Na Demetrius Njimbwi - Jeshi la Polisi,Dodoma
Mkuu wa Dawati la Jinsia Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Adolfina Chialo, amewataka askari wote nchini hususan wale waliopo katika dawati la jinsia kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Hayo aliyasema jana wakati akifunga semina ya mafunzo ya siku tano yaliyotolewa kwa Maafisa na askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wadau wa Jeshi hilo katika mkoa wa Dodoma, wilaya ya Kongwa, ambapo washiriki hao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kushughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto.
Kamishna Chialo, alisema kuwa, ili kutokomeza makosa yatokanayo na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto, ameihasa jamii kutofumbia macho uovu au aina yeyote ya ukatili na badala yake kuripoti jambo hilo mahala husika au katika madawati ya jinsia ya Polisi katika kituo chochote cha Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa huku akiitaka jamii kuimarisha ulinzi dhidi ya mtoto ikiwa pamoja na malezi bora.
Hata hivyo, akisoma lisala mbele ya mgeni rasmi na kwa washiriki wa semina ya mafunzo hayo, Albert Bilia, ambaye pia ni mshiriki katika mafunzo hayo amesema kuwa, kutokana na mafunzo waliyopatiwa yatasaidia zaidi katika kukabiliana na makosa ya ukatili na unyanyasaji ikiwa pamoja na vitendo viovu vinavyofanyika katika jamii husika alisema.
Alisema kuwa, mafunzo haya pia yatasaidia kuongeza weledi uelewa na ufanisi kwa askari Polisi pamoja na wadau wengine walioshiriki mafunzo haya mahakama, waalimu, Ustawi wa jamii pamoja na madaktari, ambao tayari wamezifahamu sheria na mikataba mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwa pamoja na sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ya Tanzania Bara na sheria ya mtoto ya mwaka 2011 ya visiwani Zanzibar.
Aidha, kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, amewataka maofisa pamoja na askari Polisi na wadau waliopatiwa mafunzo haya kuitumia vyema elimu waliyopewa katika kutanzua na kubaini viashiria vyote vinavyosababisha ukatili kwa jamii huku akiwaasa wananchi kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikichangia vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika familia alisema.
Kamanda, Misime, aliongeza kuwa, lengo kuu la mafunzo haya ni kujenga uelewa wakati wa kumuhudumia muathiliwa wa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji huku akisisitiza suala la utoaji wa huduma bora kwa wateja na kuhakikisha kuwa elimu hiyo inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa alisema.
SATURDAY, AUGUST 16, 2014 ~ COPYRIGHT: MICHUZI BLOG ~ MTUMIE RAFIKI YAKO , MAONI: 0
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni