Jumatatu, 4 Agosti 2014

UKAWA WAWATIA KIWEWE WASSIRA, MWIGULU, LUKUVI


Moshi/Dar. Mawaziri Stephen Wassira na Mwigulu Nchemba wamesema kuwa japo Bunge Maalumu la Katiba litaendelea na vikao vyake kuanzia kesho mjini Dodoma, halitakuwa na uhalali wa kisiasa.

“Tunakwenda bungeni kuendelea na vikao kwa sababu hatuvunji sheria. Kumbukeni hata walipotoka (Ukawa) wakati ule tuliendelea na vikao kwa sababu akidi inaruhusu, japo hatutakuwa na uhalali wa kisiasa lakini kisheria tuna uhalali,” alisema Wasira ambaye ni Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais, Uratibu na Uhusiano).
Hoja hiyo ilisisitizwa na Nchemba ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha kuwa vikao hivyo havitakuwa na uhalali wa kisiasa japo kisheria vina uhalali.

“Unajua kilichosababisha mkwamo huu ni kila kundi kushikilia upande wake, kama kila kundi lingeweka masilahi ya Taifa tusingefika huko. Tunakwenda bungeni, ingawa hakutakuwa na uhalali wa kisiasa lakini tutaendelea kujadili mambo ya kitaifa,” alisema Mwigulu.

Viongozi hao walisema hayo baada ya mdahalo wa Katiba uliofanyika Dar es Salam jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akisema wanakwenda bungeni kuendelea na mijadala japo katiba haitakuwa na afya... “Nawaomba Ukawa warejee bungeni, ikishindikana sisi tutakwenda, tutajadiliana, tutawaletea Katiba bora ila haitakuwa na afya bila Ukawa.”

Wengi waendelea kupinga Bunge
Mbali na mawaziri hao, idadi ya wajumbe wa Bunge hilo wanaopinga vikao hivyo kuendelea bila kushirikisha wenzao wa Umoja wa Bunge la Wananchi (Ukawa) inazidi kuongezeka.

Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki vikao hivyo.

Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki vikao hivyo.

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema jana kuwa haungi mkono mpango wa wabunge wenzake wa CCM kuendelea na Bunge la Katiba bila maridhiano.

“Pengine niwakumbushe wabunge wenzangu wa CCM kuwa kinachoandaliwa kwenye Bunge la Katiba ni Katiba ya Watanzania wote na si Katiba ya CCM. Hatua tuliyofikia siiungi mkono, kitendo cha wabunge wenzangu wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu suala la Katiba halina mshindi ni jambo la maridhiano.

“Kitendo cha sisi wabunge wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya ni matumizi mabaya ya wingi wetu mle bungeni. Ni kweli CCM ina wabunge wengi na ni kweli kwenye demokrasia wengi wape, lakini pia demokrasia pevu na yenye tija ni ile inayoheshimu na kuyafanyia kazi maoni ya wachache.”

Isome zaidi: http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Ukawa-wawatia-kiwewe-Wassira--Mwigulu--Lukuvi/-


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni