- Ahaidi kusaidia mapambano dhidi ya VVU
- Mama Maureen: Tusizuie ndoto za watoto wetu
Na Michael Katona, Njombe
“Msichana
kushiriki mashindano ya urembo, si uhuni, na sidhani kushiriki urembo ni
kukiuka maadili, ni mchezo kama ilivyo michezo mingine,” anasema Maureen
Godfrey, akiwa amekaa na mama yake, Maria Itala, wakati alipofanya mahojiano
maalum hivi karibuni.
Maureen,
akiwa Miss Redds Mkoa wa Njombe, alifanikiwa kutwaa taji la Miss Redds Nyanda
za Juu Kusini baada ya kuwashinda warembo wengine kutoka mikoa ya Iringa,
Mbeya, Ruvuma, na Rukwa.
Ni jambo
la kujivunia katika Mkoa mpya wa Njombe kutokana na ukweli kwamba ni mara ya
kwanza kufanya shindano la kumtafuta mrembo wa mkoa. Pia Njombe kama mkoa imeshiriki
kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kumtoa mshindi wa kuwakilishi kanda ya Nyanda
za Juu Kusini katika shindano kuu la kumtafuta Miss Redds Tanzania mwaka 2014.
“Tatizo
kubwa ni mtazamo uliopo hivi sasa kwa jamii kuwa warembo wanapovaa pale jukwaani
nusu uchi, ndivyo wanachukulia kwamba mashindano hayo ni ya kihuni, lakini si
hivyo, ila ni mrembo mwenyewe inategemea amelelewa namna gani na wazazi wake,”
anaongeza kusema Maureen.
Mbali na
kuwahimiza wazazi wa mkoa wa Njombe kuwaruhusu mabinti zao kupenda kushiriki
mashindano hayo ya urembo, Maureen anasema akiwa balozi wa mkoa wa Njombe
kwenye mashindano ya kumsaka Redss Miss Tanzania mwaka huu, ataendeleza kampeni
ya serikali kuhamasisha jamii kupitia kwa warembo wenzake kupiga vita maambuki
ya virusi vya Ukimwi (VVU).
“Hili
suala la ugonjwa hatari wa Ukimwi, sitakuwa nyuma katika kulipigia kampeni ili
warembo wenzangu pia watambue kwamba ni hatari kwa jamii, nitakapokuwa kambini,
nitasimama na kutoa ushauri nasaha, elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi,”
anasema Maureen.
Akizungumzia
changamoto ambazo mkoa wa Njombe imekuwa ikishindwa kutoa warembo kutokana na
wazazi wengi kutokuwa na mwamko wa kuwaruhusu mabinti zao wanaotaka kushiriki,
mama yake mzazi, Itala aliwaasa wazazi wenzake kuachana na imani potofu kuwa
urembo ni uhuni.
“Sioni
mantiki ya wazazi wenzangu mkoani Njombe na sehemu nyingine kuwakataza warembo
wanaotaka kushiriki mashindano, ni wajibu wao sasa wajue msichana anapoguswa kutaka
kushiriki wasimzuie,” anasema Itala.
Mama huyo
mzazi wa Maureen alitolea mfano alivyofanya kwa mwanae kwa kuamua kumruhusu
kushiriki mashindano hayo na hatimaye kushinda taji la Miss Njombe na
kuwakilisha Nyanda za Juu Kusini.
“Mwanangu
alikuja na kunieleza mama mimi nataka kujaribu kushiriki Miss Njombe, bila
hiyana nilimruhusu ashiriki na nilikwenda kushuhudia mashindano, sikuamini
wakati matokeo yanatangazwa kwamba mwanangu ndiye Miss Njombe,” anasema Itala.
“Hata
alivyokuwa anafanya mazoezi sikuwa na matarajio yoyote, inashangaza sana na
hata tulipokwenda kumpa ‘sapoti’ katika mashindano ya Nyanda za Juu Kusini,
nako pia nilijikuta nashangazwa ni bahati gani mwanangu ameipata,” anasema
Itala.
Mzazi
huyo wa Maureen aliwataka wazazi wasiwe wazito kuwatoa mabinti zao pale
wanapohitaji kushiriki mashindano hayo, na kwamba jambo la muhimu ni kuwatia
moyo katika mashindano hayo.
“Maureen
aliniomba niende kuangalia tukio la Miss Kanda, na akanieleza tukija sisi
wazazi na marafiki tutamtia nguvu na kufanya vyema, lakini ni maajabu kweli
binti yangu amefanya vyema tena katika shindano hilo,” anasema Itala.
“Kitu
cha msingi na rai yangu kwa wazazi wenzangu ni kuona ni jinsi gani ambavyo amempa
msingi mtoto wake wa kike kutoka awali, kwani mashindano hayo yanalenga kumpa
uelewa endapo atashinda basi yeye ndiyo kioo cha jamii,” aliongeza Itala.
Aidha
mama Maureen anasema binti yake tangu ashiriki mashindano hayo anaamini ulikuwa
ni ushindani, lakini jambo ambalo anapaswa kuliendeleza kwa binti yake ni
kumkanya asipotoke kwenye maadili aliyokuwa ametoka kwa kujitambua, eti hivi
sasa yeye ni mrembo maarufu.
“Najaribu
kumuasa na kumwangalia mwenendo wake, lakini hii yote ni kumchunga asipotoke,
na mweleza wewe ni mtoto wa kike unatakiwa kujiheshimu na kujijali na
kujitambua katika jamii, tatizo wazazi wengi hasa sisi Waafrika hatuna tabia ya
kumuambia mtoto wa kike wazi ni madhara gani anayoweza kuyapata endapo
atajiingiza katika mapenzi akiwa mdogo,” anasema.
Mzazi
huyo aliwataka wanawake hususan wazazi wa Njombe kuiga mfano alioufanya yeye,
wajitoe kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki katika mashindano hayo kwa kuwa
yanafaida kwa msichana.
“Mbali
na kupata faida yake binafsi, mtoto wangu ameweza kutambulika, lakini pia
mashindano hayo yanaleta sifa ya mkoa alikotoka, mfano ameuletea sifa mkoa mpya
wa Njombe, lakini pia ameweza kupiga hatua ya kuwa Miss Nyanda za Juu Kusini,”
anasema Itala.
Mrembo Maureen
ambaye kabila lake ni Mnyakyusa, akizungumzia historia yake ya masomo, anasema
elimu ya msingi alianza kuipata kupitia shule ya Arage iliyopo Jijini Mbeya, ambapo
baadaye alijiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya St. Marys
iliyopo pia jijini Mbeya.
Baada ya
kuhitimu kidato cha nne, hakuweza kufanya vyema na hivyo wazazi wake walimtaka
ajiendeleze kwa kuamua kujiunga na masomo katika Chuo cha Tumaini kilichopo
Iringa ambapo alichukua masomo ya Biashara, na hivi sasa ni mwaka wake wa
mwisho wa kuhitimu masomo hayo ngazi ya Diploma.
Mrembo Maureen
katika mashindano ya Redds Miss Tanzania ataiwakilisha Njombe, wakati mrembo
Martha John ambaye ni Miss Iringa 2014 na Naba Magambo Miss Ruvuma 2014, ndiyo
watakaowakilisha Nyanda za Juu Kusini
kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mtazamo na ushauri: Piga namba 0753-827444
Email:princemichaelkatona@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni