Alhamisi, 31 Julai 2014

DC Dumba: Maureen nenda kashiriki Redds Miss Tanzania kwa kujiamini



Na Mwandishi Wetu, Njombe

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba amemtaka mrembo wa Nyanda za Juu Kusini, Maureen Godfrey, kujiamini na kusimama kidete pale atakaposhiriki shindano la kumsaka mrembo wa Redds Miss Tanzania wakati akiuwakilisha mkoa wa Njombe katika shindano hilo.

Dumba alisema mrembo Maureen anayosababu ya kufanya vyema kwenye shindano hilo kwa sababu wananchi wa Njombe wako nyuma yake.

“Mimi binafsi ningependa kukuambia mrembo Maureen kuwa unakwenda kushiriki kwenye shindano la Taifa huku ukijua kuwa unayo sapoti kubwa ya watu wa Njombe nyuma yako, kwa sababu Wananjombe wana kiu kubwa ya kuona unawawakilisha vyema kwenye shindano hilo,” alisema Dumba.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema hayo wakati wa sherehe ya kumpongeza mrembo huyo iliyoandaliwa na wakazi wa mkoa huo na kufanyika katika ukumbi wa Turbo uliopo mjini hapa.

Dumba alisema wakazi wa Njombe wamekuwa na kiu hiyo kubwa, baada ya kuona mkoa wao haujaweza kutoa mwakilishi yoyote aliyeweza kushiriki fainali hizo za kumsaka mrembo wa Tanzania tangu zilipoanzishwa.

“Maureen unapaswa kwenda kushiriki mashindano hayo huku ukijiamini, ukijua kwamba unayo sapoti kubwa ya watu wa Njombe, bila shaka kuna jambo lililokusukuma wewe Maureen kushiriki shindano la urembo, hivyo uwe msingi mwingine wakati wa maandalizi yako ya kunyakua hilo taji la Taifa,” alisema Dumba.

“Hakuna lisilowezekana, kila jambo lina wezekana na mimi nina amini kwa kuwa umeanza vyema, basi utaweza kumaliza vyema, kufuatia sapoti ya watu wa Njombe, dua zao, baraka zao na kheri zote ambazo wanakutakia ili uweze kuwawakilisha,” alisema.

Mkuu huyo alisema masuala ya ulimbwende ndiyo ambayo yamewaibua baadhi ya wasichana wengi kwenye nyanja za kimataifa na wakaweza kupata fursa nyingi, hata kama hawakufanya vyema kwenye shindano la Mrembo wa Dunia, lakini baadhi yao walitafuta maendeleo ya aina mbalimbali kulingana na matarajio na utashi kwa jinsi walivyojipanga.

“Wakati Maureen unapata masomo yako kule Chuo Kikuu, lakini vilevile ujiwakilishe wewe mwenyewe kwa kutafuta fursa zingine katika mataifa na taifa letu zitakazo kufanya wewe uweze kujipatia maisha yako kwa namna vile unavyopenda mwenyewe,” alisema Dumba.


Maureen ndiye mrembo wa kwanza kuuwakilisha mkoa wa Njombe katika shindano la Redds Miss Tanzania, baada ya kushinda mataji ya kuwa Mrembo wa Njombe na hatimaye kushinda taji la pili la mrembo wa Nyanda za Juu Kusini kwa mwaka 2014/15.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni