi mbali kuchangamkia fulsa za uwekezaji wilayani humo mapema kabla
wageni hawajanza kufanya mambo yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni